Tuesday, November 16, 2010

Mzee Kataraia Amekipenda Kitabu Hiki

Blogu yangu hii ni kama kisebule changu binafsi. Naamua nini cha kukiweka hapa, na sidhani kama ninasukumwa na ukweli kwamba watu wanasoma ninayoandika. Yeyote anayepita hapa na kuchungulia, ni hiari yake. Niliwahi kujieleza hivyo katika makala hii hapa.

Basi, leo napenda kuelezea nilivyokutana na Mzee Kataraia juzi, tarehe 14, mjini Minneapolis. Hatukuwa tumefahamiana. Lakini mara tulipotambulishwa, alianza kunielezea jinsi alivyokipenda kitabu changu cha Africans and Americans.

Niliguswa, nikamsikiliza kwa unyenyekevu. Ingawa napenda kuandika makala na vitabu, na watu wengi wananielezea wanavyopendezwa na kufaidika na maandishi yangu, napata taabu kustahimili sifa. Ila huwa namshukuru Mungu kwa kunipa vipaji, niendelee kutekeleza wajibu wa kuwanufaisha viumbe wake. Hii ndio tafsiri yangu. Sifa zote na shukrani namrudishia Muumba.

Nikiwa namsikiliza, Mzee Kataraia aliendelea kunieleza jinsi alivyosafiri sehemu zingine hapa Marekani, akawaonyesha wa-Tanzania kadhaa kitabu hiki, nao wakakisoma. Aliniambia kuwa wiki hizi alizokuwa hapa Marekani, ameshafanya safari kadhaa kwa ndege. Wakati wa kungojea ndege, ameona watu wakisoma kwenye kompyuta zao, na ndege ikiwa hewani amewaona watu wakisoma vitabu. Hapo nami nikamwunga mkono, kuwa nami nimeona sana tabia hizo hapa Marekani.

Maongezi yetu yalikuwa mafupi sana, labda dakika tano tu, kwa sababu tulikuwa katika shughuli nyingine za kusalimiana na kuongea na watu. Lakini kwa dakika zile chache nilipata picha kuwa Mzee Kataraia ni m-Tanzania wa pekee.

Kwanza, kama ninavyoandika katika blogu hii mara kwa mara, si rahisi kumkuta m-Tanzania anayevutiwa na vitabu, labda vitabu vya udaku. Halafu niliguswa na moyo wa Mzee Kataraia wa kuwakumbuka wengine. Alivyoona amekuta kitu cha manufaa, ameenda kuwaonyesha wengine, wanufaike. Nimeguswa.

Sitamsahau Mzee huyu. Nitajiona nina bahati iwapo nitakutana naye tena. Nimegundua huyu ni Mzee aliyeelimika. Kwa mtazamo wangu, kama nilivyosema katika mahojiano Radio Mbao, ishara muhimu ya kuelimika ni kuwa daima na kiu ya kutafuta elimu.

11 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mzee Kataraia namfahamu. Nilikuwa nasoma huko Bukoba wakati ule akiwa Kada makini wa CCM. Sijui kulitokea nini akapotea katika siasa za Tanzania. Ni mchambuzi makini wa mambo na nakumbuka katika hotuba yake moja alituchambulia vizuri sana misukusuko ya Kisiasa kule Urusi ya zamani. Nilivutiwa naye sana.

Watu wa aina hii mara nyingi huwa hawachoki kujielimisha na kusoma vitabu kwao ni sawa na kuvuta hewa.

Ijumaa hii nami nakiagiza kitabu hiki pamoja na kile cha visaasili vya Kimatengo. Sitaki kuvinunua mtandaoni kwani nataka nakala yangu iwe na sahihi ya mwandishi!

Prof. Nitakuandikia pembeni kuhusu suala hili.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Nimefurahi ulivyomtambua huyu mzee, ingawa sikumtambulisha kikamilifu. Yawezekana ni huyu huyu unayemzunguzia.

Kusema kweli, nilishangaa jinsi maongezi yake yalivyokuwa yamelenga kwenye kitabu tu. Kwa sekunde chache hivi alijitokeza jamaa kutusalimia, lakini mara tu baada ya kusalimiana, Mzee Kataraia akaendelea na somo la kitabu, na huyu jamaa akawa amejumlishwa kwenye hili darasa la papo kwa papo.

Kwa wa-Tanzania wanaoogopa vitabu, onyo ni kuwa msiombe kukutana na Mzee Kataraia :-)

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Naamini ni yeye kwa sababu kulikuwa na mjadala uliokuwa unamuhusu kule Jamii Forums. Mtu alikuwa anaulizia alikoishia wakati kuna kipindi alikuwa kada wa kutegemewa kule CCM.
Kama kawaida mjadala haukwenda popote na uliishia katika "uchakachuaji". Kwamba pengine Mzee huyu msomi naye aliishia "kuchakachuliwa" tu na CCM.

Hata hivyo mtu mmoja akasema kwamba kwa sasa alikuwa ameonekana Marekani katika miji ya Houston, Minneapolis na Maryland. Uliposema kuwa kukutana kwenu kulikuwa Minneapolis basi mi nikachukulia kwamba ni yeye na naamini kwamba pengine niko sahihi.

Kama ni yeye basi ni mmojawapo wa watu wanaojua sana kujieleza na kupanga hoja. Na kama nilivyosema hapo juu, watu wa aina hii ni watu wanaojisomea sana!

Mbele said...

Kwa maelezo hayo, nawajibika kusema kuwa umemaliza maneno. Ni wazi kuwa tunayemwongelea ni huyu huyu. Shukrani.

Yasinta Ngonyani said...

Kwa kweli asiyesoma kitabu hiki au vitabu hivi basi achukue nafasi na asome.

Simon Kitururu said...

@Mkuu Matondo : Nanukuu
``Ijumaa hii nami nakiagiza kitabu hiki pamoja na kile cha visaasili vya Kimatengo. Sitaki kuvinunua mtandaoni kwani nataka nakala yangu iwe na sahihi ya mwandishi! ´´ -mwisho wa nukuu.

Umeniua sana tu na KAULI HIYO HAPO JUU nakunifanya nikuonee wivu kwa kuwa VITABU VYANGU havina sahihi ya mwandishi ati!:-(

Itabidi siku moja nimvizie Prof.Mbele anigawie sahihi kwenye vitabu vyake nilivyonavyo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mt. Kitururu hujakosea. Raha ya kitabu uwa na saini ya mtunzi. Si hilo tu ni rahisi kujenga urafiki kati ya msomaji na mwandishi kwa kuwa na mawasiliano ya karibu hivi.
Bado nakudai critique ya kitabu changu.
Kujisomea ni darasa tosha na nyongeza ya kibarua cha kukaa chuoni ukiachia mbali umande kwa waliosomea vijijini.

Simon Kitururu said...

@Mkuu NN Mhango:Critique ya kitabu chako inakuja Mkuu!

Nimeshea kitabu chako na Mbongo mmoja hapa na nilimuambia ntakutungulia hii kitu akadai nisubiri amalizie kukisoma na anadai itakuwa kesho kwa kuwa anataka nithiathiri mitazamo yake katika busara za kitabu chako.

Ikibidi anataka achangie naye
kitu kimtazamo wake katika critique- ....hasaaa ndio maana bado sijakutonya kitu.

Na kwa kifupi KITABU chako kama cha Prof .Mbele kuna wadau wangu kadhaa wanavibuku mpaka nafikiria kuvijaladia kabla havijaaribika ulimbwende!Unajua tena vitabu vikianza safari mikononi mwa wengi tena!:-(


Asante sana kwa mara nyingine kwa kitabu chako na kwa bahati nzuri chako umenipigia sahihi!

Mbele said...

Hiki kitabu cha Ndugu Mhango nami nimekuwa nakisikia humu bloguni, na ninataka kukipata. Nimetafuta huku na huku, maana ndio kazi ya mwenye kujali elimu, ila sijafanikiwa.

Hatua inayobaki ni kumfuata mwandishi. Je, Ndugu Mhango, unaweza kuniletea nakala? Nitafuatilia utaratibu wa kutuma hela. Au kama vipi, labda tunaweza kubadilishana, yaani unaniletea kitabu chako nami nakuletea changu, na mechi inakuwa droo :-)

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele umeniacha hoi. Naona hapa tufanye academic barter system. Nitumie anwani yako nikutumie nakala ya mwisho niliyobakiza. Email yangu ni nkwazigatsha@yahoo.com
Mt. Kitururu nakushukuru sana kwa uvumilivu na moyo wa ku-share whatever knowledge that comes your way. Ubarikiwe sana na uendelee na moyo huo.

Anonymous said...

Mwalimu asante sana kwa kitabu na nimependa sana utafiti wako kuhusu mashujaa wa kijadi. Nami nafanya kazi hizo na mjomba wangu pamoja na wanafunzi kutoka hapa Yale. Ukipata fursa ningependa kusikia fikra na maoni yako kuhusu kazi yetu. Naweka kiungo hapa www.radiomrima.org
Shukran sana,
Mohamed Yunus

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...