Leo ni Jumapili, nami nimerejea kutoka kanisani kusali. Nilipokuwa njiani, nilijikuta nikiwazia suala la dini, nikajiuliza kuhusu dhana ya dini ya kweli. Nini maana ya dini ya kweli? Kuna dini ya kweli? Kama ipo, ni ipi? Hili ni suala tata, nami napenda kuthibitisha angalau kidogo utata huo. Ninategemea kuwa wasomaji wangu watachangia mawazo.
Kwa mtazamo mmoja, tunaweza kusema kuwa kila dini ni dini ya kweli, kwa maana kwamba iko. Ni sawa na kitu chochote kinginecho kilichopo. Kila kilichopo ni kitu cha kweli, iwe ni chakula, bangi, au kifo. Vyote hivyo ni vitu vya kweli, kwa maana kwamba vipo. Na dini ni hivyo hivyo. Dini ziko. Kila dini ni dini ya kweli.
Kwa mtazamo mwingine, watu wanapoongelea dini ya kweli, wanamaanisha dini inayokubalika kwa Mungu. Wanamaanisha dini itakayomfikisha binadamu kwenye uokovu. Hapo pana utata mkubwa, kwani waumini wa dini mbali mbali wana tabia ya mwamba ngoma, ambaye huvutia ngozi upande wake. Matokeo yake katika historia ya binadamu yamekuwa mabaya. Uhasama, magomvi, mauaji, na ushetani wa kila namna.
Kwa watu hao, misahafu imekuwa silaha yao kuu. Wanalumbana kwa msingi wa misahafu. Wanatambiana kuhusu misahafu, kila mtu akiunadi msahafu wa dini yake kuwa ndio neno la Mungu.
Msimamo wangu ni tofauti. Msahafu si dini. Msahafu ukitumiwa vizuri unaweza kuwa mwongozo. Dini inatokea na inadhihirika pale mtu anapofuata huo muongozo katika maisha yake, kwa mawazo na vitendo. Uthibitisho wa dini unaonekana katika maisha ya waumini, si katika maneno au porojo.
Ni kama elimu. Mtu huwezi kusema una elimu kwa kuwa tu una vitabu. Kinachotakiwa ni kuvisoma vitabu ukiwa na akili timamu, kuvichambua, kuchota yale yanayofaa, na kisha kujijengea fikra, ufahamu, mtazamo, mwelekeo na maisha yako kwa mujibu wa yale uliyoyapata vitabuni. Uwe mtu unayefikiri, kuongea, kuishi, kama mtu mwenye elimu.
Kuna jambo moja ambalo naliona kuwa la kipuuzi, nalo ni jadi ya waumini kudai kwamba msahafu wao ndio pekee neno la Mungu. Dhana hii inatokana na ujinga. Kila jamii duniani tangu miaka maelfu yaliyopita, ilitambua kuwepo kwa Mungu. Watafiti wa masomo kama "Folklore" tunajua hilo vizuri, kwani tunayafahamu masimulizi ya mataifa mbali mbali yaliyotokana na jadi za kabla ya kuwepo maandishi, kabla ya kuandikwa kwa misahafu.
Mambo ya msingi ya imani za dini yalikuwemo katika haya masimulizi ya jadi. Wanadamu wote walitambua kuwepo kwa Mungu na walikuwa na ufahamu mzuri wa mema na mabaya. Walijua Mungu anataka nini na anakataza nini, na walijifunza na kufundishana hayo kwa masimulizi ya mdomo. Misahafu imekuja baadaye na imechota mengi kutoka kwenye hayo masimulizi ya jadi.
Kwa msingi huo, sioni kama ni sahihi kudai kuwa kitabu cha dini fulani ndio pekee neno la Mungu. Mimi kama muumini ninayefuatilia taaluma ya "Folklore," ambayo inatuingiza katika masimulizi yaliyotokana na kila taifa au kabila hapa duniani, nakiri kuwa Mungu alijitambulisha kwa mataifa yote. Kitabu si msingi. Mataifa na makabila mengi duniani hayakuwa na vitabu na mengi hayana vitabu. Lugha zao hazijaandikwa, na wanajifunza na kufundishana kwa masimulizi ya mdomo. Kwa mtindo huo, neno la Mungu daima limekuwepo miongoni mwao.
Kuna jambo jingine napenda niliseme, kuhitimisha ujumbe wangu. Ninapowazia dhana ya dini, na hasa ninapowazia dhana ya dini ya kweli, ninaihusisha na amani, upendo, na haki kwa wanadamu wote bila ubaguzi. Kwangu mimi, hivi ndivyo vigezo na ushahidi wa kuwepo kwa dini kwa maana ya dini ya kweli. Bila vigezo hivyo, sioni dini ya kweli bali ulaghai. Niliwahi kufafanua wazo hilo katika blogu hii, na kwenye sehemu ya maoni, mwishoni mwa Makala yangu, Christian Bwaya alifafanua vizuri kwamba dini kama tunavyoziona ni chimbuko la matatizo. Ninaona kuwa anachomaanisha, ndicho hiki ninachomaanisha ninapoongelea dini ya kweli, yaani kutambua umuhimu wa kuwatendea wanadamu wote kama tunavyopenda kutendewa, bila ubaguzi, tukizingatia kuwa Mungu hana ubaguzi.
Hayo ndiyo mawazo yangu ya leo Jumapili.
Sunday, May 15, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment