Wa-Tanzania Hawana Hela za Kununulia Vitabu?

Katika malumbano yetu kwenye hizi blogu, wakati mwingine tunajadili tatizo sugu na la kukera la wa-Tanzania kutokuwa na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Baadhi ya watu wanadai kuwa kipato cha m-Tanzania ni duni kiasi kwamba wazo la kununua vitabu haliwezi kuwa kichwani mwake. Anahangaika apate angalau mlo moja kwa siku.

Hii hoja ina ukweli kwa baadhi ya wa-Tanzania. Lakini kuna maelfu ya wa-Tanzania wenye uwezo wa kununua vitabu ila hawana utamaduni huo. Ushahidi kuwa wana uwezo kifedha uko kila mahali, kuanzia baa hadi kwenye michango ya sherehe ambayo haiishi, na makamuzi mengine mengi.

Nimeona picha leo kwenye blogu ya Michuzi ambayo imenikumbusha haya malumbano yetu. Inawaonyesha mashabiki katika ukumbi wa Arcade, Mikocheni, wakishangilia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha hii haihitaji maelezo zaidi, maana vyupa vya bia vinaonekana wazi vikiwa vimeota kama uyoga, na hapo pembeni kushoto vuvuzela linapigwa kwa nguvu kuboresha haya makamuzi.

Comments

SN said…
Naona umeamua kulivalia njuga hili suala! 'Nakupa tano' kwa hilo Prof. na nina uhakika huu mjadala utakuwa mrefu sana.

Nadhani wewe ulisema kuwa Watanzania hatukosi visingizio (nimemaliza kusoma mahojiano yako BC).

Tukiacha hayo, inabidi wote tuamke na tuone kuwa dunia itatuacha nyuma. Watoto na wadogo zetu hawatakuwa wanashindana (mashuleni, kutafuta kazi n.k.) na Watanzania wenzao. Shughuli itakuwa pevu kwasababu watakutana na watu kutoka kwenye mataifa mengine. Hapa sizungumzii wale ambao wanaishi ughaibuni tu; makampuni mengi kutoka Amerika, Ulaya na Asia huleta watu wao wakati mwingine.

Sasa, kuna shimo kubwa linalotenganisha watu kutoka Tanzania na mataifa mengine. Na njia pekee ya kujenga daraja ili watu waelewane au kuwa kwenye 'level' moja ni ujuzi. Unapatikana wapi? Sote tunajua...

Kwahiyo, kama wewe unadhani hautafaidika kwa kusoma vitabu, usiwadhulumu wadogo au watoto zako. Watakuja "kukuchukia" baada ya kuujua ulimwengu.

Kitu kimoja ambacho utaona kwenye mijadala yetu mingi kwenye forums mbalimbali ni kama hatujui kufanya midahalo. Kwa maneno mengine, mijadala mingi sana huishia kwa watu kutupiana vijembe -- badala ya kujaribu kutoa mitazamo tofauti na kubadilisha mawazo au ujuzi. Inasikitisha sana na kuna wakati inatia hasira! Binafsi naamini ya kuwa kama watu tungekuwa na mitazamo tofauti na ujuzi, tusingekuwa tunajisumbua kutupiana vijembe.

Sitaki kuanza kuongea kama mwanasiasa na kufanya kampeni hapa. Jaribu kutafuta vitabu vya Ben Carson "Think Big" na "Gifted Hands":

http://www.achievement.org/autodoc/page/car1bio-1

Kwa kifupi, mama yake Ben alikuwa ni fukara lakini baada ya kufanikiwa kuweka chakula mezani, aliwasukuma watoto wake kusoma vitabu kila siku. Angalia walipo sasa hivi.

______________

In fifth grade, Carson was at the bottom of his class. His classmates called him "dummy" and he developed a violent, uncontrollable temper.

When Mrs. Carson saw Benjamin's failing grades, she determined to turn her sons' lives around. She sharply limited the boys' television watching and refused to let them outside to play until they had finished their homework each day. She required them to read two library books a week and to give her written reports on their reading even though, with her own poor education, she could barely read what they had written.

Within a few weeks, Carson astonished his classmates by identifying rock samples his teacher had brought to class. He recognized them from one of the books he had read. "It was at that moment that I realized I wasn't stupid," he recalled later. Carson continued to amaze his classmates with his newfound knowledge and within a year he was at the top of his class.

______________

The dude is one of my heroes!
Mbele said…
Ndugu SN, shukrani kwa ujumbe. Nafurahi kuwa umesoma mahojiano yangu na Bongo Celebrity. Ni kweli, yale ndio mawazo yangu, na mahojiano yale yamo katika kitabu changu cha Changamoto.

Kuna jamaa pale Dar alipomaliza kusoma mahojiano yale alikuja Sinza kununua kitabu changu cha Africans and Americans, kinachoongelewa katika yale mahojiano, na ameelezea pale kwenye maoni ya wasomaji, mwezi Agosti mwaka jana. Nilipata fursa ya kumkuta.

Huyu ni m-Tanzania makini, nami namheshimu. Wala hakulalamikia bei ya kitabu. Alipotajiwa, aliingiza mkono mfukoni akatoa hela. Baadaye, kama unavyoona kwenye maoni yake, aliandika akishukuru baada ya kukisoma. Huyu anajua faida ya maarifa na elimu, wala haoni shida kutumia hela kuyasaka maarifa na elimu.

Tatizo lililopo miongoni mwa wa-Tanzania kwa ujumla ni kama unavyoelezea. Wanajichimbia kaburi. Hela za makamuzi hawakosi. Kwenye vitabu, wana visingizio elfu.

Mfano wa Dr. Carson uliotoa ni mzuri. Nimesoma baadhi ya maandishi yake. Wa-Tanzania tungekuwa makini tungekuwa tunanunua vitabu kama vya huyu Dr. Carson na kuhakikisha tumevisoma na watoto wetu nao wamevisoma. Ndio changamoto ambayo vijana wetu wanahitaji. Lakini, kwa kukosa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu, wa-Tanzania hawatayapata yale asemayo Dr. Carson. Inasikitisha kuwa ukiwa na siri ukaiweka kitabuni, wa-Tanzania hawataiona.
Fadhy Mtanga said…
Ndugu Mbele nashukuru umeleta ushahidi wa picha. Lakini bado kuna watu watabisha watasema bado Watizedi hatuna uwezo wa kumudu kununua vitabu. Jambo la kulazimisha visingizio ndilo tatizo.

Ndugu SN, nashukuru umemzungumzia Ben Carson. Mimi ni msomaji mzuri sana wa vitabu vyake. Nilikuwa nimeacha kabisa kuandika mashairi. Mwaka 2005 niliposoma Think Big, nilijifunza umuhimu wa kukiendeleza kipaji.

Watanzania tuna sababu lukuki za kwa nini hatuwezi kufanya jambo, wakati tungehitaji sababu moja tu, kwa nini tunaweza.
Kwa kweli ni jambo la kuchekesha sana hatuna hela za kununulia vitabu lakini wana hela za kupiga pombe/ugimbi ambao watakunywa na kulwa na hakuna litakaloongezeka mwilini. Afadhani hela hiyo angenunua kitabu na kusoma na kupata maarifa. Ama kweli inasikitisHA SANA KUONA HILI JINSI WA-TANZANIA TULIVYONYUMA KWA KUSOMA. Ahsante kwa mada hii nadhani nitaiazima na kuiweka pale kwangu.
Albert Kissima said…
Kuna kanuni moja muhimu sana waTanzania tulio wengi tunashindwa kuitumia na inayotupelekea kuendesha maisha shaghalabagala na kusema bora liende, siku imepita, itakuja nyingine na itapita, isipopita potelea mbali.
Laiti tungefuata kanuni hii ya "lazima na hiari" bila shaka leo hii tusingeshudia watu wawezao kunywa pombe ya maelfu ya pesa, malaki ya pesa kuhongea wanawake/wanaume,n.k wakati anashindwa kununua hata kitabu kimoja kwa ajili yake na watoto/ndugu zake. Naimani tukizingatia kanuni ya "lazima na hiari" maisha yetu kwa ujumla yatabadilika na tutakuwa na maisha bora zaidi kwa sababu si kweli kuwa wale wafanyao kazi/watafutao huwa hawapati pesa bali matumizi ndio yanakuwa mabovu kwani fedha hazitumiki kwa kadiri ya "lazima na hiari".


Kikubwa zaidi ni kuwa, waTanzania wengi bado hatuna utamaduni wa kujisomea vitabu. Watoto hawana budi kujengewa msingi huu mapema kabisa pindi tu wajuapo kusoma.
Katu said…
Kimsingi unapokosa changamoto katika matumizi ya pesa ni kitu cha kukisikitia sana ktk maisha yetu..
Profesa Mbele huko siku za zilizopita nimewahi kuleta majadiliano kuhusiana na matatizo yanayoikabili watanzania...

Mimi ninaposema watanzania naongelea wale milioni arobaini na siyo hilo matabaka wa Tanzania wa daraja kati kama wewe Profesa Mbele na wengine wa yako na pia hilo tabaka la juu linalohusisha wakuu wa serikali na matajiri wakubwa ambao wanasemekana kwa idadi ni milioni arobaini.

Namna ya kuleta nidhamu ya pesa ni lazima tuwe na serikali wajibishi kwa kila mtanzania hivyo hizo pesa za njia za mkato zitaondoka na kila raia wa Tanzania ataweza kulipa kodi na kuwa makini na matumizi ya pesa...Kimsingi wale wengi unawaona pale kwenye hiyo pesa zao wanazipata kwa sababu hawalipi kodi halisi inayotakiwa erikalini na pesa kupitia mifukoni mwa watu...

Hapa Profesa Mbele kuna tatizo la msingi nadhani juhudi zetu zielekezwe katika kupata viongozi bora wa kisiasa na siyo hawa tulikuwa nao ambao wanawashabikia wala rushwa na kuwalinda na matokea yake serikali inakuwa siyo imara na kuathiri mfumo mzima wa maisha ya Mtanzania.

Wewe Mwenyewe Profesa Mbele nahakika unakijua kipato chako cha kwa mwaka mzima....hao unawaona hapo kwenye hata ukiwauliza kipato chao cha mwaka ni kiasi gani hawata kupatia jibu lolote!!!!!....

kwa sababu pesa zao zinatokana na michezo michafu hasa rushwa na ubadhirifu maarufu siku hizi Mafisadi....

Kama unaitakiwa mema Tanzania Profesa Mbele unatakiwa kutoa elimu ya kupambana na misingi halisi hayo matatizo na siyo kuhangaika na kulaumu hayo matokeo tunayoyashuhudia na kuacha chanzo cha matatizo halisi...Ningeshriki vizuri huu mjabdala iwapo utakubali kwamba serikali iliyopo imeshindwa kupambana na rushwa na matokeo yake imeleta madhara mengi tuu...Hata wewe kwenda kusoma ughaibuni kulichangiwa na matokea ya haya utawala na mifumo mibovu.

Hakika nakuambia mkiweza kutusaidia kuelimisha wapiga kura wetu kuwa kupiga nje ya mgombea wa CCM siyo dhambi...na pia uwakilishi wabunge uliyosawa bungeni kutoka vyama vyote vya siasa utaleta tija...basi mambo mengi unayokosoa hii jamii yetu ya kitanzania yatapungua ama kutoweka kabisa katika jamii yetu....

Nilishindwa kuchangia mapema nilikuwa shambani nikushughulikia mazao yangu hivyo ni mapumziko ya siku moja...nitarudi tena shamba kuendeleza kilimo changu cha mpunga..

Nguvu ya Teknolojia ya mawasiliano inaniwezesha kuwakilisha maoni na mwazo yangu kutoka hapa kijijini kwangu Lungongole-Kikwawila-Ifakara

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini