Nimenunua "Good Prose," Kitabu Kuhusu Uandishi

Siku chache zilizopita, katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, nilikiona kitabu kiitwacho Good Prose: The Art of Nonfiction. Jina hilo lilinivutia, nikapata duku duku ya kukiangalia. Nilivyoona kuwa mwandishi mojawapo, Tracy Kidder alikuwa amepata tuzo ya Pulitzer, nilivutiwa kabisa. Hii ni tuzo ya uandishi yenye hadhi kuliko zote zinazotolewa hapa Marekani.

Nilivyochungulia kurasa zake, niliona kina mawaidha mazuri kuhusu uandishi bora. Si uandishi wa kazi za fasihi, bali uandishi kama wa insha. Huu ndio uandishi wangu, na ndio uandishi ninaofundisha. Nilivutiwa pia nilipoona waandishi maarufu wamenukuliwa katika kitabu hiki, kama vile Norman Mailer,  Ernest Hemingway, Vladimir Nabokov, na William Strunk, Jr.

Kwa bahati mbaya sikuwa na hela, nikaondoka bila kukinunua, kwa shingo upande. Leo nilikwenda tena dukani, nikakuta kitabu bado kipo. Nilikinunua hapo hapo.

Pamoja na kwamba nina uzoefu wa miaka mingi wa kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza, na pamoja kwamba ninawafundisha watu ambao ki-Ingereza ni lugha mama yao, siridhiki na ufahamu wangu. Ninajifananisha na waandishi wa ki-ingereza ambao ni maarufu duniani, na hiki ndicho kigezo sahihi, kwani katika kujipima huko, ninatambua kuwa sijawafikia. Kwa hivyo, ninatambua umuhimu wa kujielimisha muda wote. Ni ujinga kuridhika na elimu uliyo nayo.

Mtu ukitaka kujipima katika fani yako, jifananishe na wale walifanikiwa kwa kiwango cha juu kabisa. Kwa mwandishi, naona ni wajibu kujipima dhidi ya waandishi waliotwaa tuzo maarufu kama Nobel, Booker, na Pulitzer. Hapo mtu utatambua kuwa bado una njia ndefu ya kusafiri.

Good Prose: The Art of Nonfiction ni kitabu nitakachokisoma kwa makini. Kimeelezwa kwenye jalada kama "Stories and advice from a lifetime of writing and editing," na kwamba ni "an inspiring book about writing--about the creation of good prose." Bila shaka kitabu hiki kitanihamasisha kutafakari zaidi suala la uandishi bora, suala ambalo nimekuwa nikilizungumzia katika blogu hii.


Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini