Leo Nimemwandikia Mzee Patrick Hemingway

Leo nimemwandikia barua pepe Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Nilipiga naye picha inayoonekana hapa kushoto tarehe 27 Aprili, 2013, nyumbani pake mjini Craig, katika jimbo la Montana.

Nilifahamu habari zake kwa miaka mingi kabla ya kufahamiana naye na halafu tukakutana. Ni mzee mwenye maongezi ya kusisimua kuhusu baba yake Ernest Hemingway na waandishi wengine wa wakati wake. Pia ana kumbukumbu nyingi za Tanganyika, na kisha Tanzania, ambako aliishi kwa miaka yapata 25 kabla ya uhuru na baada ya uhuru, akiendesha kampuni ya utalii, na hatimaye akiwa mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mwika.

Tangu tulipoanza kufahamiana, ameguswa na ari yangu ya kutafiti maandishi, falsafa, na maisha ya Ernest Hemingway, na amevutiwa na msimamo wangu kuwa Ernest Hemingway ni mwandishi aliyetuenzi sana sisi watu wa Afrika Mashariki, na tunapaswa kujielimisha kuhusu mchango wake, na kisha kuutumia katika kujitangaza kama alivyotutangaza.

Hayo yamemfanya Mzee Patrick Hemingway awe tayari kunisaidia kwa dhati katika juhudi zangu za kujielimisha na kuuelimisha ulimwengu juu ya Ernest Hemingway. Miezi kadhaa iliyopita, nilivyomweleza kuwa napangia kutembelea hifadhi ya Ernest Hemingway katika John F. Kennedy Library, aliniambia kuwa nitakapokuwa tayari nimfahamishe ili anitambulishe kwa wahusika.

Nilipoongea naye tarehe 19 mwezi huu na kumtajia tarehe nilizopangia kwenda kwa shughuli hiyo, aliniagiza nimpelekee maelezo yangu kwa barua pepe, ili aweze kuandaa utambulisho huo. Aliniambia kuwa ninakwenda wakati mzuri, kwani kuna maonesho maalum juu ya Hemingway, ambayo yameanza siku chache zilizopita na yatadumu kwa miezi kadhaa.

Basi, leo nimemwandikia. Kilichobaki sasa ni kuandaa safari, nikajionee hiyo hifadhi kubwa kuliko zote duniani juu ya Ernest Hemingway. Hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kuitembelea hifadhi hiyo, lakini sitegemei kuwa itakuwa ni mara ya mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini