Nimemaliza Kusoma "The Pearl," Kitabu cha John Steinbeck

Leo asubuhi, nimemaliza kusoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Kitabu hiki kimeyagubika mawazo yangu siku nzima. Nilipomaliza kukisoma, nilibaki nimeduwaa, wala sikuweza kuandika ujumbe katika blogu yangu, ingawa nilitamani kufanya hivyo. Ni jioni hii, saa moja na kitu, ndipo nimeweza kuanza kuandika ujumbe huu.

Nirudi nyuma kidogo. Wiki kadhaa zilizopita, kitabu hiki nilikitaja katika blogu hii kuwa kimoja kati ya vitabu nilivyokuwa navisoma kwa mpigo. Sikuwa na haraka, bali niliamua mwenyewe muda gani nisome, na katika kusoma, niliamua mwenyewe niishie wapi, siku hadi siku. Mtindo huu naendelea nao kwa vitabu vingine.

Haiwezekani kuelezea nilivyojisikia wakati nasoma The Pearl. Ni kama kumwelezea mtu ambaye hajawahi kuumwa na jino au kula embe, jinsi jino linavyouma, au utamu wa embe. Hata hivi, naona nigusie tu kuhusu kitabu hiki,

Ni hadithi yenye mvuto wa pekee. Inasisimua, inasikitisha, na inatisha pia. Ni hadithi iliyoniteka, kama vile ndoto ya ajabu au jinamizi. Kisa chenyewe kinamhusu Kino, mvuvi anayebahatika kuokota lulu baharini, lulu kubwa, ya thamani isiyoelezeka. Jamii yake yote inapata habari hima, kuanzia walalahoi ambao ni majirani zake, mabepari wachuuzi wa lulu, padri, daktari, omba omba, kila mtu. Habari ya lulu hii inawasisimua wote hao kwa namna tofauti, wengi kwa wivu na tama ya kumwibia maskini mvuvi huyu. Kwa kutumia habari ya hii lulu, Steinbeck amefanikiwa kuanika tabia na hisia za binadamu.

Kino mwenyewe anajawa na ndoto za kuiwezesha familia yake kuondokana na maisha duni na kumpa fursa mtoto wake mdogo ya kusoma. Lakini pole pole, wasi wasi unaanza kumnyemelea Kino, na hofu pia, kuhusu usalama wa lulu yake na hata maisha yake, hasa pale watu wasiofahamika wanapomnyemelea usiku.

Hapo hadithi inaanza kutisha. Steinbeck ni mbunifu wa kiwango cha juu sana. Hadithi inaendelea hadi mwishoni Kino, mkewe, na mtoto wao wanahama mji usiku, kuinusuru lulu na maisha pia. Ajabu juu ya ajabu, baada ya kutembea kwa mwendo wa mbali usiku, na hatimaye kujificha porini, asubuhi Kino anawaona watu watatu wakija pole pole katika barabara ile ile aliyopitia. Ni wapelelezi makini, ambao wanaweza kutambua hata njia aliyopita mnyama kwenye miamba, ambako alama za nyayo hazionekani kwa binadamu wa kawaida.

Hapo nilijikuta nimeelemewa na hofu, ambayo iliongezeka kadiri nilivyoendelea kusoma kisa hiki. Naona nisiendelee, bali niseme tu kuwa hadithi inapoisha, watu kadhaa wamepoteza maisha, akiwemo mtoto wa Kino, na kwa jinsi lulu ilivyoandamana na mikosi, Kino na mkewe wanaenda ufukweni na kuitupilia mbali baharini.

Nina hakika nilikifahamu kitabu hiki tangu nilipokuwa nasoma sekondari, Seminari ya Likonde. Nilipomaliza kukisoma kitabu hiki, wazo moja kubwa lililokuwa akilini mwangu ni kuwa mara nitakapopata wasaa, nisome The Grapes of Wrath, kitabu kingine maarufu cha Steinbeck, ambacho nimetamani kukisoma kwa miaka mingi. Nimemaliza kusoma The Pearl nikiwa na masononeko, nikiwafikiria wa-Tanzania ambao hawajui ki-Ingereza, na mengi ya thamani yanawapitia mbali. Bado nimesononeka.

Comments

Unknown said…
Ahsante kwa kushare nasi LULU.

Neno la mwisho katika post yako limeniumiza sana...labda ipo siku.

Je ni hatua zipi zipitiwe ili kukifasiri?
Mbele said…
Ndugu Yusuf Mcharia, asante kwa ujumbe wako. Nami naumizwa siku zote na hayo niliyoyasema kuhusu jamii ya wa-Tanzania.

Uzembe umeigubika jamii yetu ya Tanzania. Hata pale ambapo vitabu vimetafsiriwa katika ki-Swahili, sioni msisimko wa kuvisoma.

Nitoe mifano ya maandishi muhimu sana ambayo yanapatikana katika ki-Swahili. Kwanza, kuna kitabu cha Frantz Fanon kiitwacho "The Wretched of the Earth." Kitabu hiki ni hazina kubwa, katika kuwawezesha watu waliotawaliwa na wakoloni kujitambua, kutambua matatizo yao, na kusonga mbele. Kilitafsiriwa kwa ki-Swahili miaka mingi kidogo iliyopita, kikachapishwa kwa jina la "Viumbe Waliolaaniwa." Lakini pita mitaani Tanzania, au mashuleni, au maofisini, wizarani, na kadhalika, uangalie ni nani anamfahamu Frantz Fanon, na nani amesoma angalau hiki kitabu kimoja kilichotafsiriwa kwa ki-Kiswahili.

Mfano wa pili ni kitabu cha Rene Dumont, ambacho kilitafsiriwa kwa ki-Kiswahili na Profesa Gabriel Ruhumbika, kikaitwa "Afrika Inakwenda Kombo." Ni kitabu muhimu sana. Lakini zunguka huko na huko Tanzania, kuanzia kwa mawaziri, wanafunzi wa vyuo vikuu, na huko mitaani, uone kama ni wangapi wanakifahamu kitabu hiki. Au angalau pitia magazeti ya Tanzania, uone ni mara ngapi yanaandika kuhusu vitabu kama hivi.

Mfano wa tatu. Maandishi mengi ya Mwalimu Nyerere yanapatikana katika ki-Swahili, kama vile "Ujamaa Vijijini," "Siasa ni Kilimo," "Mwongozo," "Binadamu na Maendeleo." Achilia mbali tafsiri za Mwalimu Nyerere za tamthilia mbili za Shakespeare: "Juliasi Kaizari" na "Mabepari wa Venisi." Shakespeare ni mwandishi aliyetufundisha walimwengu mambo mengi kuhusu masuala ya maisha. Hata mwandishi maarufu wa kwetu, Shaaban Robert, alimsifu sana Shakespeare. Lakini, ni wa-Tanzania wangapi wamesoma au wanasoma haya maandishi ya Mwalimu Nyerere?

Mfano wa nne. Shaaban Robert aliandika riwaya, mashairi, na insha kwa ki-Swahili. Miaka ya karibuni, kimechapishwa kitabu cha barua alizomwandikia mdogo wake Yusuf Ulenge. Maandishi yote hayo yamejaa mambo ya thamani kwa jamii yetu na walimwengu kwa ujumla. Lakini, ni wa-Tanzania wangapi wanayafahamu maandishi hayo, ambayo yamo katika ki-Swahili? Waziri yupi, mkurugenzi yupi, wasomi wepi, wanafunzi wepi, na raia wepi wanavyo vitabu hivi na wanavisoma au wamevisoma?

Nikirudi kwenye hiki kitabu cha "The Pearl" cha Steinbeck, ninahisi kuwa hata kikitafsiriwa, hakitasomwa. Kuna vitabu kadhaa vya waandishi maafuru katika ki-Ingereza ambavyo tayari vimetafsiriwa kwa ki-Swahili, lakini wa-Tanzania hawana habari navyo, sembuse kuvisoma.

Wa-Tanzania wakisikia kuna kitabu kuhusu mapenzi, au kashfa za hao wanaoitwa "mastaa," wanakuwa na hamu ya kukisoma. Lakini kitabu kinachofikirisha kuhusu masuala ya jamii hawatakisoma.

Nimalizie kwa kusema kuwa mimi mwenyewe, ingawa tangu zamani nimekuwa nikiandika makala na vitabu kwa ki-Ingereza, miaka michache iliyopita wa-Tanzania fulani walinihoji kwa nini siandiki kwa ki-Swahili ili wa-Tanzania wenzangu waweze kusoma mawazo na mitazamo yangu.

Niliamua kulifanyia kazi wazo hili, na hatimaye kuchapisha kitabu cha wastani kiitwacho "CHANGAMOTO: Insha za Jamii." Humo nilijitahidi kuibua masuala mbali mbali ya kufikirisha. Lakini je, kitabu hiki kinasomwa? Ninavyofahamu ni kuwa hakina wasomaji. Ila kuna wa-Kenya, fulani, walipokiona kwenye meza yangu katika tamasha hapa Minnesota katika miaka tofauti, walinunua nakala.

Kama walivyo wa-Tanzania wa kule nyumbani, na hao wa ughaibuni (Diaspora) ni vile vile. Hawana mwamko kuhusu usomaji wa vitabu. Kama ninavyosema mara kwa mara katika blogu hii, ninahudhuria matamasha ya vitabu na tamaduni hapa Marekani na ninapita sana katika maduka ya vitabu na sijui ni lini nitamwona m-Tanzania sehemu hizo.

Hapo nimeelezea kifupi tu msingi wa masononeko yangu kuhusu wa-Tanzania. Labda ninasononeka kwa kuwa mimi ni mwalimu.Unknown said…
Hili ni janga ambalo nadhani linaweza tatulika japo kwa mbinde. Uliyosema ni kweli tupu tena kweli yenyewe kama hali ilivyo.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini