Ukimwuliza mwandishi kwa nini anaandika, anaweza kukuelezea msukumo, sababu, na malengo yake. Nami kuna mambo yanayonisukuma niandike, hasa hamu ya kuwafikishia watu fikra na mitazamo yangu kuhusu masuala mbalimbali. Nina hamu ya kujieleza kwa namna ya kuwagusa wasomaji, na ninapoona nimefanikiwa, ninafurahi. Wasomaji hao wananipa motisha ya kuendelea kuandika.
Hapa kushoto niko na mama Kandie, m-Marekani. Alikuwa mfanyakazi katika Chuo cha St. Olaf nilipoajiriwa mwaka 1991, tukawa tunafurahi na kuongea kila tulipokutana. Ni msomaji wa vitabu vyangu tangu zamani. Baadaye alistaafu kazini. Picha hii tulipiga mjini Faribault, mwaka jana. Tunapokutana tunajiona kama ndugu.
Hapa kushoto niko na wadau wawili. Huyu wa katikati ni bwana Richard, kutoka Sierra Leone. Baada ya kununua na kusoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, alinunua vingine akawapelekea marafiki sehemu mbali mbali hapa Marekani. Hii picha tulipiga katika tamasha la utamaduni Brooklyn Park. Richard alimleta huyu mwenzake, mzaliwa wa Sudan, kumtambulisha kwangu ili naye ajipatie kitabu. Richard mwenyer ameshika kijitabu changu kingine, Africans in the World, ambacho alikinunua siku hiyo.
Pichani hapa kushoto niko na dada Latonya, m-Marekani Mweusi. Tulipiga picha hii katika tamasha la Afrifest mjini Brooklyn Park, baada ya yeye kununua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho anaonekana amekishika. Latonya hataki kukosa ninachoandika, hata mitandaoni. Tunafurahi kila tunapokutana.
Kuhitimisha ujumbe wangu, napenda kusema kwamba habari kama hizi nilizoleta hapa ni za maana sana kwangu. Sio siri kwamba kuna watu wanaoandika vitabu kwa mategemeo ya kupata fedha. Lakini kwa upande wangu, kuwagusa watu kwa maandishi yangu ni tunu isiyo kifani, yenye thamani kuliko fedha. Maisha yangu, sawa na ya binadamu mwingine yeyote, ni mafupi, lakini maandishi yangu yatadumu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment