Wanataaluma wa fasihi simulizi wanaelewa kuwa haya masimulizi yaitwayo saga ni ya nchi za ulaya Kaskazini, kama Iceland na Ireland. Ni sawa na tendi za kale katika utamaduni wa wa-Swahili.
Nilivutiwa na wazo la kuhusisha fasihi simulizi ya Iceland katika kozi yangu ya Folklore, kutokana na kufundisha utungo wa Kalevala kutoka Finland. Utungo huu , ambao umetafsiriwa katika lugha nyingi, ikiwemo ki-Swahili, iulinifungua macho kuhusu fasihi simulizi ya Ulaya ya kaskazini. Mvuto wa usimuliaji wa hadithi, mila na imani zilizomo zilinigusa kwa namna ya pekee.
Kuhusu hizi saga, kwa miaka mingi nilikuwa ninafahamu uwepo wake, na nilifahamu majina ya baadhi ya hizi saga. Wakati ninasoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86, profesa Harold Scheub alitufundisha kuhusu Njal's Saga, ambayo inafahamika sana.
Baada ya kuamua kuhusisha fasihi simulizi ya Iceland katika kozi yangu, na baada ya kuamua kuwa nitumie saga, nilianza kutafakari ipi nitumie saga ipi. Mwanafunzi wangu mmoja hapa chuoni St. Olaf aliniambia kuwa mama yake alifanya utafiti na kuhitimu shahada ya uzamifu juu ya saga za Iceland. Tulikubaliana awasiliane naye, na ndiye aliyependekeza nitumie Hrafnkel's Saga.
Baada ya kupata pendekezo hilo, nilifanya utafiti kidogo, nikagundua kwamba Hrafnkel's Saga inazua malumbano miongoni mwa wanataaluma. Suali mojawapo ni iwapo kisa hiki asili yake ni fasihi simulizi au andishi. Baada ya kuona huo utata, niliona kuwa kisa hiki kitafaa katika kozi yangu kama changamoto ya kusisimua akili.
No comments:
Post a Comment