Friday, June 1, 2012

Tamko la Maaskofu Kuhusu Machafuko na Hali ya Vitisho Zanzibar

Sisi Maaskofu, Mapadre, Wachungaji na Waumini tunaoishi Zanzibar,
tumekutana leo tarehe 30 Mei 2012 kufutia hali ya machafuko, uvunjifu
wa amani, uchomaji wa Makanisa, uharibifu wa mali za Kanisa na vitisho
dhidi ya Wakristo na mali zao.

Tumekutana na tunatoa tamko baada ya muda mrefu wa kimya na uvumilivu
tuliosafiri nao kwa takribani miaka 11, kwa kumbukumbu zetu tangu
mwaka 2001. Tunajua na tunauambia umma wa wapenda amani kuwa matukio
ya tarehe 26 hadi 28 Mei 2012 ni matokeo ya mahubiri na mihadhara
ambayo imekuwa ikiendeshwa iliyolenga kwa makusudi kuutukana na
kuukashifu Ukristo hapa visiwani Zanzibar na hivi kupandikiza hofu
miongoni mwa waumini wa dini ya Kikristo. Tunashawishika kusema kuwa
ufadhili na ushawishi wa vurugu na vitisho hivi vina udhamini wa ndani
au nje ya nchi yetu.

Tumefikia hatua hiyo baada ya matukio mbalimbali yaliyokuwa yanafanywa
dhidi ya Kanisa na mali zake tangu mwaka 2001 hadi hivi majuzi
yalikuwa yakitolewa taarifa kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa
visiwani Zanzibar lakini ushirikiano umekuwa mdogo na kwa sehemu kubwa
dhaifu sana. Kwa maelezo na vielelezo ni kwamba, jumla ya makanisa
yasiyopungua 25 yamevunjwa na kuchomwa moto tangu mwaka 2001, pamoja
na ahadi za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo
yote yaliyopata kutolewa taarifa hakuna hata moja lililothibitika
wahusika kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za
kisheria.

Kumekuwa pia na vitendo vya kuchoma magari huko Pemba na hapa Unguja,
na Serikali kwa upande wake imeshiriki hata kupora ardhi na majengo ya
Kanisa hapa Unguja na huko Pemba.

Tumebaini pia hasa baada ya matukio ya vurugu za tarehe 26 hadi 28 Mei
2012 kuwa kuna mikakati ya makusudi ya kuwafanyia Wakristo vurugu.

Mikakati hiyo inajumuisha mambo kama vile kuchoma Makanisa zaidi,
kuharibu mali za Makanisa yakiwemo mashule, vituo mbalimbali vya
Kanisa vinavyotoa huduma za kijamii hapa Visiwani.

Mkakati au mpango huo umepangwa na unakusudiwa kutekelezwa kati ya
tarehe 1 na 2 Juni, na tarehe 8 na 9 Juni mwaka huu. Tunazo taarifa
tunazoweza kuzithibitisha kuwa baadhi ya Wakristo wamekuwa wakitumiwa
jumbe za simu za mkononi (SMS) zikiwatisha na kuwataka waondoke
visiwani humu mara moja hata kama ni wazawa.

Sehemu ya pili ya mkakati ni kuwasaka Wakristo nyumba kwa nyumba kwa
ajili ya kuwaangamiza, kuwabaka na kuwalawiti.

Chakusikitisha zaidi ni pale ambapo baadhi ya walinzi wa Usalama wa
raia hasa Polisi wenye asili ya hapa Visiwani Zanzibar kusikika
wakisema kuwa wataunga mkono vurugu kila zitakapotokea.

Kufuatia maelezo hayo yote, Sisi Maaskofu, Wachungaji, Mapadre na
waumini tuliokutana leo, tunapenda kwanza kutoa neno la shukrani kwa
uongozi wa Serikali kwa ushirikiano iliyotuonyesha kufutia matukio ya
hivi majuzi, na hasa kwa kupewa fursa za kukutana na viongozi na
kusikilizwa.

Tunatamka kuuelezea umma wa wapenda Amani wote tukisema, tumechoswa
kuishi na kuchukuliwa kama raia wa daraja la pili katika nchi yetu.

Tunaonya kuwa hatuko tayari tena kuvumilia vitendo vya uvunjaji wa
amani na haki zetu na tabia za kufanywa tuishi kwa hofu.

Kadhalika tunaiomba seriakli yetu ituhakikishie usalama wa maisha
yetu, mali zetu pamoja na majengo yetu ya ibada.

Wito wetu kwa viongozi wa dini mbalimbali hapa nchini ni kuwa, kila
mmoja anawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba nchi yetu inatawaliwa kwa
mujibu wa sheria za nchi na kwmba kila mmoja ahubiri kwa lengo la
kukuza amani, utulivu na usalama wa kila mtu na mali zake.

Mwisho, tunapenda kuhitimisha tamko letu kwa kuwaalika wakristo wote
kuiombea nchi yetu amani, utulivu na mshikamano ambazo ni tunu
tulizoachiwa na waasisi wetu.

Ni imani yetu pia kwamba viongozi wetu wataendeleza wajibu wao na
mamlaka waliyopewa na Mungu pasipo upendeleo wa aina yoyote.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Zanzibar.

Kwa niaba ya Wakristo wote;

Ni sisi Maaskofu wenu

1. Michael Hafidh
Askofu wa Kanisa Anglikana Zanzibar

2. Augustine Shao
Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar

3. Pastor Timothy W. Philemon
Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Makanisa ya Pentekoste
Zanzibar

SOURCE: Kiongozi [Toleo Na: 22 Juni 01-07,2012 (uk 2)].

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...