Sunday, April 5, 2009

Kujichapishia Vitabu

Tangu shughuli ya uchapishaji wa vitabu ilipoanza nchini mwetu, wakati wa ukoloni, kuchapishwa kwa kitabu kulitegemea uamuzi wa mchapishaji. Waandishi hawakuwa na madaraka juu ya mchapishaji bali walikuwa kama watumwa mbele ya mchapishaji. Hali hii haikuwa kwa upande wa vitabu tu, bali hata aina nyingine za maandishi. Watunzi wa mashairi, kwa mfano, au insha, walikuwa chini ya himaya ya wahariri na wachapishaji pia. Ilikuwa ni kawaida kwa waandishi wa mashairi kuanza shairi kwa kumbembeleza mhariri asiwatupe kapuni.

Ukifanya utafiti kuhusu yule mwandishi wetu maarufu, Shaaban Robert, kwa mfano, utaona kuwa pamoja na kipaji kikubwa alichokuwa nacho, hakuwa na madaraka juu ya wachapishaji wake. Hali hii ya waandishi kuwategemea wachapishaji bado haijabadilika nchini Tanzania. Wachapishaji wameendelea kuwa kama miungu, na waandishi wanalalamika sana kuhusu wachapishaji. Malalamiko ni ya namna nyingi, kama vile kucheleweshwa taarifa kuhusu miswada, kucheleweshwa kuchapishwa miswada, kucheleweshwa malipo ya ruzuku ya uandishi, au kutolipwa kabisa.

Sio jambo jema kwa waandishi wetu kubaki na mtazamo tegemezi, tuliorithi tangu zamani. Dunia inabadilika. Mabadiliko hayo yapo pia katika uwanja wa uchapishaji vitabu. Maendeleo ya tekinolojia yamefikia mahali ambapo mwandishi anaweza kujichapishia vitabu vyake bila kutegemea wachapishaji.

Niligundua hayo miaka kumi na kidogo iliyopita, nilipokuwa tayari kuchapisha kitabu changu cha hadithi za waMatengo. Nilikuwa nimesikia na kusoma kuhusu kuwepo kwa tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Nilifanya utafiti, nikaona aina mbali mbali za uchapishaji huo. Hatimaye, niliamua kuchapisha kitabu changu kwenye kampuni mojawapo. Niliendelea kuandika, na papo hapo nikaendelea kufanya utafiti juu ya tekinolojia ya uchapishaji. Hatimaye, nikagundua kampuni iliyonivutia zaidi, na huko ndiko ninachapisha vitabu vyangu.

Ushauri wangu kwa waandishi wa Tanzania na kwingineko ni kuwa badala ya kukaa na kuendelea na jadi ya kuwalalamikia wachapishaji, watafakari suala la kujichapishia wenyewe vitabu vyao. Kitu cha msingi ni kuhakikisha mswada umeandikwa vizuri na kuhaririwa kikamilifu. Kwa kawaida, mswada unachapishwa mtandaoni kama ulivyoandikwa, hata kama una makosa. Hakuna huduma ya uhariri. Hii ndio tahadhari. Vinginevyo, kama mswada umeshakuwa tayari, uchapishaji unaweza kuchukua dakika chache tu, badala ya miezi au miaka, kama ilivyo sasa. Leo hii, kutokana na maendeleo ya tekinolojia, kila mtu anaweza kuchapisha kitabu chake.

26 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Profesa. Hapa umegusia jambo kubwa, la muhimu na zito. Wachapishaji ni mojawapo vipingamizi vikubwa kwa nini Tanzania sekta ya vitabu - kutoka uchapishaji mpaka usomaji wake -bado imedorora. Mimi mwenyewe nina miswada ya vitabu viwili hapa lakini nimeshindwa nivipeleke wapi. Mchapishaji mmoja aliyeko Arusha alisema nijaze fomu na kutoka hapo sijamsikia tena. Wazo hili la kujichapishia vitabu ni wazo la kimapinduzi. Hata hivyo nadhani kwamba inategemea ni vitabu gani na vimeandikwa kwa lugha gani. Vitabu vyako vyote vimeandikwa kwa Kiingereza na mada zake kwa ujumla ni mada ambazo naweza kusema ni za kimataifa (hadithi za Kimatengo, mwongozo wa Things Fall Apart na kile kingine cha utamaduni). Je, vingekuwa vimeandikwa kwa Kiswahili bado ungetumia huyo mchapishaji uliyenaye? Kuna mchapishaji wa mtandaoni ambaye anaweza kukubali vitabu vya Kiswahili? Nitashukuru sana kwa maoni yako kuhusu suala hili.

Mbele said...

Shukrani kwa ulizo lako. Kuna aina nyingi za uchapishaji huu wa mtandaoni. Kuna sehemu ambako kuna watu wanaoangalia miswada na kisha kuiweka kwenye mitambo ya uchapishaji. Hao wanatoa pia huduma za uhariri. Kuna sehemu ambako mwandishi unachangia fedha kulipia gharama ya uchapishaji.

Lakini kuna sehemu ambako yote hayo hayako. Wewe mwandishi unaenda kwenye kompyuta na diski ya mswada wako, au faili pepe la mswada wako. Unautumbukiza huko mtandaoni mswada huo wewe mwenyewe. Mtindo huu wa kujitegemea ndio ninaotumia katika kuchapisha vitabu vyangu. Ni kama unavyofanya unapoweka makala au picha kwenye blogu yako.

Mimi natumia mitambo ya mtandaoni ya lulu ambayo iliandaliwa na mjasiriamali Bob Young, kwa lengo la kumwezesha yeyote kuchapisha kitabu chake. Hakuna ubaguzi. Unaweza kuchapisha kitabu cha lugha yoyote, na hata vitabu vya kiSwahili nimeviona huko. Uamuzi wa kuchapisha ni wako wewe mwandishi. Hakuna mtu mwingine ambaye yuko pale kuukubali, kuukataa au kuurekebisha mswada wako. Uamuzi ni juu yako wewe mwandishi.

Kuna masuala mengi yanayotokana na hii tekinolojia mpya. Suala mojawapo ni kuwa hakuna udhibiti wa nini kinachochapishwa. Tekinolojia hii imeleta uhuru kamili na demokrasia katika uchapishaji. Kila mtu anaweza kuchapisha kitabu, hata kama ameandika upupu mtupu, usio na kichwa wala miguu.

Simon Kitururu said...

Uhuru huu wa kuchapisha unatisha pia hasa ukizingatia kuwa kuna wasomaji ambao ni wavivu kuchambua ni nani wakutilia maanani katika hoja ikiwa hata asiye na hoja anaweza kuchukuliwa ndiye aongeaye KWELI TUPU kwa sababu haandiki mcharazo.

Katika kuangalia nani anaaminika...

Nakumbuka miaka fulani nilishawahi kubishiwa na fundi viatu mmoja ambaye hajawahi kuondoka Morogoro kuhusu MENYU za kwenye ndege , wakati mimi ndiye nimekuja Tanzania kwa ndege lakini yeye ndiye aaminiwaye mtaani kwa simulizi zake za kuanzia Simba na Yanga, Mbunge anahawala wapi, mpaka kwa nini hakuna Rais Mwinyi akoseapo.

Nachojaribu kusema ni; hili swala la kujichapishia linazalisha pia mpaka magazeti ya ajabu Tanzania ambayo utashangaa kuwa asilimia kubwa ya watu ndio huchukulia kuwa ndio chanzo cha maarifa cha kuaminika wakati hata habari zake hazijatafitiwa na aliye andika. Na hili naamini litakuja vitabuni ukizingatia lipo tayari kwenye blogu.



Uhuru pamoja na kuwa na faida zake, naamini kuna watakao amini uongo na kudharau ukweli kutokana na hili.

Na naamini tatizo hili lipo mpaka katika demokrasia ya Tanzania kwa ujumla ambapo unaweza kuahidi mpaka mbingu wakati ya dunia huyawezi kwa kuwanunulia wapiga kura ubwabwa ukaaminika unauwezo katika jamii ambayo kielimu wengi hawaelewi uchumi unavyokwenda na wala haki zao binafsi.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mmenifungua macho kwani mpaka sasa nimeandika miswaada mitatu haijatoka hata moja. nimeandika juu ya vijana na maisha ya leo, juu ya albino na juu ya mahakama ya kadhi na OIC sasa nitajaribu njia hizi.

Mbele said...

Ndugu Kamala, lengo langu lilikuwa hilo hilo la kuwafungua macho wengine, baada ya mimi mwenyewe kugundua hii njia na kuona faida zake. Nimeshawapa ushauri watu kadhaa kutoka sehemu mbali mbali duniani, na wamechapisha vitabu vyao kwa mtindo huo.

Ukiwa na muda, anza kusoma kidogo kidogo maelezo yaliyopo hapo lulu. Huna haja ya kuzunguka, bali anzia hapo panapoelezea uchapishaji. Huwa niko tayari kutoa maelezo ya ziada kwa wenye kuniuliza, maana nina kauzoefu ka kutosha.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ahasant prof. naazia hapa. nikishindwa ntakutafuta

Longolongo said...

Profesa hii ni mada muhimu sana,na ninafurahi kukutana nayo.mimi nina kitabu changu(comic book)ambacho hakijamalizika ambapo nanuia kutoa elimu kwa jamii yetu kuhusu magonjwa mbalimbali kwa mtindo wa hadithi za picha.Naamini kwamba njia hii ni rahisi zaidi kuwavutia watu kusoma vitabu.Sasa sijui hao lulu kama wanashughulika pia na vitabu vya namna hii.Kwenye website yangu(changa)www.afyachoice.com ambayo naitumia kama kufnya mazoezi ya kuandika na kujikumbushia kuchora(maana nilikuwa sijchora kwa muda sasa) nimewek baadhi ya cartoons,na nilipanga kuitumia hiyo kutafuta publishers..nashukuru sana kwa mwanga uliotoa.
Fredirick

Samuel Aron Barabara said...

Prof Mbele, nimefurahi sana kukutana na mada hii hapa, mimi pia ninakitabu changu, ninahitaji Kama inawezekana nifike Ofisini kwako kwa Ushauri zaidi, Asante sana Brother Sam Aron. 0754 469057

Mbele said...

Ndugu Sam Aron,

Shukrani kwa ujumbe, na hongera kwa kuandika mswada wa kitabu. Namba ya simu yako inanipa picha kuwa uko Tanzania, kumbe mimi niko huku Marekani. Kama ni hivyo, itabidi ujaribu kujichapishia, endapo mswada wako tayari uko katika disketi au compyuta, yaani "digital file."

Ukitaka kutumia mitambo ya lulu.com, utaona kuwa kuna maelezo ya hatua kwa hatua ya namna ya kufanya. Mimi ingawa sikuwa na uzoefu wa tekinolojia hizi, niliweza kufanya hivyo, na hatimaye nikaanza hata kuwasaidia wengine, tukiwa mbele ya kompyuta.

Jaribu kuingia hapo lulu.com kwenye sehemu ya "Create," ufuatilie. Unaweza kuniandikia tena na tena, ikibidi.

Kila la heri.

Christian Sikapundwa said...

Tuna kushukuru sana Frofesa Mbele kwa kuwapa moya waandishi wa vitabu.Ni ukweli usipingika kuwa waandishi wengi wa vitambu wanashindwa kifikia malengo yao kwa sababu ya miswada yao kuishia kapuni au kuibiwa na kuambiwa haina kiwango cha kuwa chapwa, lakini pia kukosa 'Publisher' atakaye mhariria kazi yaka ili mswada uweze kuchapishwa.

Mbele said...

Mzee Sikapundwa

Shukrani kwa ujumbe. Kwa kweli hao waandishi wetu wakifuatilia dokezo ninazotoa katika blogu hii, wataweza kupata ufumbuzi. wa matatizo haya. Hasa wafuatilie suala la kuchapisha mtandaoni. Kuna aina mbali mbali za uchapishaji huo.

Kuna wa-Tanzania wengine wameingia katika uchapishaji wa aina hiyo katika lulu.com kama ninavyochapisha mimi. Lakini nashauri pia waandishi wafuatilie anavyochapisha Evarist Chahali, mmiliki wa blogu ya Kulikoni Ughaibuni.

Emmanuel Kachele said...

Na mimi napenda kuchangia, Kwanza nakushukuru sana kwa msaada wako juu ya kuchapisha kazi mtandaoni. Lakini mimi nina swali moja; kwa nini hapo pia umeeleza kuwa 'kampuni moja wapo' bila kutaja jina, kwa nini usitutajie na sisi ili tujue ni makampuni gani tunaweza kuyafuata na sisi ili tuweze kuchapa vitabu vyetu?
Kwa mfano, tunataka kujua ni nini sera ya makampuni ya uchapishaji kama vila Mkuki na Nyota, Oxford, na mengineyo katika uchapajia?
Kwa kweli tuko wengi wenye vipaji lakini kadiri muda unavyokwenda vinazidi kupotea.
Naomba msaada kwa hili!

Mbele said...

Ndugu Emmanuel Kachele

Ninaongelea uchapishaji wa mtandaoni, ambao umekuja kutokana na maendeleo ya tekinolojia. Ni tofauti sana na uchapishaji tuliozoea, wa makampuni kama haya uliyoyataja.

Nimeandika makala kadhaa katika blogu hii na katika kitabu changu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kuhusu uchapishaji wa mtandaoni, na nitaendelea kuandika kwa kuwa daima kuna mambo mapya ya kujifunza katika uwanja huu.

Hiyo niliyoiita kampuni mojawapo ni ile ambayo nilianza nayo. Ukifuatilia vizuri makala yangu, utaona kuwa niliendelea na utafiti, nikagundua kampuni bora zaidi. Tatizo kubwa la kampuni zile za mwanzo ni kuwa mwandishi ulitakiwa kulipia hela ili kitabu chako kichapishwe. Malipo yalitofautiana kutoka kampuni moja hadi nyingine, kwa mfano dola za ki-Marekani 300 hadi zaidi ya 1000.

Nilipogundua miaka ya baadaye kuwa tekinolojia imepiga hatua mbele, kumwezesha mwandishi kuchapisha kitabu bila malipo, na tena tekinolojia hiyo mpya inakuwezesha kuchapisha mswada wako ukawa kitabu tayari ndani ya dakika kadhaa tu, nikaamua kupendekeza hivyo, kama unavyoona katika makala yangu. Nisingewashauri watu waende kule kule ambako ni kugumu.

Mwakajila Frank A said...

Asante kwa ushauri mzuri mzee, Mimi ni mwandishi mchanga kwenye Tasnia hii ningependa kufahamu zaidi juu ya mchakato Mzima wa mswada hadi kufika hatua ya uchapishaji wa kitabu. Nina mawazo mengi juu ya uchapishaji lakini yanakosa mwelekeo wa kiujuzi. Chapisho lako limenifungua Ufahamu kwa kiasi na naomba niendelee kukusumbua kwa faragha.
Frank Mwakajila
mwakajila900@gmail.com
+255 755 457 971

mmassy said...

Mzee wangu Prof.Mbele nitakuwa sio mwenye busara kama sita kushukuru kwa kunifungua macho.Nilikuwa na jumla ya miswada 11 ambayo nilikuwa naumia kichwa kwamba nitaichapaje.Imenifungua kiasi cha kwamba nimeshachapisha NNE hadi sasa na ni siku ya pili tu tangia nimekusoma hapa na kutekeleza.Mungu akufunulie uendelee kutusaidia vijana was kitanzania tuendelee kuamsha vipaji vyetu ambavyo vilikaribia kupotea kutokana na ugumu ulio katika uchapishaji wa vitabu Tanzania.Changamoto iliyopo ni kwamba jamii hizi za kitanzania bado kununua vitabu online ni changamoto kubwa sana.Kila anayeona dollar anaona kama kazi za wazungu.Wengine wanasema wanataka kulipa kwa Tsh. Nadhani tushauri pia makampuni yaliyo maaminifu katika uchapishaji na yaliyo na bei rafiki kwetu.Ahsante sana
naitwa JEROME ERNEST MMASSY
Was Arusha

Mbele said...

Ndugu Jerome Ernest Mmassy

Shukrani kwa ujumbe wako. Nafurahi kuwa ushauri wangu umekusaidia. Lengo langu ni kuwanufaisha wengine kwa yale ninayookota huko na huko katika kujielimisha. Ualimu wangu hauishii darasani tu, bali pia huku uraiani ulikonikuta.

Changamoto kuhusu ununuaji wa vitabu miongoni mwa wa-Tanzania ziko, tena kubwa. Kwanza kukosekana kwa utamaduni wa kununua vitabu, hata kama vipo madukani. Pili ni kukosekana kwa utamaduni wa kusoma vitabu, hata kama viko maktabani. Ukienda maktabani, utawakuta wanafunzi. Likifanyika tamasha la vitabu, ni hivyo hivyo. Hutawaona wazazi, wanasiasa, wafanya kazi, wala wazee. Ni wanafunzi na waalimu.

Kuhusu kununua vitabu mtandaoni, inatakiwa mtu awe na "credit card." Sijui kama "credit card" za Tanzania zinaweza kutumiwa kununulia vitu nje ya Tanzania. Lakini, kwa vyovyote vile, kwa kuwa dunia yote inasonga mbele katika matumizi ya intaneti, ninategemea kuwa Tanzania nayo itafikia hatua ya kushiriki maendeleo hayo kikamilifu.

Ninasema kushiriki, kwa sababu ninaangalia pande mbali mbali. Ninaangalia upande wa sisi kununua bidhaa mtandaoni, lakini pia upande wa kuuza. Ninaongelea pia mambo kama haya ya wewe na mimi kuchapisha vitabu mtandaoni.

Nimeona vitabu ulivyochapisha hadi leo, na nimeona ni vitabu pepe. Mimi ninachapisha aina zote mbili, yaani kitabu pepe na kitabu halisi. Ninaagiza nakala za kitabu halisi, na kuwapelekea watu wanaohitaji. Kwa mtindo huo, akitokea mtu aliyeko Tanzania akahitaji kitabu, ninaweza kumpelekea akalipia kwa shilingi za Tanzania. Tena basi, sihitaji hata kukiona kitabu hicho, bali hapo hapo mtandaoni ninapoagiza ninaweka anwani ya mteja na ninalipia. Atapelekewa bila mimi kuhusika tena.

Godfrey Mutuli said...

una ushauri mzuri bwana professa.Nielezee baadhi ya mitandao inayochapisha vitabu ambayo yanaaminika.

Mbele said...


Shukrani ndugu Godfrey Mutuli, kwa ulizo lako kuhusu kuaminika. Mtandao nilioutaja hapo juu, uitwao lulu, hauna tatizo. Mwandishi unaweza ufuatilia kila kitu. Unaweza kufanya chochote na kitabu chako, kama vile kukirekebisha, kuongeza au kupunguza bei, kufuatilia idadi ya vitabu vinavyouzwa, na hela zinazoingia kwenye akaunti yako. Saa yoyote ukitaka, unaweza kukiondoa kitabu chako, kisichapishwe tena.

Mtandao wa www.amazon.com ni mwingine ambao unatumiwa sana na waandishi kuchapishia vitabu vyao. Nao ninaupendekeza bila wasi wasi.

Kwa kuwa tekinolojia ya uchapishaji mtandaoni inaendelea kuleta mambo mapya, sawa na tekinolojia zingine, nakushauri uwe unafuatilia mabadiliko haya mtandaoni.

Unknown said...

Shukrani prof. kwa kufanyika msaada kwa watu na mimi nikiwa miongoni mwao, nina maswali kadhaa ambayo yanahitaji msaada wako.

La kwanza; kwa kuelewa watanzania kununua vitabu mtandaoni bado ni changamoto nikaamua kutochapisha vitabu pepe kabisa nikachapisha vitabu halisi na nikaomba nakala nitumiwe ili niwafikidhie mwenyewe wale watakaokuwa wanahitaji kuvinunua kwa Tshs je hakuna gharama ya kuchapisha hivyo vitabu halisi badala ya vitabu pepe? Na je hakuna gharama yoyote ya kugharamia kutumiwa nakala kutoka lulu.com?

La pili; vipi ulinzi wa hiyo kazi yangu kwa mfano nimetumiwa nakala za kitabu changu halisi kutoka lulu.com na nikampelekea mpokeaji akaamua kutoa nakala na yeye na kuzisambaza nitakuwa na sauti gani ya kumdhibiti huyu mtu wakati kitabu changu kimeandaliwa nje ya Tanzania?

La mwish; je haitakuwa illegal kwa mimi kuwauzia watu hicho kitabu na wakati hakina uthibitidho wa hapa nchini endapo nitakiuza kama hardcopy kwa kuwapelekea mwenyewe hizo nakala??
Msaada hapo prof.

hydrazineazine@gmail.com

Mbele said...

Shukrani, ndugu Hydrazine Azine, kwa ujumbe wako. Masuali yako yanasisimua akili. Kuna sehemu mbali mbali mtandaoni ambapo unaweza kuchapisha vitabu halisi au vitabu pepe. Sehemu zingine unalipia na sehemu zingine, kama hapa lulu.com, hulipii. Mimi ninachapisha hapo lulu.com vitabu halisi na pia vitabu hivyo hivyo kama vitabu pepe. Silipii hata senti moja.

Hapa lulu.com na sehemu zingine kadhaa, dhana ya uchapishaji si hii iliyozoeleka. Kinachofanyika ni kuwa unauingiza mswada wako, ambao ni faili la kielektroniki, hapo mtandaoni. Kwa ki-Ingereza, hiyo huitwa "up-loading." Yaani kuna mtambo ambao unapokea mswada wako na wewe mwenyewe unatekeleza uchapishaji. Hicho kitabu kinabaki humo mtamboni kama faili la kielektroniki.

Wewe mwenyewe ukitaka kukipata hicho kitabu, unalipia kwa kutumia "credit card," na unachagua kama unataka kitabu halisi au kitabu pepe. Kama ni kitabu halisi, unaweka taarifa za wapi kitabu kipelekwe. Yaani unaweka anwani yako au ya yule unayetaka akipate.

Kwa hivyo, kujibu suali lako kuhusu gharama, ni kwamba kuna gharama ya kuagiza hicho kitabu, kiwe ni kitabu halisi au kitabu pepe. Lakini gharama ni nafuu kwako mwandishi kuliko kwa mnunuaji mwingine. Mwandishi unatambulika kwa "password" unayotumia kuingilia hapa mtandaoni kinapopatikana kitabu. Gharama sio ya kununulia tu, bali pia ya kusafirishia, ambayo unachagua mwenyewe, kwani kuna aina tofauti za usafirishaji.

Hayo ni maelezo ya kununua kitabu halisi. Kama unanunua kitabu pepe, basi unalipia, na unakishuhia katika kifaa chako cha kusomea, yaani "e-reader," au "e-book reader." Hii inaweza kuwa katika komputa yako au hata "cellphone." Mfano wa "e-book reader" ni Kindle, ambayo inatumika Amazon.com.

Suala la mtu kurudufu kitabu chako na kutoa nakala akauza ni ukiukwaji wa haki miliki. Hairuhusiwi kisheria na kimaadili. Lakini nchini mwetu na sehemu nyingi zingine kuna utovu wa elimu, au ustaarabu, au maadili. Kama wanavyopora kazi za wasanii, kama vile muziki, na maandishi ni hivyo hivyo. Hata humu mitandaoni kuna uporaji mwingi wa kazi za watu.

Ingepaswa mashuleni na vyuoni katika nchi yetu masuala haya ya haki miliki yafundishwe kikamilifu. Ingepaswa watu waelimishwe kuhusu kosa liitwalo "plagiarism." Lakini katika nchi yetu, hii inayoitwa elimu ni ovyo katika masuala haya.

Kuhusu kitabu kuwa kimeandaliwa nje ya Tanzania, ni suala la tekinolojia. Tekinolojia ya intaneti imefuta dhana ya mipaka ya nchi. Sijui nchi yetu imetafakari vipi masuala haya ya tekinolojia ya mtandao na utandawazi yanavyoathiri shughuli kama biashara. Sijui Tanzania imetafakari vipi suala la biashara za mtandaoni, makampuni ya mtandaoni, na kadhalika. Hilo suali lako la kitabu kuwa na uthibitisho nchini linaingia hapo. Kifupi ni kwamba tekinolojia inabadilika upesi, na inabadilisha kwa kasi mambo tuliyozoea, na tusipoendana na kasi hiyo, tutakwama.





Unknown said...

Thank you so much prof. kwa msaada wako God bless you.

Hadithi za Madaruweshi said...

Sina Swali Profesa, lakini nakushukuru kwa majibu yako mazuri na ya ufasaha kabisa. Tupo nyuma sana kifikra kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kusoma vitabu. Tunajali sana weledi wa fani fulani kwa minajili ya kupata riziki na wala si kwa ajili ya maarifa. Ulipo huko unapata taarifa za haraka kuhusu mageuzi ya Teknolojia. Tafadhali usisite kutujuza ili nasi tuendane na kasi hiyo. Blogu yako nimeipenda na umefanya kazi kubwa sana kutuelimisha. Mungu akubariki.

Mbele said...

Ndugu Fredrick Joseph

Shukrani sana kwa ujumbe wako. Mimi kama mwalimu ninawapenda watu wa aina yako, kwa sababu mnaheshimu elimu na mnatafuta elimu. Mimi kama mwalimu ninayejali kazi yangu ni mtafutaji makini wa elimu, ili kile ninachojifunza niweze kuwamegea wengine. Sijielimishi kwa ajili yangu pekee, bali kwa ajili ya wengine. Kwa hivo, tuko pamoja. Na kuna usemi wa ki-Ingereza, "Birds of a feather flock together," yaani ndege wanaofanana manyoya husafiri pamoja.

Naahidi nitaendelea kutafuta maarifa huku niliko ili nawe na watafutaji wenzako muendelee kunufaika. Tuendelee kubadilishana mawazo. Blogu hii ipo kwa ajili hiyo, na ndio maana nikaiita Hapa Kwetu. Karibuni sana.

Unknown said...

Pro Mbele,,nakushukuru Sana kwa makalahii nzuri inayo tuelimisha sisi waandishi was vitabu hasa wachanga katika tathnia hii.
Mimi nimewahi kutuma miswaada ya vitabu viwili katika kampuni Fulani, lakini nilicho ambulia ni kuambiwa gharama kubwa Sana ambayo sikuwatayari kukabiliana nayo na hatimayake niliambiwa Sina vigezo na miswaada yangu ikapotelea huko.

Shikrani zangu kwako kwa hi elimu, lakini ndugu pro Mbele sisi vijana bado hatuaminiki kuwa tunaweza kuandika vitabu, na sio vitabu tu hata katika jamii na shughuli zetu.Kijana Kama Mimi nimeamua kuwaandikia vijana wenzangu kitabu ambacho, kijana au mtu yeyote atakae kisoma atawaelewa vijana na kijana mwenyewe atajitambua na kupata nguvu na hali mpya ya kulipenda na kulijenga Taifa na kujipenda kijana na kulijenga kiuchumi,mahusiano,utamaduni nk.

Naamini nitatumia ushauri wako kukichapisha kitabu changu. Naomba barua pepe yako , yangu ni sospeterdamas744@gmail.com

Mwisho, ushauri kwa waandishi wenzangu, kabla hatujaanza kuandika vitabu vyetu vizuri ni vyema na hali tukafanya UTAFITI wa kutosha,KUJISOMEA vyakutosha na kuisoma hadhira tunayo ikusudia kuiandika.
Asante PRO MBELE, asanteni nyote.

Unknown said...

SOSPETER MUHUGO wa MWANZA TANZANIA

Mwl. said...

Nimependezwa sana na msaada wako Prof. Ninaomba namba zako za whatsap nitakutafuta ili nipate darasa Zaidi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...