Kitabu cha "Siasa Hapo Kale"

Ninasoma Siasa Hapo Kale, kitabu ambacho nilikifahamu na kukipenda tangu nilipokuwa nasoma shule ya msingi kule nyumbani kwangu Litembo, katika mkoa wa Ruvuma. Mtunzi wa kitabu hiki ni Lucius Mabasha Thonya. Kama sikosei, nilikuwa na nakala ya kitabu hiki miaka ile kijijini kwangu. Ingawa sijui kilienda wapi, mara moja moja nimekikumbuka, hasa kwa vile mimi ni mtafiti katika fasihi simulizi. Hilo ni jambo moja katika utangulizi wa makala ya leo.

Jambo jingine ni kuwa kwa miaka kadhaa, nimevutiwa na juhudi za Dada Yasinta katika kudumisha lugha ya ki-Ngoni kwa kuanzisha na kuendesha blogu ya Vangoni. Ingawa ki-Ngoni sio lugha yangu, ninaielewa kiasi fulani nikiisikia au kuisoma, kwa vile inakaribiana na lugha yangu ya ki-Matengo.

Katika kusoma blogu ya Vangoni, nilipata wazo la kumwambia Dada Yasinta kuhusu kitabu hiki cha Siasa Hapo Kale. Hatimaye, nilimpelekea ujumbe, nikijua kuwa atapenda kusikia habari zake, na ndivyo ilivyokuwa. Kupitia maktaba ya hapa chuoni ninapofundisha, nilikipata kwa kutumia utaratibu unaotumiwa na maktaba wa kuazimishana vitabu na machapisho mengine, utaratibu uitwao "interlibrary loan."

Nilifurahi kukipata. Nilitengeneza nakala nikampelekea Dada Yasinta, naye aliandika habari hiyo katika blogu yake.

Siasa Hapo Kale ni mkusanyiko wa methali za ki-Ngoni, ambazo mtunzi amezitungia hadithi za kuzielezea. Katika maelezo yake, amefanikiwa vizuri kutupa maana na matumizi ya methali hizi, kwa kutumia maisha na mahusiano ya wahusika katika hadithi hizo. Anahitimisha kila hadithi kwa kusisitiza ujumbe muhimu uliomo katika methali. Kwa maneno yake mtunzi mwenyewe:

Hadithi zilizomo kitabuni humu zimesimuliwa kwa njia ya kubuniwa tu kupatana na mambo yalivyoweza kutokea katika maisha ya watu wa zamani zile. Hadithi hizo zimebuniwa ili kuwaangalisha wasomaji katika matukio ya namna mbalimbali yalivyopata kutokea katika kabila la Wangoni wa wilaya ya Songea iliyopo kusini mwa Tanganyika iliyo karibu na ziwa Nyasa.

Methali hizi zinathibitisha busara za wahenga, yenye falsafa, maadili, na mafundisho muhimu ya maisha. Napenda kunukuu baadhi ya methali, na tafsiri zilizomo kitabuni: "Njala likoko, yikoma na mhavi" (Njaa ni adui, hata mchawi inaua). "Mbanga kufwata manji kwegihamba" (Fuata maji yanakokwenda). "Katumbi ka ngolyongo ikwela mwe ngolyongo" (Utando wa buibui akwea yeye mwenyewe tu). "Mheka pangende kumwoyo lwitimba lungi" (Yu mcheshi machoni moyoni kuna mengine). "Imekela kandumba ka ngemelelu" (Ajivunia dawa ya bahati).

Mwandishi alifanya kazi kubwa ya kufikiri katika kuzitunga hadithi zilizomo kitabuni. Vile vile, ameandika kwa ki-Swahili sanifu, kinachovutia. Kitabu hiki kilichapishwa mwaka 1960, nami nakumbuka kuwa waandishi maarufu kama Shaaban Robert walikuwa bado hai. Miaka ile ya zamani, shirika la uchapishaji la East African Literature Bureau lilikuwa makini katika kuangalia matumizi ya lugha, kabla ya kuchapisha kitabu.

Comments

Simenya said…
Nimekuwa nikitafuta hiki kitabu mtandaoni ndipo nikafika ukurasa huu. Nilikisoma nikiwa mdogo na kilikuwa cha mafunzo na ngano tamu. Hata ingawa mimi si Mngoni bado nakumbuka hizo medhali za Kingoni. Baadhi ya medhali ni "kita wifuna kukoma liyoka (lijoka), tova ku mutu. Je naweza kununua hiki kitabu wapi?

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini