Saturday, August 28, 2010

Maonesho Faribault, Minnesota

Nimerejea muda mfupi uliopita kutoka Faribault, kwenye maonesho ya utamaduni ambayo hufanyika mara moja kila mwaka, chini ya kamati ya Faribault Diversity Coalition. Mimi ni mwanakamati.

Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu.

Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania.
Baada ya meza yangu kukamilika, niliketi nikingojea wateja na watu wa kuongea nao kuhusu shughuli zangu za uandishi na ushauri juu ya masuala ya elimu na tamaduni. Picha hii, na jinsi nilivyokaa imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu uuzaji wa vitabu. Kijuu juu naonekana nimekaa kama muuza dagaaa. Ukweli ni kuwa hapa huwa ni darasa zito siku nzima.

Walikuwepo wacheza ngoma za kabila la Aztec. Hao wamekuwa wakishiriki maonesho haya mwaka hadi mwaka, na huwa ni kivutio kikubwa.




Watu walileta vitu mbali mbali vya kuuza, kama vile vyakula, vinywaji, na kazi za sanaa. Katika maonesho haya, huwa napata fursa ya kukutana na watu wengi wapya.


Leo, kwa mfano, nimekutana na huyu mama, ambaye aliniambia kuwa alisoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hii ilikuwa ni ajabu, kwani nami nilisoma katika Chuo hicho hicho, miaka ya kabla yake. Halafu, aliniambia kuwa alishachukua kozi moja ya Profesa Harold Scheub iliyohusu fasihi hadithi za Afrika. Profesa huyu ndiye aliyesimamia tasnifu yangu ya shahada ya udaktari. Kweli milima haikutani, binadamu hukutana.
Huyu kijana hapa kushoto, baada ya kununua kitabu hiki alichoshika, aliomba tupige picha. Akanipa kitabu changu kingine nishike, na rafiki aliyekuja naye akatupiga picha.

Tabia hii si ngeni kwa wa-Marekani. Huwa wanapenda kumbukumbu za aina hii. Wengi wanapenda mwandishi atie sahihi kwenye kitabu wanachonunua. Nami leo nimefanya hivyo kwa wateja wangu.
Katika mji wa Faribault kuna wa-Somali wengi, ambao wamefika miaka ya karibuni. Leo hapo kwenye maonesho nilikutana na hao wa-Somali wawili. Huyu aliyeko kushoto anaishi kwenye mji mwingine. Lakini huyu wa kulia ni rafiki yangu, ambaye anafuatilia maandishi na shughuli zangu kuhusu masuala ya tamaduni. Ni kijana makini, na tunapangia kushirikiana katika shughuli hizo.

5 comments:

emuthree said...

Hongera sana , wewe unafanya kazi kubwa sana, natumai jamii ingekuunga mkono wa kila hali

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe wako. Hizi shughuli nazipenda sana. Ninafurahi kuwa katika shughuli hizi, kama vile mpenzi wa Yanga au Simba anavyofurahi kujumuika na mashabiki wenzake kwenye vikao vya klabu au kwenye mechi.

Na sawa na hao mashabiki wa kabumbu, ambao wanagharamia shughuli za klabu na wanalipa viingilio kwenye mechi, nami pia nafurahi kugharamia shughuli zangu hizi, kwa roho moja.

Niko tayari kulipia gharama ili kushiriki shughuli kama hizo. Kwa mfano, wiki chache zilizopita nililipa shilingi 300,000 kushiriki tamasha lililoandaliwa na Tripod Media hapa Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Bofya hapa.

Nilijua fika kuwa wa-Tanzania hawana utamaduni wa kununua au kusoma vitabu, lakini nilishiriki. Ninafanya hivyo kwa vile ni fursa ya mimi kumwaga sera, na kuongea na watu, ambalo ndilo jambo linalonifurahisha sana, kwani katika kuongea na hao watu najiongezea upeo wa mawazo na fikra.

Niliuza kitabu kimoja tu hapo Diamond Jubilee Hall. Wengine wangesema kuwa nilipata hasara kwa kulipia zile shilingi 300,000. Kwa akili yangu mimi, sikupata hasara yoyote, na niko tayari kufanya tena hivyo siku zijazo. Naaamini kuwa elimu na uzoefu ninaopata katika shughuli hizi ni faida tupu.

Tuko pamoja, nami nakutakia kila la heri katika shughuli zako.

Yasinta Ngonyani said...

Kwa kweli ni kweli kabisa unafanya kazi nzuri na kubwa sana. Ubarikiwe sana.

Mbele said...

Dada Yasinta, kitu kinachonisikitisha ni kimoja, ambacho nimeeleza tena na tena katika blogu na kwingineko, nacho ni kuwa huku ughaibuni (kama vile Marekani) wenzetu wako makini na shughuli za aina hii, wakati Bongo hakuna mwamko.

Mimi kwa vile nashughulika pande zote mbili, naona hii tofauti ilivyo kubwa. Inatisha kutambua kuwa kwa mwendo huu, hatutawaweza hao wenzetu.

Laiti tungefuata ule ushauri wa Mwalimu Nyerere kuwa wakati wenzetu wanatembea, sisi twende kwa mbio. Lakini sasa, sielewi pa kuanzia katika kuwahamasisha wa-Tanzania wenzetu.

Kuna wakati nawazia labda bora kushughulika na watoto, ambao bado hawajaharibiwa akili, na ndio taifa la kesho. Ninaandaa makala kuhusu suala hili, na itatokea katika hii blogu yangu.

emuthree said...

Wakati mwingine nawaza kuwa kuna watu walizaliwa kipindi ambacho sio, yaani sisi bado tupo nyuma sana, halafu wanazaliwa watu wa hatua mbele. Watu kama hawa hupata taabu sana, kwasababu wanajua nini kinatakiwa lakini waliopo hawajui na vigumu kuwaelimisha.
Wewe ni miongoni mwa vichwa vya tanzania, Mungu atakusaidia na ipo siku Watanzania watazinduka na kugundua umuhimu wa vitabu!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...