Ujumbe wa Msomaji wa Kitabu

Naichukulia blogu hii kama mahali ambapo naweka mambo yangu binafsi: kumbukumbu, fikra, dukuduku, hisia na kadhalika. Ingawa najua watu wanasoma ninayoandika, siwezi kusema kuwa wao ndio walengwa. Ninajiandikia mwenyewe, kwa uhuru na namna ninayotaka, mambo yangu binafsi.

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mshiriki mmojawapo wa warsha niliyoendesha Dar es Salaam mwaka jana. Bofya hapa. Ameniulizia naenda lini kutoa warsha zingine akahudhurie.

Pia amesema kuwa kitabu cha Africans and Americans ambacho alikinunua wakati wa warsha kinamsaidia katika kutoa mihadhara na kushughulikia masuala mengine ya mahusiano sehemu za kazi.

Ni wazi nimefurahi kusikia hayo. Nani asingefurahi? Nimemwambia nafarijika kuwa kitabu kimezaa matunda mema kwake, hasa nikikumbuka gharama ya warsha na kitabu. Lengo moja la kuandika kitabu hiki lilikuwa kuwasaidia wanaohitajika kutoa mihadhara kuhusu tofauti za tamaduni na matatizo na changamoto zitokanazo na tofauti hizi. Wengine wanakuwa na majukumu ya kusuluhisha migogoro. Mimi mwenyewe nakitumia kitabu hiki, mahali pa kuanzia.

Maoni ya wasomaji ni msaada mkubwa kwa mwandishi. Nami nina bahati ya kuyapata mara kwa mara. Wengine, kama ilivyo katika ulimwengu wa vitabu, wanayaweka maoni yao hadharani, kama haya hapa. Nawajibika kutoa shukrani.

Comments

lubasha said…
Mimi huwa nafatilia shughuli zako kwa kiasi fulani. Ningependa kujuwa wapi unaweza kupata vitabu vyako hapa Dar
Mbele said…
Shukrani sana kwa ujumbe wako. Ninajitahidi vitabu vipatikane hapa Tanzania. Kwa sasa unaweza kuvipata sehemu hizi:

Arusha (Kimahama Literature Center)
0786242222

Dar es Salaam (Sinza)
0754 888 647
0717 413 073

Bagamoyo
0754445956

Karatu (Bougainvillea Lodge)
0754576783

Longido (Cultural Tourism Program)
0787855185

Mto wa Mbu (Cultural Tourism Program)
0786373099

Kila la heri.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini