Kitabu "Qur'an and Woman" Kimewasili

Ninafurahi kwamba kitabu nilichoagiza hivi karibuni, Qur'an and Woman, kilichotungwa na Amina Wadud, nilikipata jana. Siku chache zilizopia, katika blogu hii, niliandika kuwa nimeagiza kitabu hiki.

Niliagiza kitabu hiki ili nikisome, kama sehemu ya maandalizi ya kufundisha kozi mpya, "Muslim Women Writers" hapa chuoni St. Olaf, juu ya fasihi iliyoandikwa na wanawake wa ki-Islam kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Mara nilipokipata, nilisoma utangulizi, ambao umenivutia, kwa jinsi ulivyoelezea mambo yaliyomo kitabuni. Mwandishi alifanya utafiti wa miaka kadhaa katika kuandaa kitabu hiki, ambacho kinaweka wazi vigezo vya kutathmini nafasi ya mwanamke katika u-Islam.

Mwandishi anasema kuwa aliamua kusimama na kuzama katika Qur'an, kwa kuwa hiki ni kitabu kinachokubalika na kuheshimiwa na wa-Islam wote, pasipo wasi wasi wala ubishi. Kwa hivi, ili kuelezea nafasi ya mwanamke katika u-Islam, aliona ni muhimu kujikita katika Qur'an.

Mwandishi anasema kwamba katika jamii za ki-Islam, wanawake wana hadhi duni kwa kulinganisha na wanaume. Lakini, ili kubaini hadhi ya wanawake katika u-Islam, hatuwezi kuzingatia hali yao katika jamii, bali turudi katika Qur'an. Katika utafiti wake wa kina wa Qur'an, amethibitisha kuwa Qur'an haimweki mwanamke chini ya mwanamme. Inamweka kama mshirika wa mwanaume, na wote wawili wanategemeana, bila mmoja kuwa bora au juu ya mwenzake. Anaandika:

Mercifully, the more research I did into the Qur'an, unfettered by centuries of historical androcentric reading and Arabo-Islamic cultural predilections, the more affirmed I was that in Islam the female person was intended to be primordially, cosmologically, eschatologically, spiritually, and morally a full human being, equal to all who accepted Allah as Lord, Muhammad as prophet, and Islam as din.

Huu ndio mtindo wa uandishi anaotumia Amina Wadud, lugha pevu inayopiga shabaha kwenye hoja. Kwa leo, sitataja kila kilichomo katika utangulizi wake. Nitabakiza  kiporo, nimpe msomaji fursa ya kucheua hicho kiasi. Nitaendelea siku nyingine, Insh'Allah. Ninaandika mambo hayo kama namna ya kujidhihirishia maendeleo yangu katika kutafuta elimu.

Comments

Hongera! Japo wapo takaoshangaa 'hongera' kwa jambo gani? Kwa kupata kitabu na kusoma japo kwa utangaulizi tu. Huku kwetu mtu hapewi hongera kwa kupata kitabu seuze kukisoma. Hongera Prof. Bila shaka yapo mengi ya kujifunza na nitajitahidi kutafuta kopi yangu ya kitabu hicho. Kipo kitabu 'History of Islam' ambacho nacho kilieleza nafasi ya mwanamke katika Uislamu kwa kuwataja hasa wanawake shupavu walioshiriki vita sambamba na wanaume na kila mmoja kwa nafasi yake. Wanaume mstari wa mbele wanawake wakitoa huduma muhimu kwa wapiganaji.

Shida ya kitamaduni ni pale, tamaduni au dini moja inapomtizama mwanamke katika mizani ya tamaduni yake kisha kudai kuwa wao jinsia mbili zina usawa na tamaduni au dini nyingine hazina usawa. La msingi ni kuwa yapo ambayo usawa wa jinsia ni muhimu na lazima na yapo mambo tofauti zilizopo ndio usawa wenyewe. Mathalani, mwanamke kuwa na choo chake na mwanaume kuwa na choo chao. Huo ndio usawa wenyewe.

Si dhani kwamba ni usawa wa maana sana kuwa na bondia mwanaume na mwanamke wapambane ulingoni.

Tusome na tutafakari.

Mbele said…
Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ujumbe wako. Tuko njia moja katika kutafuta elimu, na juhudi yako ya kunitajia vitabu vingine naiangalia kwa mtazamo huo. Tunatambua kuwa elimu ni bahari kubwa na kile tunachokijua ni kama tone. Hatupaswi kuridhika na tone. Na nimesoma kwa miaka na miaka kuwa u-Islam unahimiza elimu. Kwa maana hiyo, mu-Islam anapaswa kuwa mtafuta elimu makini. Amina Wadud naye amekumbushia hilo katika kitabu chake. Hayo nitaongelea siku zijazo, Insh'Allah, kama nilivyogusia.

Ni kweli, kuna vitabu na maandishi mengine mengi kuhusu suala hilo la u-Islam na mwanamke. Kama nilivyosema siku zilizopita, ninaelekeza nguvu zangu wakati huu kwenye suala hilo katika kujiandaa kufundisha kozi yangu. Kusoma haya maandishi ambayo tunayaongelea ni kujijengea msingi na mfumo wa fikra na mitazamo itakayotusaidia katika kuzichambua kazi za fasihi. Kazi za fasihi zina upekee wake na uchambuzi wake ndio jukumu tutakalokuwa nalo muhula wote wa masomo.
Faraja ilioje kuwa na mimi leo hii nimeipata softcopy ya kitabu hicho. Japo hakikuwepo katika list ya vitabu vya kusomwa mwezi huu, nitajihidi kupitia kwa juu juu na baada ya kumaliza kusoma nitatoa maoni yangu juu ya asemayo mwandishi siku za usoni, Insha Allah.

Tafadhali, nitafurahi kusoma 'uhakiki au maoni yako' baada ya kuwa umemaliza kusoma. Ahsante.
Mbele said…
Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Hongera kwa kukitafuta na kujipatia kitabu hiki. Hii duku duku ya kutafuta elimu ndio ishara ya kuelimika. Kwa ki-Ingereza huitwa "intellectual curiosity." Nilidokeza siku chache zilizopita kwamba himizo la kutafuta elimu limo katika mafundisho ya u-Islam. Kwa hilo, ni wazi kuwa wewe unafuata njia sahihi ya u-Islam. Nakupa hongera.

Narudi kwenye hiki kitabu. Nami nitafanya juhudi niendelee kukisoma hadi mwisho. Wahenga walisema, maji ukiyavulia nguo, sherti uyaoge. Huko mbele ya safari huenda tutaweza kubadilishana mawazo vizuri zaidi.

Papo hapo, tunakubaliana kwamba kuna vitabu vingine na maandishi mengine mengi juu ya suala hili la Qur'an na mwanamke, au u-Islam na mwanamke. Tena, bila shaka wako watafiti wengine ambao nao wamo kazini na watachapisha vitabu na makala. Kwa hivi, hatuwezi kusema kitabu fulani ndio pekee chenye ukweli. Ingekuwa tuna uwezo tungejitahidi kusoma kila kilichopo, hadi mwisho wa uhai wetu.

Tuombe uzima, tuweze kuendelea kujielimisha na kuelimishana.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini