Siendi Mahali Kuuza Vitabu

Mimi ni mwalimu, mwelimishaji, darasani na katika jamii. Ili kufanikisha majukumu yangu, ni mtafutaji wa elimu bila kuchoka. Ni mwanafunzi muda wote ili kujiimarisha katika ualimu na uelimishaji.

Nafundisha na kujufunza kwa kuongea na watu ana kwa ana, iwe ni darasani au nje ya darasa. Nafundisha na kujifunza kwa mawasiliano ya masafa marefu, iwe kwa barua pepe au kwa simu. Hivi karibuni, nimeanza pia kutumia Skpe. Hizi zote ni njia za kuelimisha sambamba na kujielimisha.

Lakini vile vile, mimi ni mwandishi wa makala na vitabu. Kwa kawaida uandishi wa nakala huchukua muda mwingi, na vitabu ndio zaidi, kwani kitabu kinaweza kuchukua miaka kukiandaa na kukiandika. Kwa ujumla unaandika katika upweke. Nakubaliana na kauli ya Ernest Hemingway, "Writing, at its best, is a lonely life."

Kwangu mimi kama mwalimu naona uandishi wa aina ya vitabu ninavyoandika kuwa ni mwendelezo wa ufundishaji. Ninapokwenda na vitabu vyangu kwenye tamasha au maonesho, ninakwenda kama mwalimu. Siendi kufanya biashara.

Ni tofauti na mvuvi anapoenda na tenga lake la samaki sokoni, au mkulima anapoenda na mkungu wake wa ndizi. Hao wanaenda kuuza samaki au ndizi. Ikifika mwisho wa siku hawajauza hizo samaki au ndizi, wanaona wameshindwa biashara siku hiyo, au wanaona wamepata hasara.

Mimi, pamoja na kuwa ninaenda maoneshoni na vitabu vyangu, nisipouza hata kimoja sioni kama nimeshindwa kwani ninakuwa nimeshaongea na watu wengi, kuwaelimisha na kuelimishwa nao. Wengine huulizia kuhusu uandishi au uchapishaji wa vitabu. Wengine huulizia kuhusu masomo ninayofundisha au kuhusu utafiti wangu. Niligusia masuala haya katika blogu hii.

Hutokea, mara kwa mara, kuwa katika kuongelea mambo hayo, watu hao hupenda wenyewe kununua vitabu vyangu. Labda wanataka kufahamu zaidi fikra na mitazamo yangu. Labda wanataka kumbukumbu ya kukutana kwetu na maongezi yetu. Na hapo ndipo linapoingia suala la watu kutaka kusainiwa kitabu. Ni kumbukumbu.

Nikirejea tena kwa mvuvi muuza samaki au mkulima na mkungu wa ndizi, sijui kama kuna watu wanapokuwa sokoni wanaenda kumwuliza mvuvi habari za uvuvi au wanaenda kwa muuza ndizi kupata elimu kuhusu kilimo cha ndizi. Na sijui kama muuza samaki mwenyewe au muuza ndizi mwenyewe anategemea hivyo.

Zaidi ya yote, mimi kama mwalimu sina masaa ya kazi. Najiona niko kazini muda wote, tangu asuhuhi mpaka usiku, labda tu ninapokuwa katika majukumu mengine ya binafsi, familia, au jamii. Kama siko darasani, niko ofisini, maktabani, au nyumbani, ninasoma. Niko mahali ninatayarisha masomo au ninasahihisha kazi za wanafunzi. Hakuna jamii hapa duniani ambayo inamlipa mwalimu kwa masaa yote hayo anayokuwa kazini.

Kwa kurudia, ninapokuwa maoneshoni na vitabu vyangu, niko pale kama mwalimu. Si mfanyabiashara, ambaye anahesabu mafanikio yake kwa kigezo cha fedha anachopata siku hiyo.

Comments

Kaka Mbele usemayo ni kweli. Sikumbuki kutegemea pesa ya vitabu nilivyotunga. Kwa mtu mwenye taaluma yake si rahisi kutegemea vitabu zaidi ya kutoa mchango wa maarifa kwa jamii. Hebu fikiria ni watu wangapi wamenufaika na kitabu chako cha "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences."
Huwezi kulinganisha faida uliyotoa kwa jamii na kidogo wanacholipa watu kununua maarifa ambayo wanaishi nayo hadi kufa wakati pesa wanayolipa inaliwa na kuisha.
Mbele said…
Ndugu Mhango, shukrani kwa ujumbe. Niliona nijieleze kama nilivyojieleza, na nitaendelea kujieleza, ili walimwengu waelewe vizuri fikra na mitazamo yangu.

Kuna tatizo kubwa katika jamii yetu ya Tanzania, tatizo la kuabudu pesa, na kuiona pesa ndicho kigezo cha juu kabisa cha mafanikio.

Nathamini sana elimu, kwa maana ya kujielimisha mimi mwenyewe na kuwaelimisha wengine, kutumia elimu yangu kuwaelimisha wengine. Ninapima mafanikio yangu kwa kigezo hicho.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini