Sunday, September 18, 2022

Tanga Watafakari Changamoto za Tofauti za Tamaduni


Tarehe 11 Juni, 2022, nilikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kwanza wa kikundi cha watu wa mataifa mbali mbali kilichoanzishwa Tanga kwa lengo la kutafakari na kuchambua changamoto za tofauti za tamaduni. Kikundi kinajulikana kama Cross Cultural Dialogue.

Mratibu wa kikundi, Georgina, alikuwa amesoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, wakati niko bado Marekani, akaamua kunialika kuongea nao.

Safari yangu kutoka Marekani nilitua Nairobi, nikapitiliza hadi Mombasa. Kutokea Mombasa, nilishuka Tanga. Nilipumzika siku moja nikisubiri mkutano. Mkutano tulifanyia Hashtag Cafe, na ulifana sana. Wadau walifurahia kunisikiliza, tukabadilishana uzoefu na mitazamo. Nilikuwa nimeleta nakala za vitabu vyangu: Matengo FolktalesAfricans and Americans: Embracing Cultural Differences, na Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Wadau walivinunua.

Kuanzishwa kwa Cross Cultural Dialogue ni jambo muhimu sana. Dunia inavyozidi kuwa kijiji, watu wa tamaduni mbali mbali, tupende tusipende, tunajikuta katika mahusiano ya kila aina ambayo huja na changamoto nyingi, ndogo na kubwa, kwa sababu ya tofauti za tamaduni. Tofauti hizi zinaweza kukwamisha au kuharibu mahusiano, iwe ni ya binafsi, biashara, diplomasia, na kadhalika.

Cross Cultural Dialogue wameendelea kukua. Nafurahi wanavyotumia vitabu vyangu kama dira na kichocheo cha tafakari. Mwamko wa aina ya Cross Cultural Dialogue unaleta matumaini kwa hatima ya Tanzania, katika ulimwengu wa leo wa ushindani mkubwa. Kwa wanaopenda, vitabu vinapatikana kwenye dula la A Novel Idea lililoko Slipway, Msasani, na pia katika TFA Center iliyopo Barabara ya Sokoine, Arusha.

No comments:

Leo mjini Burnsville, Minnesota, nilikutana na wasomaji wangu wawili: Sarah B. Kamsin mwenye asili ya Sudan na Brighid McCarthy kutoka Marek...