Saturday, January 13, 2018

Mwalimu Nyerere na Vyama vya Upinzani

Ninakumbuka jinsi mchakato wa kuanzishwa kwa vyama vya siasa Tanzania ulivyokuwa. Hapa simaanishi vyama vya ile miaka ya Uhuru, bali miaka hii ya CCM. Mchakato ulisukumwa na mambo kadhaa, yakiwemo mabadiliko ya ulimwengu na msukumo kutoka katika jamii ya wa-Tanzania.
Kati ya watu waliosukuma mchakato huu kutoka ndani ya Tanzania ni Mwalimu Nyerere. Alifanya hivyo kutokana na kukerwa hadi kuchoshwa na tabia ya CCM, ya kujisahau na kuwa ni chama kilichoingiwa na kansa na ubovu katika uongozi wake. Mwalimu Nyerere mwenyewe aliandika katika kitabu chake, "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania," kuwa ubovu wa uongozi wa CCM ndio ulimfanya ahamasishe uwepo wa vyama vingi. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa kuwepo kwa vyama vya upinzani kungeweza kuinyoosha CCM.
Lakini CCM haikuwa na msimamo huo. Tangu vilipoanzishwa vyama vya upinzani, CCM ilikuwa inajaribu kwa kila namna kuvihujumu. Kwa mfano, ninakumbuka kwamba Lyatonga Mrema alikuwa kiongozi wa upinzani aliyependwa sana. Katika mikutano yake, wanachama wake walikuwa na tabia ya kusukuma gari lake baada ya mikutano, kama ishara ya mapenzi yao kwake.
CCM walikuwa wakizuia wanachama wale wasisukume gari la Mrema. Mwalimu Nyerere aliwakanya CCM, akasema kuwa wawaache watu wasukume gari. Hicho ninachosema ni ukweli.
Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa na msimamo wake wa kutetea vyama vya upinzani, ingawa yeye mwenyewe aliendelea kuwa mwana CCM. Katika kitabu hicho cha "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania" (uk. 66), Mwalimu Nyerere alitamka wazi kuwa kutokana na ubovu wa CCM, alitamani kipatikane chama bora cha upinzani ili kiongoze nchi badala ya CCM.
Wazo hili la chama kingine kuongoza nchi halijawahi kukubaliwa na CCM, hadi leo. Badala yake, CCM imezidisha nguvu ya kuvihujumu vyama vya upinzani. Leo hii, CCM inatumia polisi wazi wazi, kinyume kabisa na sheria ya vyama vya siasa. CCM imekwenda mbali sana, na leo inawaona wapinzani kama si wazalendo. Inatisha kwamba tumefika hapa.
Ninawashauri wa-Tanzania wenzangu tusikilize mawaidha ya Baba wa Taifa. Angalau tusome vitabu vyake, hata kama ni viwili vitatu tu. Kuna usemi wa wahenga kuwa asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Kwa kutozingatia ushauri wa Mwalimu Nyerere kuhusu umuhimu wa upinzani, CCM itaendelea kuipeleka Tanzania kubaya. Hatimaye ni kuvunjika guu.
Rais Magufuli anasema daima kwamba msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. Nadhani anamaanisha wale wanaosema yaliyomo moyoni na akilini mwao, bila unafiki. Kama nimemwelewa vizuri, basi mimi ni mmoja wa hao wasema ukweli. Sikubaliani na sera yake Rais Magufuli ya kuubana upinzani. Ninataka afuate nyayo za Mwalimu Nyerere, ambaye alitetea upinzani, mikutano na maandamano ya amani, hata kusukuma magari.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...