Mteja Wangu wa Kwanza

Tarehe 8 Mei, 2010, mteja alinunua kitabu changu cha Changamoto, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Niliguswa na kitu hicho, nikasema itabidi nikiongelee hapa kwenye blogu.

Nimechapisha vitabu kadhaa, na wateja ninao. Siri moja ya uchapishaji vitabu mtandaoni kama ninavyofanya ni kuwa ninaweza kufuatilia mauzo ya vitabu saa yoyote. Ndio maana niliweza kuona kuwa mteja wa kwanza wa Changamoto amepatikana.

Kitabu hiki ni cha pekee kwangu kwa sababu ni kitabu changu cha kwanza cha ki-Swahili. Mimi si mwandishi bora wa ki-Swahili, lakini naona nina haki ya kujipongeza kwa juhudi niliyofanya, hasa nikizingatia kuwa sisi wasomi ni wavivu katika kutumia ki-Swahili, na wengi tunaamini kuwa ki-Swahili hakina utajiri kama ki-Ingereza. Kwa vile nilisomea taaluma ya lugha na isimu ya lugha, ninaelewa kuwa dhana kama hii ni potofu. Hakuna lugha maskini.

Kama mimi, ambaye ni mwalimu wa ki-Ingereza, nimeweza kujibidisha hadi kuandika kitabu kwa ki-Swahili, sioni kwa nini wasomi wengine wasiweze kufanya hivyo hivyo.

Ninapomwazia huyu mteja wangu wa kwanza nijiuliza masuali. Sijui ni nini kilichomfanya akanunua kitabu cha ki-Swahili kilichoandikwa na mtu kama mimi. Au labda kasoma makala zangu katika gazeti la Kwanza Jamii? Au labda ni mteja wa maandishi yangu ya ki-Ingereza? Au labda ana dukuduku ya kujua nimeandika nini na ninaandika vipi? Kwa vyovyote, napenda kumshukuru na kumfahamisha kuwa ameweka historia kwa kuwa mteja wangu wa kwanza.

Comments

Fadhy Mtanga said…
Kwanza napenda kukupongeza sana kwa kuandika kitabu katika lugha ya Kiswahili. Ni changamoto kwa hakika.

Pili nakupongeza kwamba hatimaye chapisho lako limepata mteja wa kwanza.

Ni utamaduni mpya juu ya uchapaji na nimeupenda sana kama nilivyopata kusema.

Nakutakia kila la kheri. Lakini hii naipokea kama changamoto ili nasi wanablog tuweze kuchapa vitabu mtandaoni. Changamoto hii haishii hapo tu, bali tujenge utamaduni wa kununua vitabu mtandaoni.

Uwe na wakati mzuri.
Mbele said…
Ndugu Mtanga, shukrani kwa ujumbe. Ni kweli, tekinolojia hizi ni ukombozi kwa waandishi. Hawana sababu tena ya kukaa na kuwalalamikia wachapishaji wa vitabu, kwani njia iko wazi kujichapishia mwenyewe mtandaoni.

Labda tatizo linalobaki ni uwezo wa kuagiza vitabu mtandaoni. Inabidi mtu awe na kadi kama vile "credit card" ya kununulia vitu mtandaoni.

Hadi sasa si wa-Tanzania wengi wenye kadi hizi. Lakini dunia inabadilika, na kadi hizi zitaenea.

Tatizo kubwa zaidi ni kuwa wa-Tanzania hawako makini na masuala ya vitabu, kama tunavyosema siku zote humu kwenye blogu zetu. Ingekuwa wa-Tanzania wako makini, wale walioko ughaibuni wangeweza kuwa wanatumia kadi zao na kununua vitabu na kuwapelekea ndugu na jamaa Tanzania, au kuvipeleka kwenye shule huko vijijini ambako wanaenda kusalimia ndugu na jamaa. Mimi huwa siji Tanzania bila vitabu viwili vitatu vya kugawa kwenye shule au maktaba.
Katu said…
Hapo umenigusa haswa nategemea na wengine pia kwenye hilo la credit card....

Sasa Profesa Mbele vitabu vitanunuliwaje iwapo hakuna kuhaminiana kati waliopo ughaibuni na hapa nyumbani kwenye masuala yanayohusiana na pesa....!?

Kwa sababu utakaponunua huku kitabu utategemea kurudishiwa pesa yako na wewe kutumia huduma ya tovuti ya benki yako ya ughaibuni ama nyumbani Tanzania.

Na pia tukumbuke kuwa watu dhuluma hawana lebal Profesa Mbele....!!!!??

Ni ngumu kujua yupi ni yupi na matokea yake watanzania ughaibuni wanatakuwa makini sana na pesa zao

Nafikiri hili suala na mada nyingine pia inatakiwa kufanyiwa uchunguzi na utafiti wa kina kuifahamisha jamiii ya kitanzania.Au unasemaje hapo Profesa Mbele!

Nguvu ya teknolojia ya mawasiliano inaniwezesha kuwakilisha mawazo na maoni yangu binafsi kutoka hapa Lungongole-Kikwawila-Ifakara
Mbele said…
Ndugu Katu, mimi ninaponunua vitabu ambavyo navigawa mashuleni na kwenye maktaba Tanzania, huwa navitoa bure.

Kama kila mmoja wetu akifanya kitu cha maendeleo, hata kama ni kwa kiasi kidogo, tutaanza kuleta mabadiliko nchini mwetu. Ninajua kuwa kupeleka kamusi ya ki-Ingereza kwenye sekondari ya Tunduru si lazima ningoje sera kutoka CCM au ningoje hadi utakapotoweka ufisadi na utapeli katika jamii ya wa-Tanzania.

Ninajua kuwa kamusi ile moja ya ki-Ingereza italeta mapinduzi katika ile shule ya Tunduru, mapinduzi katika ufundishaji wa lugha ya ki-Ingereza. Mwalimu ataweza kujua kwa uhakika neno "arrive" linaandikwaje, na atawafundisha watoto maandishi sahihi.

Hayo ni mapinduzi yanayotokana na kupeleka kitabu kimoja. Leo nimesoma taarifa kuwa wa-Tanzania waliopo Dar wamechanga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kampeni za CCM mkoani Kilimanjaro.

Wangenigawia milioni 10 kati ya hizo, ningeweza kupeleka kamusi za ki-Ingereza katika shule nyingi kwenye kila mkoa.

Jamii ya ki-Tanzania imefilisika kimawazo na haijali. Itakomeshwa na ulimwengu.
Katu said…
Nimeshukuru sana na kufarijika na mtazamo wako kuona moyo wako wa kuleta mabadiliko ya kweli ktk jamii ya kitanzania hasa baada ya kuandika hili suala linalonihumiza kichwa kila kunapokucha asubuhi na jua kuzama jioni na nukuu...."Jamii ya ki-Tanzania imefilisika kimawazo na haijali. Itakomeshwa na ulimwengu"....

Hawa watu kilimanjaro wanachangia hiyo kiasi hicho cha pesa imetoka wapi na wanafaidika kivipi na hao wanaowachangia...!!!!!!?

Kifupi hiyo pesa iliyochangwa na wakazi wa Kilimanjaro ingechangishwa kwa ajili ya kufufua kilimo cha zao la kahawa ingeweza kuleta maendeleo zaidi ya hapo wanapoona wao watu kutoka mkoa huu waliopofikia ktk suala la maendeleo.

Nguvu ya teknolojia ya mawasiliano inaniwezesha kuwakilisha mawazo na maoni yangu binafsi kutoka hapa Lungongole-Kikwawila-Ifakara.
mimi ninatumia card ya benki inayodai kuwa kuna visa, na nyingine mastercard lakini utumiaji wake ni imposible kila nijaribupo kuitumia kule wanakojinadi kuwa zinakubalika

inabidi ufanye haraka utupatie acces ya kitabu hicho, usiandikie walioko ughaibuni pekeee
SN said…
Mimi ni mgeni kidogo hapa. Na nimefurahi kukutana na hii makala/huu mjadala.

Prof. Mbele, hongera kwa kuandika kitabu! Kwa kifupi, mimi binafsi nimeanza kuandika kitabu cha hadithi fupi za Kiswahili ambazo malengo yake yake makubwa ni kuanzisha mijadala ya mambo yanayotokea kwenye jamii (na kuiamsha fasihi yetu kwa ujumla).

Kwahiyo nitaendelea kufuatilia hii makala na maoni ya watu; lengo haswa ni kujua nini nikitegemee huko mbeleni.e
kwa ushauri zaid kwa SN nunu kitabu hiki na vingine vya prof ili unakili baadhi ya maandishi yake! bila shaka itapendeza na prof atafuarahia zaidi na zaidi
Mbele said…
Ndugu SN, nakutakia mafanikio katika uandishi wako. Kuna mambo mengi ambayo naweza kukumegea. Ila mambo ni hatua kwa hatua. Kwa sasa, zingatia suala la kuandika mswada wako na kuufanya uwe mzuri na kamilifu kadiri unavyoweza. Ni jambo jema pia kuwaonyesha wanaojua zaidi wakusaidie kuunyoosha, kabla hujachapisha.

Hatua ya pili itakuja, ambayo ni nama ya kuchapisha kitabu chako. Unaweza, ukitaka, kutumia mtindo ninaotumia mimi, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika hii blogu yangu. Hii blogu nataka iwe kama darasa, masomo bila malipo.
SN said…
@ Kamala, ushauri wako ni mzuri ila baadhi ya watu huwaonya waandishi (hasa "creative writing") kusoma kazi za waandishi wengine hasa wakati unaandika kitabu chako. Hii husaidia kuepuka ile "influence" ya kazi ya mtu mwingine. Haitakuwa jambo la busara kama Prof. akija kusoma kitabu changu na kuona kuwa nimetumia karibia nahau na misamiati yake yote! Nitanunua kitabu chake BAADA ya kumaliza kuandika changu :).

@ Prof, Shukrani kwa ushauri. Nitautilia maanani na muda ukifika - baada ya kumaliza kuandika muswada wangu - nitakuandikia ili kujua ni hatua gani nyingine muhimu zifuatwe.
SN said…
Nilisahau kuwaambia kuwa hadithi zangu zinatapatikana hapa:

http://vijanafm.blogspot.com/2010/05/mungu-nimekukosea-nini.html

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini