Saturday, January 6, 2018

Utendi wa Vita vya Igor

Wiki hii nimesoma The Lay of the Warfare Waged by Igor. Huu ni utendi maarufu wa vita vya shujaa Igor wa Urusi. Nilinunua nakala ya utendi huu, ambayo picha yake nimeweka hapa, Dar es Salaam. Sikumbuki nilinunua mwaka gani.

Ninakumbuka pia kuwa niliwahi kusoma utendi huu, lakini nimeusoma tena. Unaongela matukio ya mwaka 1185 nchini Urusi. Igor, wa ukoo wa kifalme, alikwenda kuwashambulia watu wa kabila la Polovtsi akiwa na wapiganaji aliowachagua kwenda nao vitani.

Walipata ushindi mwanzoni, lakini baadaye walielemewa na kushindwa na Igor kutekwa. Wapolovtsi walisonga mbele na kuleta maafa katika Urusi. Hatimaye, kwa msaada wa m-Polovsti mmoja, Igor anafanikiwa kutoroka na kurejea nyumbani.

Mtunzi wa utendi huu analalamikia maafa yaliyoipata nchi yake ya Urusi. Analalamikia kukosekana kwa umoja miongoni mwa watawala wa maeneo mbali mbali ya Urusi. Anamlalamikia Igor kwa kujitosa vitani bila kuwashirikisha wengine, kwa kiburi chake na kutaka umaarufu binafsi.

Jambo mojawapo la pekee katika utendi huu ni jinsi nchi na viumbe kama wanyama na ndege wanavyoonyesha hisia kama binadamu. Kwa mfano, viumbe wanatabiri maafa wakati Igor akielekea vitani:

And now the birds in the oaks
Gloat over his misfortune to come.
The wolves howl in the gullies
Raising a storm,
The eagles call the beasts
To glut upon bones,
The foxes bark
At the scarlet shields.

Utendi huu unaibua masuali kuhusu ushujaa. Igor amekurupuka na kwenda vitani ili kujipatia umaarufu. Ni shujaa, ila ana ubinafsi na kiburi kupitiliza. Anafanana na Gassire, mhusika mkuu wa utendi wa Afrika Magharibi uitwao Gassire's Lute. Wakati Igor anaelekea vitani, anapuuzia hata ishara za mikosi. Kiburi hiki wa-Griki wa kale walikiita "hubris." Ni fundisho kwa jamii.

1 comment:

Rashid Rashidy said...

Profesa nimepitia hii bashraf ya utendi... Hakika mwandishi alimwelezea vizuri sanasana shujaa Igor na kama jamii ya kitanzania pans kitu cha kujifunza juu ya mustakabali ya mwelekeo wa nchi yetu na huyu Igor wetu tulie nae...

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...