Showing posts with label " Seminari Likonde. Show all posts
Showing posts with label " Seminari Likonde. Show all posts

Wednesday, November 30, 2016

Kitabu cha Historia ya Chai

Leo nimenunua kitabu, A Brief History of Tea, cha Roy Moxham, nilichokiona jana katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf. Nilivutiwa na taarifa kwenye jalada la nyuma:

Behind the wholesale image of the world's most popular drink lies a strangely murky and often violent past. When tea began to be imported into the West from China in the seventeenth century, its high price and heavy taxes made it an immediate target for smuggling and dispute at every level, culminating in international incidents like the notorious Boston Tea Party. In China itself the British financed their tea dealings by the ruthless imposition of the opium trade. Intrepid British tea planters soon began flocking to Africa, India and Ceylon, setting up huge plantations. Workers could be bought and sold like slaves.

Maelezo haya yalinisisimua nikaona sherti nikinunue kitabu hiki. Niliona wazi kuwa kitanielimisha kuhusu mengi tusiyoyajua juu ya chai, kinywaji ambacho wengi tunakitumia. Mambo hayo ni pamoja na uchumi, historia, siasa, na mahusiano ya jamii, na mahusiano ya mataifa.  Kitabu hiki kimenikumbusha kitabu cha Sidney Mintz. Sweetness and Power: The Place of Sugar in Modern History, ambacho kinahusu sukari. Iwe ni chai au sukari, ni msingi wa kutafiti na kuelewa masuala mengi. Tafakari ya aina hii inanikumbusha pia Karl Marx, ambaye alitafakari kitu kinachoitwa bidhaa ("commodity"), akathibitisha jinsi bidhaa inavyobeba mambo mbali mbali ya jamii, ikiwemo mahusiano ya binadamu.

Nimeanza kusoma A Brief History of Tea na kujionea jinsi mwandishi alivyo na kipaji cha kujieleza. Ameanzia na maelezo ya maisha yake, alivyokuwa kijana u-Ingereza, akawa amechoshwa na maisha ya kule. Katika kutafuta fursa nje ya nchi yake, aliweka tangazo gazetini, na hatimaye akaajiriwa kuwa afisa katika shamba la chai Nyasaland, ambayo leo ni Malawi. Hapo ndipo yanapoanzia masimulizi ya kusisimua na kuelimisha yaliyomo katika kitabu hiki.

Tuesday, August 12, 2014

Nimemaliza Kusoma "The Pearl," Kitabu cha John Steinbeck

Leo asubuhi, nimemaliza kusoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Kitabu hiki kimeyagubika mawazo yangu siku nzima. Nilipomaliza kukisoma, nilibaki nimeduwaa, wala sikuweza kuandika ujumbe katika blogu yangu, ingawa nilitamani kufanya hivyo. Ni jioni hii, saa moja na kitu, ndipo nimeweza kuanza kuandika ujumbe huu.

Nirudi nyuma kidogo. Wiki kadhaa zilizopita, kitabu hiki nilikitaja katika blogu hii kuwa kimoja kati ya vitabu nilivyokuwa navisoma kwa mpigo. Sikuwa na haraka, bali niliamua mwenyewe muda gani nisome, na katika kusoma, niliamua mwenyewe niishie wapi, siku hadi siku. Mtindo huu naendelea nao kwa vitabu vingine.

Haiwezekani kuelezea nilivyojisikia wakati nasoma The Pearl. Ni kama kumwelezea mtu ambaye hajawahi kuumwa na jino au kula embe, jinsi jino linavyouma, au utamu wa embe. Hata hivi, naona nigusie tu kuhusu kitabu hiki,

Ni hadithi yenye mvuto wa pekee. Inasisimua, inasikitisha, na inatisha pia. Ni hadithi iliyoniteka, kama vile ndoto ya ajabu au jinamizi. Kisa chenyewe kinamhusu Kino, mvuvi anayebahatika kuokota lulu baharini, lulu kubwa, ya thamani isiyoelezeka. Jamii yake yote inapata habari hima, kuanzia walalahoi ambao ni majirani zake, mabepari wachuuzi wa lulu, padri, daktari, omba omba, kila mtu. Habari ya lulu hii inawasisimua wote hao kwa namna tofauti, wengi kwa wivu na tama ya kumwibia maskini mvuvi huyu. Kwa kutumia habari ya hii lulu, Steinbeck amefanikiwa kuanika tabia na hisia za binadamu.

Kino mwenyewe anajawa na ndoto za kuiwezesha familia yake kuondokana na maisha duni na kumpa fursa mtoto wake mdogo ya kusoma. Lakini pole pole, wasi wasi unaanza kumnyemelea Kino, na hofu pia, kuhusu usalama wa lulu yake na hata maisha yake, hasa pale watu wasiofahamika wanapomnyemelea usiku.

Hapo hadithi inaanza kutisha. Steinbeck ni mbunifu wa kiwango cha juu sana. Hadithi inaendelea hadi mwishoni Kino, mkewe, na mtoto wao wanahama mji usiku, kuinusuru lulu na maisha pia. Ajabu juu ya ajabu, baada ya kutembea kwa mwendo wa mbali usiku, na hatimaye kujificha porini, asubuhi Kino anawaona watu watatu wakija pole pole katika barabara ile ile aliyopitia. Ni wapelelezi makini, ambao wanaweza kutambua hata njia aliyopita mnyama kwenye miamba, ambako alama za nyayo hazionekani kwa binadamu wa kawaida.

Hapo nilijikuta nimeelemewa na hofu, ambayo iliongezeka kadiri nilivyoendelea kusoma kisa hiki. Naona nisiendelee, bali niseme tu kuwa hadithi inapoisha, watu kadhaa wamepoteza maisha, akiwemo mtoto wa Kino, na kwa jinsi lulu ilivyoandamana na mikosi, Kino na mkewe wanaenda ufukweni na kuitupilia mbali baharini.

Nina hakika nilikifahamu kitabu hiki tangu nilipokuwa nasoma sekondari, Seminari ya Likonde. Nilipomaliza kukisoma kitabu hiki, wazo moja kubwa lililokuwa akilini mwangu ni kuwa mara nitakapopata wasaa, nisome The Grapes of Wrath, kitabu kingine maarufu cha Steinbeck, ambacho nimetamani kukisoma kwa miaka mingi. Nimemaliza kusoma The Pearl nikiwa na masononeko, nikiwafikiria wa-Tanzania ambao hawajui ki-Ingereza, na mengi ya thamani yanawapitia mbali. Bado nimesononeka.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...