Thursday, December 30, 2010

Utamaduni na Utandawazi: Tunawafahamu wa-Turuki?


Wasomaji wa blogu zangu wanafahamu kuwa suala la utamaduni na utandawazi ni moja ya masuala ninayoyatafakari sana. Ninaelezea umuhimu wa suala hili kwa namna ya pekee katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Dhana ya utamaduni ina maana nyingi, na ni muhimu kwa mtumiaji wa dhana hii kuelezea anaitumia kwa maana ipi. Ili nieleweke vizuri na kiurahisi, singependa kuleta nadharia na mambo ya kufikirika. Badala yake, nimeamua kuuliza suali: Tunawafahamu wa-Turuki?

Leo hii, Tanzania na u-Turuki zinajenga uhusiano kwa kiwango ambacho hatujawahi kuona kabla, katika nyanja kama biashara, utalii, na elimu. Shirika la ndege la u-Turuki linapiga hatua katika kuimarisha safari baina ya Tanzania na u-Turuki. Ni wazi kuwa watu wa nchi hizi mbili wataendelea kuwa na mahusiano ya karibu katika nyanja mbali mbali.

Kama ninavyosema mara kwa mara, naamini kuwa mahusiano yoyote baina ya watu wa tamaduni mbali mbali yanaathiriwa moja kwa moja na tofauti za tamaduni hizo. Ndio maana ninauliza iwapo tunawafahamu wa-Turuki.

Sambamba na kuanzisha uhusiano na watu wa utamaduni tofauti na wetu, kuna umuhimu wa kujielimisha. Jambo moja ni kusoma vitabu. Nikiendelea na mfano huu wa u-Turuki, kuna waandishi maarufu wa ki-Turuki, kama vile Nazim Hikmet na Orhan Pamuk, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 2006. Kuna masimulizi ya kale, kama yale ambayo mhusika wake ni Nasreddin Hodja, maarufu kwa wa-Turuki na wasomaji wengine duniani.

Kwa miaka kadhaa nilifahamu kuhusu utungo maarufu unaojulikana kama The Book of Dede Korkut. Nilinunua nakala, lakini sikupata fursa ya kuisoma. Wiki hii nimeanza kuisoma, nikiwa nimesukumwa na hili suala la kukua kwa uhusiano baina ya Tanzania na u-Turuki. Lakini vile vile ni kwa sababu nimeamua kufundisha kitabu hiki katika kozi ya fasihi nitakayofundisha kuanzia wiki ijayo.

Kama nilivyotegemea, kitabu hiki ni hazina kubwa na njia nzuri ya kuwafahamu wa-Turuki: mtazamo wao wa maisha na mahusiano ya jamii, maadili yao na kadhalika. Kitabu hiki ni maarufu duniani. Wenzetu wa Brazil kwa mfano, ambao tunawaona kama rafiki zetu, wanakienzi kitabu hiki. Soma hapa.

Katika makala hii, juu ya kupokelewa kwa tafsiri ya The Book of Dede Korkut Brazil, tunaona wenzetu wanavyoelewa umuhimu wa kujisomea vitabu ili kujenga maelewano na watu wa nchi zingine na kuboresha mahusiano. Ni elimu ambayo inatufaa sote, kuanzia wafanya biashara, wadau wa elimu, diplomasia, utalii na kadhalika. Hayo ni baadhi ya mambo muhimu ninayomaanisha ninapoongelea suala la utamaduni na utandawazi.

Ingawa nimewataja wa-Turuki, siwaongelei wao tu. Tujiulize kama tunawafahamu wa-Hindi, wa-Australia, wa-China, wa-Marekani, wa-Rusi, na kadhalika. Jambo la kuzingatia ni kuwa dunia ya utandawazi wa leo inakuja na mitego na mitihani mingi, si ya kuivamia kichwa kichwa, bila elimu.

3 comments:

Emmanuel said...

Aksante Prof kwa kuisemea hili. Wenzetu wanajua wanachokitaka ila tatizo sisi kama wanasemavyo watanzania hatuna utamaduni wa kujisomea, tunaibuka na kila jambo linalojitokeza na hatima yakitutokea puani tunaanza kujilaumu. Tanzania kama nchi lazima ijue inataka marafiki wa namna gani na katika kila mahusiano ya kisiasa na ya kijamii ijue ijue na yenyewe inafaidika vipi. Kwenda kichwa kichwa ndo kulikotuacha kwenye mataa baada ya jumuiya ya kutofungamana na upande wowote kufa kufuatia kuporomoka kwa urusi.

Mbele said...

Ndugu Emmanuel, shukrani kwa ujumbe wako. Kutoelewana kunaweza kutokea kiurahisi sana. Mwaka huu unaoikwisha, kwa mfano, nilifuatilia sakata lililotokea baina ya vigogo wa Tanzania na kampuni ya Marekani iliyokuja kuwekeza katika mradi wa majumba au labda niseme maskani ya kupangisha.

Nilivyofuatilia mchakato mzima wa sakata hilo, niligundua vipengele ambavyo vilitokana na tofauti za mitazamo, ambayo zao la utamaduni wa mhusika. M-Marekni akisema kitu kwa namna fulani anaweza asijue kuwa m-Tanzania anaelewa vingine, na m-Mtanzania akisema kitu kwa namna fulani, m-Marekani naye anaweza akaelewa vingine.

Mambo hayo ya tofauti katika mitindo ya mawasiliano zinaweza kuchangia kukua kwa tatizo ambalo halingekuwa kubwa.

Suali linabaki: tutaelewaje yote hayo kama hatujielimishi? Tutaelewaje kama hatusomi vitabu? Hao vigogo waliohusika na huu mradi nilioutaja hapo juu wanajua nini kuhusu wa-Marekani? Au wanadhani kinachokubalika kwa m-Swahili na kwa m-Marekani ni hiki hiki?

Nawasifu wa-Marekani kwa sababu angalau wengi wao wanaonyesha mwamko wa kutaka kujua masuala hayo. Ukipitia blogu zangu, au ukizunguka mtandaoni, utaona hayo. Sisi waTanzania hata kuwazia jambo hili bado sana.

Ninasema hivyo kutokana na juhudi nilizofanya kwa miaka mitatu za kuja Tanzania kuendesha warsha juu ya utamaduni na utandawazi, warsha ambazo zinahusu yale yale ninayowaeleza hao wa-Marekani unavyoona kwenye blogu zangu.

Mbele said...

Nimeandika makala nyingine kuhusu kitabu hiki katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Hii hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...