Monday, April 19, 2010

Fisadi Anapoingia Baa

Binafsi, siwaamini wa-Tanzania wanapojifanya kuwalalamikia mafisadi. Hapo nawaongelea wa-Tanzania kwa ujumla, ingawa bila shaka wako baadhi ambao kweli wanachukia ufisadi. Lakini jamii kwa ujumla, siamini kama inachukia.

Wa-Tanzania wanapenda sana starehe, au kwa maneno ya siku hizi, makamuzi na minuso. Shughuli muhimu katika maisha ya wa-Tanzania ni sherehe. Pamoja na kwamba yote hayo yanagharimu sana, michango ya sherehe haiishi.

Katika hali hii yeyote anayechangia sana sherehe hizi anaheshimiwa na kushangiliwa. Fisadi anayo nafasi kubwa ya kujijengea heshima katika jamii yetu, kama ni mchangiaji bora wa sherehe hizi.

Fisadi akiwa baa na kuwanunulia watu bia sana, anajijengea heshima kubwa. Wote wanamtetemekea na kumwita "mzee," na heshima yake inabaki juu.

Wa-Tanzania hawaulizi huyu mtu anapata wapi hela. Na hata wakijua, maadam anawanunulia bia na kuchangia sherehe kwa kiwango cha juu, wanafurahi na kumwenzi. Pamoja na kelele zote za kulalamikia ufisadi, sijawahi kuwasikia wa-Tanzania wakizisusia bia za fisadi. Kelele hizi kwa kiasi kikubwa ni usanii mtupu.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kiongozi umesema jambo la msingi sana. Mara nyingi huwa nawaambia rafiki zangu, waTz wanapenda ufisadi. Mtu anayelalamikiwa kwa ufisadi, akitoa mamilioni kufadhili klabu ya mpira, anapewa shangwe vibaya mno kiasi cha kufunika tuhuma zake.
Halafu nao wajanja kweli. Wanajua mahali pa kupatia ahueni ya umaarufu wao.

Christian Bwaya said...

Mafisadi wanatoka kwenye jamii na hivyo tusitegemee watakuwa tofauti na jamii yao.

Tukitaka kuijua jamii yetu vyema na kwa uzuri, tuwatazame hao tunaowaita mafisadi, ambao kimsingi ni wenzetu ila wametuzidi malimbikizo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...