Showing posts with label majarida. Show all posts
Showing posts with label majarida. Show all posts

Thursday, May 11, 2017

Shukrani kwa Msomaji

Msomaji mwingine wa kitabu cha Africans and Americans; Embracing Cultural Differences amejitokeza na kuandika maoni yake kuhusu kitabu hiki. Ameandika maneno matatu tu, "Short and sweet," katika mtandao wa Goodreads, ambao ni maarufu miongoni mwa wasoma vitabu. Humo wanaweka maoni yao kuhusu vitabu walivyosoma au vitabu wanavyopangia kusoma.

Kama ilivyo kawaida yangu katika blogu hii, ninamshukuru kwa kujipatia kitabu hiki, kukisoma, na kuwajuza walimwengu maoni yake. Amefanya hivyo kwa hiari yake, akijua kwamba kauli yake itasomwa na watu wengi. Namshukuru kwa hisani yake; amenifanyia kazi bila malipo wala kutegemea shukrani.

Maoni ya wasomaji yana manufaa makubwa. Kwanza yananiwezesha kufahamu kama ninafikisha ujumbe wangu na unaeleweka vipi. Kila msomaji anapotoa maoni, hutaja jambo fulani au mambo fulani yaliyomgusa kwa namna ya pekee. Wasomaji wanaweza kuwa wamekipenda kitabu hicho hicho, lakini kwa misingi au namna mbali mbali.

Pili, kuwepo kwa maoni ya wasomaji kunaniondolea jukumu la kukiongelea kitabu changu, kwa watu wanaokiulizia. Badala ya mimi kuwaelezea, ninawaelekeza watu wakasome maoni hayo, ambayo wasomaji wameyatoa kwa hiari yao, bila msukumo wa aina nyingine.

Siku nne zilizopita, kwa mfano, m-Tanzania moja aishiye Marekani, aliniandikia ujumbe binafsi katika Facebook akinielezea kuwa anatakiwa kuongea na waalimu kutoka Marekani katika kuwaandaa kwa safari ya Tanzania. Hiyo ni programu baina yao na walimu wa Tanzania kuhusu tamaduni na ufundishaji. Alihitaji pendekezo la kitabu kuhusu tamaduni.

Nilimtajia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na baadaye nimemshauri kuwa ili ajiridhishe, aangalie maoni ya wasomaji kwenye mtandao wa Amazon na pia mtandao wa Goodreads. Kuna sehemu zingine pia ambapo maoni yamechapishwa, kama vile blogu, tovuti, na majarida.

Wednesday, March 15, 2017

Maktaba ya Chuo Kikuu cha Minnesota

Mara kwa mara, ninaandika kuhusu maktaba ninazozitembelea, hapa Marekani na Tanzania. Mifano ni maktaba ya John F. Kennedy,  ya Brookdale, ya Southdale, ya Moshi, ya Tanga, ya Iringa, ya Dar es Salaam, na ya Songea.

Jana, nilikuwa Minneapolis kwa shughuli binafsi. Baadaye niliingia katika maktaba ya Wilson. Nimezoea kwenda kusoma katika maktaba hii, ambayo ni moja ya maktaba za Chuo Kikuu cha Minnesota. Kati ya hizo, hii ndio inayonihusu zaidi, kwa sababu humo ndimo kuna majarida, vitabu, na hifadhi za lugha na fasihi.

Ingawa chuoni St. Olaf ninapofundisha pana maktaba kubwa, ambayo imeunganishwa na maktaba ya chuo cha Carleton, maktaba ya Wilson ni kubwa zaidi.

Picha zinazoonekana hapa nilipiga jana. Hiyo ya juu ni ubavuni mwa maktaba, na hiyo ya chini ni sehemu ya mbele, kwenye mlango. Ardhini inaonekana theluji, kwani ni bado kipindi cha baridi.


Saturday, November 5, 2011

Maktaba ya Mkoa, Tanga

Maktaba ya mkoa, mjini Tanga, ilifunguliwa mwaka 1958. Wa-Ingereza, ambao walikuwa wanatawala Tanganyika, ndio waliojenga maktaba hii. Ni jengo zuri sana, kama inavyoonekana hapa kushoto.








Nimetembelea maktaba hii mara kadhaa. Ni mazoea yangu kutembelea maktaba, kama nilivyoeleza hapa na hapa. Tangu nilipofika hapo maktaba ya Tanga mara ya kwanza, miaka kadhaa iliyopita, nilipata fursa ya kufahamiana na mkurugenzi, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Nimepata fursa ya kuingia ndani na kuangalia vitabu na machapisho mengine, nikachangia nakala za vitabu vyangu.



Maktaba hii ilikuwa nzuri sana tangu ilipofunguliwa. Lakini leo, hali si nzuri, kama ilivyoelezwa hapa. Maktaba inahitaji ukarabati, vitabu vipya, majarida na kadhalika. Kwa nchi tajiri kama Tanzania, ambayo ina rasilimali kuliko nchi nyingi, haieleweki kwa nini isiwezekane kukarabati maktaba kama hii. Jawabu linaeleweka: ni ujinga, ufisadi na ukosefu wa uongozi kitaifa.





Uongozi wa maktaba unajitahidi sana kufanya kazi vizuri, ingawa mazingira ni magumu. Wanajitahidi kukidha mahitaji kufuatana na mabadiliko ya wakati. Kwa mfano, mara ya mwisho nilipoingia katika maktaba hii, nilionyeshwa sehemu ambayo imewekwa maalum kwa mahitaji ya wanafunzi wa chuo kikuu huria. Wanastahili pongezi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...