Wednesday, April 15, 2009

Hadithi za waMatengo Minnesota

Jana nilifika hapa mjini St. Joseph, Minnesota, nikiwa mgeni wa vyuo vya St Benedict/St. John's. Nilialikwa na Profesa Lisa Ohm, ambaye alihudhuria semina niliyoshiriki kuiendesha miaka michache iliyopita, kuhusu hadithi za waSomali. Katika semina ile, Profesa Ohm alipata fursa ya kununua kitabu changu cha hadithi za Wamatengo. Baada ya kukisoma, aliniandikia ujumbe akisema kuwa amekipenda sana na akanipa tafakari yake kuhusu yaliyomo katika baadhi ya hadithi zile. Tafakari yake ilinifungua macho, kwani alinionyesha mambo ambayo sikuwa nimeyawazia, ingawa mimi ni mMatengo.

Profesa Ohm alinieleza kuwa anatumia kitabu kile cha hadithi za waMatengo katika kozi yake ya hadithi. Alisema pia kuwa hapo mjini St. Joseph wana kikundi cha watu ambao wamekuwa wakizisoma na kuzijadili hadithi zile. Ziara yangu ilitazamiwa kuwa fursa ya wanafunzi wake na wanakikundi kujifunza zaidi kuhusu hadithi na utamaduni wa waMatengo na waAfrika kwa ujumla.

Jana tulijumuika katika huo mjadala, ambao ulidumu kiasi cha saa nzima. Nilijitambulisha kifupi, na nikatoa fursa ya wao kuuliza masuali. Walikuwa na masuali mengi kuhusu vipengele mbali mbali vya hadithi za kiMatengo na utamaduni wao, na pia masuala ya hadithi kwa ujumla, wakizingatia yale niliyoandika katika kitabu changu.

Baadhi ya masuala yaliyojitokeza ni athari za kurekodi katika maandishi hadithi ambazo kwa asili yake ni za masimulizi ya mdomo. Katika hali yake ya kawaida, ya masimulizi, hadithi hizi hubadilika muda wote, hata kama ni kwa kiasi kidogo sana, kwani wasimuliaji hawakariri maneno ya hadithi. Wakiambiwa kusimulia tena na tena hadithi ile ile moja, tofauti nyingi zinajitokeza. Ukirekodi mara moja hadithi hiyo, kama tunavyofanya, na kisha kuiweka kitabuni, unakuwa umeipa sura ambayo haibadiliki, wakati katika mazingira yake halisi, hadithi hii haina sura moja.

Hili ni tatizo moja, ambalo nimelielezea katika kitabu changu. Yako masuala mengi mengine. Kwa mfano, kuna dhana zilizomo katika hadithi, ambazo undani na maana yake sisi watu wa leo hatuzielewi. Ni dhana za kale mno, na hata lugha inayotumiwa aghalabu hatuielewi, kwani nayo ni ya kale mno. Suala hili linajitokeza zaidi kwenye nyimbo zilizomo katika hadithi, na msingi wa tatizo ni kuwa nyimbo huwa na muundo maalum ambao si rahisi kubadilika, na kila kizazi kinarithi nyimbo hizi na kuziimba kama zilivyo. Watafiti wanakubaliana kuwa nyimbo ni kati ya vipengele vya hadithi ambavyo ni vigumu kabisa kubadilika.

Suala jingine lililojitokeza ni vitendo vya kutisha vilivyomo katika hadithi, kama vile vifo visivyo vya kawaida na mapambano baina ya binadamu na majitu ya kutisha. Leo waMarekani wengi wanajiuliza kama mambo hayo yanastahili kusimuliwa kwa watoto au la. Kumekuwa na juhudi ya miaka mingi Ulaya na Marekani ya kujaribu kurekebisha hadithi ili kupunguza vipengele hivyo vya kutisha, kwa hoja kwamba vinaweza kuwa na athari mbaya kwa watoto.

Binafsi, ninazingatia kuwa tangu enzi za mababu na mabibi, kuanzia huko kwetu hadi Ulaya na sehemu zingine duniani, jamii asilia hazikuwa na tatizo lolote kuhusu suala hilo. Hadithi hizi ndizo walizokuwa wanasimuliwa watoto, na hazikuwaathiri. Hata hadithi za waJerumani wa zamani, ambazo hatimaye zilirekodiwa na watafiti kama akina Jacob Grimm na mdogo wake Wilhelm Grimm, ambao walianza kuzichapisha mwaka 1812, zilikuwa na mambo ya kutisha au "yasiyofaa." Kuna malumbano miongoni mwa watafiti kuhusu suala la kama hao jamaa walizirekebisha kabla ya kuzichapisha.

Wanasaikolojia wa Marekani wanahangaika na masuali hayo, lakini kwa mtazamo wangu na uzoefu wangu wa kusimulia hadithi hizi kwa watu wazima na pia watoto wa hapa Marekani, naona labda watu wazima hawawaelewi vizuri watoto. Kila nilipopata fursa ya kuwasilimua watoto wa kiMarekani hadithi, wameonyesha kuvutiwa nazo kwa namna mbali mbali, hata kama zina mambo ambayo watu wazima wangesema yanatisha. Naona kuwa saikolojia ya watoto ni fumbo ambalo sisi watu wazima wa leo bado hatujalifumbua. Ni suala linalohitaji utafiti zaidi. Hayo yote nilipata fursa ya kuyaeleza kwenye mazungumzo ya jana.

Baada ya mjadala huo wa darasani, nilipata fursa ya kuongea tena kwa undani na Profesa Ohm, nyumbani kwake. Tuliongea kirefu, yeye, mume wake, na mimi, na Profesa Ohm alieleza kwa undani zaidi uchambuzi na tafakari yake kuhusu vipengele mbali mbali vya hadithi za kiMatengo. Aliniuliza pia masuali ya kufikirisha. Niliona jinsi anavyozama katika uchambuzi na kufichua mambo ambayo sikutegemea, yanayoonyesha falsafa nzito katika hadithi hizo. Pamoja na kuwa nami ni mtafiti, na ni mzaliwa katika utamaduni wa kiMatengo, ninakiri kuwa ninayo mengi ya kujifunza kutoka kwa watafiti makini kama Profesa Ohm. Nimeamini kwa miaka mingi kuwa mtu wa utamaduni tofauti anaweza kukuonyesha mambo yaliyomo katika utamaduni wako ambayo wewe mwenye utamaduni yatakufungua macho na akili kwa namna ambayo hukutegemea.

Sitasahau jambo hili, la kukutana na wageni hao, waMarekani, ambao wanazama namna hii katika kutafakari hadithi na utamaduni wa kwetu. Ni fundisho kwetu pia, kwamba tujizatiti kujifunza mambo ya wenzetu. Tutatambua tunavyofanana au kutofautiana, na tutajenga heshima kwa tamaduni zote, kwani kila utamaduni umesheheni hazina kubwa ya sanaa, falsafa na maadili ambayo kwa ujumla wake ni hazina kwetu binadamu wote.

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nimefurahi sana kusoma makala hii kwa kweli kama makabila yote ya TZ yangekuwa yanaandika hadithi zote zinazosimuliwa tungepata faida sana. Binafsi nimebahatika kusoma vitabu kadhaa vya hadithi za kingoni za mwandishi ANGELA AMANDUS HAULE. Nilifurahi sana kwani zilikuwa zile hadithi ambazo nilisimliwa nilipokuwa mdogo na babu na bibi yangu. Asante sana kwa kumbukumbu. Na endelea kutawanya mila na utamaduni wetu.

Albert Kissima said...

Profesa Mbele ninakiri kuwa unafanya kazi nzuri sana na hakika najivunia na kujituma kwako. Hakika unatuwakilisha vizuri sisi watanzania.

Hongera sana.

KITABU MUHIMU KWA MAJADILIANO

Tarehe 5 Oktoba, Profesa Artika Tyner anayefundisha sheria katika Chuo Kikuu cha St. Thomas, alikweka picha hii hapa kushoto, akaambatiisha ...