
Uhuru tulipata tarehe 9 Desemba, 1961. Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, na ninakumbuka msisimko, hata kule kijijini kwangu. Waalimu wetu, Charles Kinunda, John Pantaleon Mbonde, na Alois Turuka, walikuwa chanzo kikubwa cha ufahamu wetu wa mambo yaliyokuwa yanatokea.
Kati ya kumbukumbu ambazo haziwezi kutoweka akilini mwangu ni picha ya askari Alexander Nyirenda akiweka mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro. Sambamba na tukio hili la kihistoria ni hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, ambamo alisema:
Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau.


Hayo yote, tangu enzi za harakati za Uhuru hadi miaka ya mwisho mwisho ya sabini na kitu, yalifanyika chini ya uongozi wa chama cha TANU. Mtazamo na mwelekeo wa TANU ulikuwa wa kuongoza mapinduzi, kufuatana na mazingira ya kihistoria: kwanza ilikuwa kuwaunganisha wa-Tanganyika na kuwaongoza katika kupigania Uhuru, halafu, kuongoza harakati za kujenga ujamaa na kujitegemea.
Mwalimu Nyerere alifahamu fika kwamba Uhuru haukuwa mwisho wa safari. Kulikuwa na haja ya kupambana na urithi wa ukoloni, yaani ukoloni mamboleo na kuleta uhuru wa kweli, unaodhihirishwa na hali ya kujitegemea chini ya uongozi bora.
Miaka ilivyopita, baada ya chama kipya cha CCM kushika hatamu, hali ilikuwa hiyo kwa kipindi cha mwanzo. Lakini, pole pole, mwelekeo huu wa kuwa daima katika harakati za mapinduzi, ulianza kubadilika. Chini ya sera za CCM, kama vile "Azimio la Zanzibar," nchi imeendelea kuzama zaidi na zaidi katika mfumo wa matabaka na ukoloni mamboleo. Kwa lugha rahisi, CCM ni mhujumu wa Mapinduzi.
Ndoto na mategemeo ya Uhuru yametekwa nyara. Pamoja na kwamba tunasherehekea Uhuru tuliojipatia mwaka 1961, tutambue, kama TANU ilivyotambua, kuwa ule haukuwa mwisho wa safari. Enzi za TANU, tulitegemea kuwa tutajenga nchi ambayo iko chini ya mamlaka ya wakulima na wafanyakazi. Lakini, kama nilivyosema hapa juu, tunazidi kuzama katika ukoloni mamboleo. Wakulima na wafanyakazi, pamoja na washiriki wao, bado wana jukumu la kuendeleza harakati za kutafuta Uhuru wa kweli.