"Lonely Planet" Waidhalilisha Arusha

Leo nimeona taarifa mtandaoni kuwa Lonely Planet hivi karibuni ilitoa taarifa ikiutaja mji wa Arusha katika orodha ya miji isiyofaa duniani. Arusha imeshika namba nane. Bofya hapa. Sikujua kuwa kuna taarifa ya namna hii, hadi leo, nilipoiona katika Jamii Forums. Bofya hapa.

Inaeleweka kwa nini wahusika wa mji wa Arusha na labda wa-Tanzania wengi wanaishutumu taarifa hii ya Lonely Planet. Mji wa Arusha unajulikana kwa utalii, na katika ushindani uliopo duniani, wahusika wote wanajitahidi kuwa na jina zuri, ili wafanikiwe kibiashara.

Pamoja na yote hayo, sisi wa-Tanzania tunapaswa kujifunza kutokana na makosa. Hii si mara ya kwanza watu wa nje kutangaza habari za nchi yetu kwa namna ambayo haitupendezi. Kwa mfano, tumelalamika kwa muda mrefu kuwa nchi jirani inatangaza kuwa Mlima Kilimanjaro uko kwao. Na sasa tunalalamikia hii taarifa ya Lonely Planet kuhusu Arusha. Je, tutalalamika mpaka lini? Je, tutaweza kushindana na hao wapinzani wetu kwa kulalamika tu?

Katika blogu zangu, na za wengine, na pia katika kitabu changu cha Changamoto, nimeandika tena na tena kuwa wa-Tanzania tuache uzembe. Tujibidishe katika elimu, ambayo ni pamoja na elimu ya lugha. Tuwe na uwezo wa kujieleza, kwa ufasaha na viwango vya juu kabisa, iwe ni kwa ki-Swahili au ki-Ingereza. Tuwe na tabia ya kununua na kusoma vitabu, kujiongezea maarifa na ujuzi, pamoja na ujuzi wa lugha.

Njia madhubuti ya kupambana na propaganda hizi tunazozilalamikia ni sisi wenyewe kuandika habari za nchi yetu na kuzisambaza duniani. Katika dunia ya leo, ya utandawazi na tekinolojia ya mawasiliano ya mtandaoni, uwanja uko wazi kwetu sote. Tutumie fursa hizi kama wanavyozitumia hao tunaowalalamikia.

Kama kweli tunaudhika na yale tunayofanyiwa, njia iliyopo ni hii ya kujibu mapigo. Binafsi, najitahidi kuandika habari zetu, kama njia moja ya kuipa dunia mtazamo wa m-Tanzania. Ninaandika kuhusu wa-Tanzania na wa-Afrika, kuhusu u-Tanzania na u-Afrika, ili kupambana na hao waliojivika kofia ya kuwa wasemaji wetu, wakati hatujawapa wadhifa huo.

Kampuni ya Lonely Planet ni kubwa sana duniani, ambayo vitabu vyake vinasomwa na watu zaidi ya 900,000. Mimi ni mtu moja tu, na sina mtandao na nguvu za kiuchumi namna hiyo. Lakini, hii sio sababu ya kukata tamaa. Cha msingi ni kujiamini. Wahenga walituachia busara katika methali zao. Walituambia, kwa mfano, kuwa mwanzo wa makubwa ni madogo na pia bandu bandu humaliza gogo.

Juzi tu kwenye blogu hii, bofya hapa, nilimnukuu msomaji wangu mmoja akisema kuwa kitabu cha Africans and Americans alikiona kuwa bora zaidi kuliko cha Lonely Planet. Pamoja na hali yangu ya chini sana nikifananisha na Lonely Planet, sina wasi wasi kuwa kadiri siku zinavyopita, nitalipunguza hili gogo liitwalo Lonely Planet.

Walichoandika Lonely Planet kuhusu Arusha kiwe ni changamoto kwetu wa-Tanzania, kwamba tusikae tunalalamika tu. Tupambane nao kwa vitendo.

Comments

Fadhy Mtanga said…
Prof Mbele tatizo la ulimwengu wa magharibi ni kuharibu sifa ya dunia yetu. Tunao wajibu Watanzania kujibu mapigi kwa kufanya jitihada kama usemavyo.
Nadhani sisi wanablog tunayo nafasi nzuri ya kuitangaza vema nchi yetu.
Watanzania wengi, hususani tuishio hapa hapa Bongo, hatupendi kuandika vitabu. Pengine gharama na ukosefu wa mitaji.
Lakini tunao wajibu kufanya hivi.
Tujenge mshikamano ili kuipigania nchi yetu ndani na nje ya mipaka.
Mbele said…
Ni kweli, hizi blogu nazo ni fursa nzuri tuliyo nayo ya kujieleza sisi wenyewe na kuitangaza nchi badala ya kutegemea au kunyanyasika na sauti na mitazamo ya wengine.

Tunazo blogu nyingi sisi wa-Tanzania, na kwa ujumla wake ni wimbi kubwa la sauti zetu ambalo linaenda duniani kote. Tukitambua hilo, tutajipanga vizuri ili tuandike, au tuyape kipaumbele yale yanayotekeleza ajenda tunayoongelea.
Bennet said…
Nashauri kama kuna mtu anasafiri sana hasa mbugani au kama ni mwongoza watalii, basi aanzishe blog yake na sisi sote tumsupport, siku hizi sisafiri sana mbugani ingekuwa miaka ya nyuma ningeanzisha mimi, ni mawazo tu
Mbele said…
Ndugu Bennet, naafiki kabisa wazo lako. Ni njia nzuri ya kujijengea tabia ya sisi kujieleza wenyewe na kuilezea nchi yetu sisi wenyewe, kwa mtazamo wetu.

Nitaendesha warsha Meeting Point Tanga (tarehe 12 Juni), Arusha Community Church (tarehe 3 Julai), na sehemu zingine mbili tatu, kuhusu masuala ya utamaduni na utandawazi, na suala la utalii litakuwemo. Mawazo kama haya yako yatawekwa bayana, kama changamoto kwa washiriki, kuwahamasisha kufikiria mikakati ya kujinasua na kushindana katkka ulimwengu wa leo wa utandawazi.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini