Showing posts with label maoni. Show all posts
Showing posts with label maoni. Show all posts

Thursday, October 12, 2017

Profesa Amekifurahia Kitabu

Ni kawaida yangu, kuchapisha maoni ya wasomaji wa vitabu vyangu. Leo nimepata ujumbe kutoka kwa profesa moja ambaye alihudhuria mkutano wa Africa Network nilioshiriki kuuandaa hapa chuoni St. Olaf.

Profesa huyu Mmarekani anawapeleka wanafunzi wa ki-Marekani Kenya na Rwanda. Katika mkutano wetu, aliongelea programu hiyo, akielezea jinsi tofauti za tamaduni zinavyojitokeza.

Nilivutiwa na mhadhara wake, kwa kuwa nami ni mzoefu wa programu hizi za kupeleka wanafunzi Afrika, ikiwemo Tanzania. Nilimpelekea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, naye ameniandika ujumbe huu:

Dear Joseph,
There were several wonderful things that came from my attending the Africa Network conference. Meeting you and learning more is one. I just finished your book and enjoyed it so much. It made me laugh out loud and understand my Kenyan teaching colleague even more. I have been both to Rwanda and Kenya many times and am aware of many of the situations and misunderstandings you describe. I’ve shared my thoughts with Kitito and we hope to use your book in some way for our spring Cultural Identity course. 
Thanks again.

Ninashukuru kwamba kitabu hiki kinatoa mchango ambao nilipangia nilipokiandika, ikiwemo kuwaelimisha wanaohusika na programu za kupeleka wanafunzi Afrika. Msukumo wa kukiandika ulitoka katika mikutano ya jumuia ya vyuo iitwayo Associated Colleges of the Midwest (ACM), na baada ya kukichapisha, wahusika wa programu zingine nao wanakitumia. Mifano ni programu ya  chuo kikuu cha Wisconsin-Oshkosh na pia program ya chuo cha Gustavus Adolphus, ambayo nimeitaja mara kwa mara katika blogu hii.


Tuesday, July 18, 2017

Mhadhiri wa Algeria Amekifurahia Kitabu

Mimi kama mwandishi, ninaguswa na maoni ya wasomaji. Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mhadhiri wa chuo kikuu kimoja cha Algeria, Samir, ambaye tumewasiliana kwa miaka michache, na nilimpelekea nakala ya kijitabu changu, Notes on Achebe's Things Fall Apart.

Nanukuu sehemu ya ujumbe wake:

I hope this finds you safe. I am so pleased to let you know that your book on Achebe's TFA is very helpful!! It really helped me. It is a pleasure also to inform you that I am citing you in my phd thesis on Gender in Ngugi's fiction. Your name will also be cited in my Acknowledgements and Dedications. Thank you so much....We love you much.

Kwa wale wasiojua ki-Ingereza, napenda kuelezea anachosema mhadhiri huyu kwa ujumla. Anasema kuwa anategemea ujumbe wake utanifikia nikiwa salama. Amefurahi sana kunifahamisha kuwa kitabu changu kuhusu riwaya ya Achebe ya Things Fall Apart ni mchango mkubwa sana na kimemsaidia sana. Anafurahi kunifahamisha vile vile kuwa ananukuu kitabu changu katika tasnifu yake ya uzamifu kuhusu jinsia katika riwaya za Ngugi wa Thiong'o. Jina langu litatajwa katika orodha ya watu waliochangia tasnifu hii. Anahitimisha kwa kusema, "Asante sana....Tunakupenda sana."

Ujumbe wowote kutoka kwa wasomaji makini una manufaa kwangu kama mwandishi. Ninayachukulia maanani maoni yao, hasa nikijua kuwa wametumia hela zao kununua kitabu changu. Kuna wengine ambao ninakuwa nimewapa nakala ya bure. Hao wanaponiandikia maoni yao juu ya kitabu ninaona kama wamelipa fadhila. Maoni yao ni muhimu kwangu kuliko hela.

Kitabu hiki na vingine vinapatikana hapa

Saturday, May 13, 2017

Msikilize Raia wa Marekani Anavyomrarua Kiongozi

Jambo moja linalonivutia kuhusu Marekani ni uhuru wa kujieleza. Katiba ya Marekani inalinda uhuru huo kikamilifu. Kwa mfano, kulikuwa na kesi dhidi ya mtu aliyechoma moto bendera ya Taifa, lakini mahakama kuu iliamua na imeendelea kusisitiza kuwa kuchoma moto bendera ya Taifa ni sehemu ya uhuru wa kujieleza, ambao unalindwa na katiba. Mahakama kuu inasisitiza kuwa kauli tata, za kukera, au za kuwakosoa watawala ndizo hasa katiba ilikusudiwa kuzilinda.

Serikali ya Marekani inafahamu kuwa raia ana uhuru na haki kamili ya kuikosoa. Viongozi wa Marekani wanajua hilo. Ninaleta video hapa, inayomwonyesha mwananchi akimfokea kiongozi bila kumung'unya maneno. Mwone kiongozi huyu kutoka chama tawala cha Rais Donald Trump alivyonywea, wakati kipigo kinaendelea.

Thursday, August 26, 2010

Ujumbe wa Msomaji wa Kitabu

Naichukulia blogu hii kama mahali ambapo naweka mambo yangu binafsi: kumbukumbu, fikra, dukuduku, hisia na kadhalika. Ingawa najua watu wanasoma ninayoandika, siwezi kusema kuwa wao ndio walengwa. Ninajiandikia mwenyewe, kwa uhuru na namna ninayotaka, mambo yangu binafsi.

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mshiriki mmojawapo wa warsha niliyoendesha Dar es Salaam mwaka jana. Bofya hapa. Ameniulizia naenda lini kutoa warsha zingine akahudhurie.

Pia amesema kuwa kitabu cha Africans and Americans ambacho alikinunua wakati wa warsha kinamsaidia katika kutoa mihadhara na kushughulikia masuala mengine ya mahusiano sehemu za kazi.

Ni wazi nimefurahi kusikia hayo. Nani asingefurahi? Nimemwambia nafarijika kuwa kitabu kimezaa matunda mema kwake, hasa nikikumbuka gharama ya warsha na kitabu. Lengo moja la kuandika kitabu hiki lilikuwa kuwasaidia wanaohitajika kutoa mihadhara kuhusu tofauti za tamaduni na matatizo na changamoto zitokanazo na tofauti hizi. Wengine wanakuwa na majukumu ya kusuluhisha migogoro. Mimi mwenyewe nakitumia kitabu hiki, mahali pa kuanzia.

Maoni ya wasomaji ni msaada mkubwa kwa mwandishi. Nami nina bahati ya kuyapata mara kwa mara. Wengine, kama ilivyo katika ulimwengu wa vitabu, wanayaweka maoni yao hadharani, kama haya hapa. Nawajibika kutoa shukrani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...