Kitabu kwa Wasafiri Watokao Nebraska

Leo nimeona taarifa kutoka sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, kuhusu maandalizi ya safari za kwenda Tanzania. Safari hizo zimefanyika tangu miaka iliyopita. Kuna sehemu iitwayo "Preparatory Reading," na kama miaka iliyopita, katika sehemu hiyo kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimependekezwa kwa wasafiri hao:

For those persons wanting to more deeply explore cultural differences between Africans and Americans, the book Africans and Americans: Embracing Cultural Differences by Joseph Mbele is recommended. The book is available at www.africonxion.com.

Kwangu kama mwandishi, hii ni habari njema, ingawa si mpya. Viongozi wa programu kama hiyo ya Nebraska wana uzoefu wa miaka mingi wa kwenda Tanzania. Wana uzoefu wa utamaduni wa Tanzania. Kuendelea kwao kukipendekeza kitabu changu ni ushahidi kuwa wameona kinawafaa wa-Marekani wanaowapeleka Tanzania.

Watu kutoka Nebraska wanaosairi kwenda Tanzania nimewahi kuwataja katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Ninajisikia kama vile, kwa njia ya kitabu changu, nina uhusiano wa kudumu nao.

Nimeandika nilivyoandika, ingawa ninafahamu kuwa kwa mujibu wa utamaduni wa leo wa Tanzania, tunaogopa kuambiwa tunaringa. Ninaamini kuwa ni sahihi mtu kujivunia kazi yake na mafanikio yake, kama wafanyavyo wanamuziki wetu, ambao aghalabu tunawasikia wakitamba wanapoandaa albamu au wimbo wa kutupagawisha. Tunapowasikia wakisema hivyo, tunafurahi na kusubiri kwa hamu.

Lakini ni ajabu kuwa tunaona si sahihi kwa mwanataaluma kujivunia kazi yake. Lakini ninaona tujikumbushe kauli iliyomo katika "Azimio la Arusha" kuwa katika nchi yetu, kazi iwe ni kitu cha kujivunia; na uvivu, ulevi, na uzembe viwe ni vitu vya kuvionea aibu. "Azimio la Arusha" linazungumzia kila kazi yenye manufaa kwa mtu na jamii.

Kama kichekesho, ninakumbushia methali iliyomo katika riwaya ya Things Fall Apart ya Chinua Achebe: "The lizard that jumped from the high iroko tree to the ground said he would praise himself if no one else did," ambayo inamaanisha kuwa ukifanikisha jambo, usichelee kujisifu mwenyewe. Labda huo ndio utamaduni tunaouhitaji.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini