Jana jioni nilivyokuwa ninachapisha kitabu changu kipya mtandaoni, nilijipiga picha kwa ajili ya kuiweka kwenye jalada la nyuma la kitabu. Nilikuwa nimetumia masaa yapata manne katika kuweka marekebisho ya ziada ya mswada na pia katika hatua za kwanza za kuuweka mswada mtandaoni.
Picha niliyojipiga inaonyesha dalili za uchovu niliokuwa nao baada ya kufanya kazi ya kufikirisha. Sikujali. Niliamua kuitumia picha hiyo hiyo, nikamalizia shughuli ya kuchapisha kitabu.
Tukijiuliza kwa nini tunaweka picha kwenye jalada la kitabu, tutakumbana na masuala na masuali. Suali pana zaidi ni kwa nini tunajipiga picha. Picha kama hii niliyojipiga jana itakaa kwenye jalada hivyo ilivyo, pamoja na kwamba inaleta taswira yangu ilivyokuwa kwa sekunde ile moja ilipopigwa.
Baada ya sekunde ile moja, uso wangu haukubaki hivyo. Huenda nilitabasamu au kununa. Baada ya muda, sikuwepo humu ofisini, na vitabu nyuma yangu, wala sikuvaa nguo zinazoonekana pichani.
Tunaweza kusema kuwa picha ni udanganyifu. Inatuaminisha kuwa huyu ni fulani, lakini fulani huyu si mtu hai. Hapumui wala haongei. Angalia hata macho. Yatabaki hivi kwa miaka na miaka, bila kuyapepesa. Angalia nywele na ndevu. Baada ya muda, mvi zitakuwa zimetanda. Cha zaidi ni kuwa siku chache zilizopita, kinyozi alizipunguza. Kama tunapenda kuwa wakweli, labda tuwe tunajipiga video muda wote, maisha yote, bila kuacha hata sekunde moja.
Udanganyifu wa picha hauishii hapo. Kwa ujumla, watu wanajiandaa kabla ya kupigwa picha. Wanajiweka katika hali ya unadhifu. Wengi wanaamini ni muhimu kutabasamu wakati wa kupigwa picha, hata kama moyoni kuna machungu.
Masuala na masuali ni mengi, yanayogusa nyanja mbali mbali, kama vile saikolojia, falsafa na sanaa ya upigaji na upigwaji picha. Hata namna tunavyoziangalia na kuzielewa picha ni suala linalofungamana na misingi kama utamaduni na saikolojia. Wataalam wanayatafakari masuala hayo, na wameyaandikia makala na vitabu, kwa mfano Photography Theory in Historical Perspective cha Hilde Van Gelder na Helen Westgeest.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Profesa sijui kama nimeelewa mada yako. Kama una wasi wasi na picha hivyo umeweka ya nini? Naona kama ulichosema na kuweka picha kama kujichanganya kwa kiasi Fulani. Hata hivyo mimi si mtaalamu kama wewe. Nangoja kusikia wataalamu wengine watasemaje.
Ndugu Anonymous,
Nimeweka ujumbe huu ili kuonyesha angalau kidogo sana jinsi suala la picha lilivyo tata. Hata ningebadili picha niweke nyingine, masuala tata na masuali tata yangekuwepo vile vile. Nimeandika ili kuchochea tafakari kwa suala hili la picha ambalo watu tunalichukulia kijuu juu.
Kuhusu kujichanganya au kuchanganyikiwa, ni kwamba mtu ukiamua kulitafakari suala lolote kwa dhati na bila mipaka, hatimaye utaishia kuchanganyikiwa kwani utajikuta unazama zaidi na zaidi katika utata. Watu tunajidanganya kwamba ukitafakari suala, hatima yake ni kuona jawabu na mwanga. Ninaamini kwamba huku ni kujidanganya. Na kwa jinsi tulivyo wavivu wa kufikiri, tunaona masuala ni rahisi, hayahitaji kusumbua akili zetu.
Post a Comment