Sunday, March 27, 2016

Nimechapisha Mwongozo wa "Song of Lawino"

Leo nimechapisha kitabu ambacho ni mwongozo wa Song of Lawino, utungo maarufu wa Okot p'Bitek. Kitabu hiki, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino, ni zao la miaka mingi ya kutafakari utungo huu maarufu katika fasihi ya Afrika.

Nimejitahidi kuandika mwongozo ambao unaichambua Song of Lawino katika mkabala wa fasihi ya Afrika, kwa maana ya mtazamo wa fasihi linganifu, na masuala ya itikadi. Vile vile, nimetumia dhana za nadharia ya fasihi, ambazo zina umuhimu katika kuuelezea utungo wa Song of Lawino.

Uandishi wa miongozo ya kazi za fasihi nilianza zamani. Mwongozo wa kwanza kabisa nilioandika ni juu ya tamthilia ya Arthur Miller, A View From the Bridge, ambao niliuandika kwa ajili ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Tanzania, miaka ya sabini na kitu. Niliwahi pia kuandika mwongozo juu ya The African Child, utungo wa Camara Laye. Mwongozo wangu ambao unajulikana zaidi ni Notes on Achebe's Things Fall Apart, ambao historia yake niliielezea katika blogu hii.

Kwa kadiri ninavyokumbuka, sijawahi kufundisha Song of Lawino. Kazi ya kuandaa mwongozo huu ilikuwa ni ya kujitakia tu, kutokana na kuupenda kwangu utungo huu maarufu. Kadiri nilivyokuwa naendelea kusoma fasihi za ulimwengu na nadharia za fasihi nilivutiwa na wazo la kuuchambua utungo wa Song of Lawino. Nilitaka nitoe mchango kwa wanafunzi na wasomaji katika kuutafakari utungo huu.

Kwa sababu hii, nimeweka pia maswali mwishoni mwa Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Ninategemea masuali haya yatakuwa changamoto ya kufikirisha kwa wasomaji wa Song of Lawino.

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Mbele,
Hongera kwa kufanikisha hili la kuichambua na kuichapisha Song of Lawino. Kila niendapo -pamoja na kuacha tani nyingi za vitabu vyangu -huwa siachi kuandamana na nakala za Song of Lawino na Things Fall Apart. Kwani hivi vitabu viwili ndivyo vilivyonichochea kuwa mwandishi na mshairi kama nilivyo leo. Nikiwa sekondari, pindipo niliposoma Song of Lawino, nilijikuta navutiwa kiasi cha kutamani kuandika kitabu au vitabu ya mashairi huria kama nipendavyo kuyaita. Tokana na msukumo huu, nimeishachapisha vitabu viwili yaani Born with Voice na Souls On Sale. Kitabu kingine cha Psalm of the Oppressed ktatoka hivi karibuni wakati kile cha Perpetual Search kikikaribia kuisha huku Hello John Pombe Magufuli ikiwa imeshachapishwa gazetini.
Kuhusiana na Things Fall Apart -tokana na riwaya hizi kutotumika sana -niko namalizia kitabu ambacho hata hivyo nahagaika na kukipa jina stahiki. Kwa sasa nakiita How the High and the Mighty Eat National Cake japo baadaye naweza kulifupisha au kulibadili. Sijui kama Song of Lawino bado inafundishwa mashuleni. Hata hivyo, ni ushairi mulua tena unaosomeka kirahisi.
Nakupongeza ndugu Mbele kwa mchango huu adhimu na muhimu kwenye ushairi wa kiingereza ulioandikwa kiafrika.
Kazi njema.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Shukrani kwa ujumbe. Ni kweli kuwa "Song of Lawino" ilileta mwamko mpya kote Afrika Mashariki, na sehemu zingine, kuhusu ushairi katika lugha ya ki-Ingereza. Ni utungo uliohamasisha utungaji wa mashairi wa aina mpya. Nilipokuwa nasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, tulifundishwa "Song of Lawino" na mwalimu Grant Kamenju (marehemu sasa), ambaye alituchangamsha akili kwa kutumia fikra za akina Karl Marx, Frantz Fanon, na wengine wa aina hiyo.

Ni muhimu kukumbuka tulikotokea katika safari ya uandishi, na ni ukweli pia "Things Fall Apart" ni utungo mwingine ambao umeathiri na kurutubisha uandishi katika Afrika. Muhimu pia kuweka katika maandishi ushahidi kuwa tulikuwepo hapa duniani, kama walivyofanya waliotutangulia, ambao wanakumbukwa na wataendelea kukumbukwa ingawa hawako hai.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...