Thursday, November 25, 2010

Kuendesha Blogu Mbili

Nina blogu mbili: ya ki-Swahili na ya ki-Ingereza. Kuendesha blogu moja ni kazi, blogu mbili ni zaidi. Kwa nini naendesha blogu mbili?

Nimewahi kuelezea kwa nini ninablogu. Labda nisisitize tu kuwa blogu yangu ya ki-Swahili inanipa fursa ya kujiongezea uzoefu wa kuandika kwa ki-Swahili, na pia kuwasiliana na wa-Tanzania wengi, wakiwemo wale wasiojua ki-Ingereza. Ninafahamu pia kuwa wako wasomaji wa blogu hii ambao si wa-Tanzania. Kuna hata wa-Marekani ambao wameniambia kuwa wanaisoma. Wanajikumbusha mambo ya Tanzania na pia lugha ya ki-Swahili.

Katika blogu yangu ya ki-Ingereza siandiki sana masuala ya Tanzania. Kadiri siku zinavyozidi kwenda, napata hisia kuwa ninaandika kwa ajili ya walimwengu kwa ujumla. Naona jinsi ninavyozingatia masuala ya taaluma, hasa fasihi. Naamini natoa mchango kwa wale wapendao fasihi au wenye duku duku ya kuifahamu. Hapo nawafikiria sana wa-Tanzania.

Katika kuongelea kazi za fasihi, siandiki makala ndefu, bali nagusia vipengele muhimu, na pia natoa dokezo ambazo ni changamoto kwa yeyote, aweze kuzifanyia utafiti na tafakari. Naamini kuwa kwa namna hii, yeyote atajiongezea ufahamu wa fasihi.

Labda nijieleze zaidi kwa wa-Tanzania wenzangu: siandiki kwa ajili ya wale ambao lengo lao kuu ni kupasi mtihani. Naandika kwa ajili ya wale wenye kupenda fasihi au wenye duku duku ya kujifunza fasihi. Pia kama nilivyosema kabla, naandika kwa ki-Ingereza ili kutoa mfano wa uandishi bora wa ki-Ingereza, jambo ambalo linahitajika katika jamii yangu ya wa-Tanzania.

Ingawa kuendesha hizi blogu mbili si kazi rahisi, nitajitahidi kuzimudu kwa kadiri ya uwezo wangu. Kazi ya kuendesha blogu hizi inaniwekea aina ya nidhamu katika maisha yangu. Kuandika katika blogu hizi mara kwa mara imeshakuwa kama deni na wajibu, lakini naona manufaa yake kwangu, kwa jinsi ninavyotumia muda wangu na akili yangu kwenye shughuli ya maana.

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nakubaliana na wewe kwa kweli ni kazi kuendesha blog mbili lakini pia ni mengi sana mtu unajifunza. Na pia kama ulivyosema kufahamiana na watu wengi pia kuendeleza lugha hasa kwa waio ishi TZ. Binafsi nina ya kiswahili na kingoni hakika wala sijilaumu kuwa na hizi blog.

Albert Kissima said...

Profesa, huwa nazifurahia sana makala zako. Zimesheheni mengi ya kujifunza. Naufurahia uandishi wako wa pekee, wenye mpangilio uletao mtiririko mzuri wakati wa kusoma.
Mbali na uyazungumzayo kwenye makala zako, huwa najifunza namna yako hii nzuri ya uandishi yenye mtiririko unaomshawishi mtu kuendelea kusoma. Hongera sana Profesa Mbele.

Mbele said...

Dada Yasinta, shukrani kwa ujumbe wako, nawe ukiwa ni mzoefu wa kuendesha blogu mbili. Wazo lako la kuwa na blogu ya ki-Ngoni, ambayo nimeifahamu tangu mwanzo, ni murua sana.

Nimekuwa daima mshiriki na mhamasishaji wa kurekodi, kutunza, na kutangaza urithi wa historia, lugha na tamaduni zetu. Ni muhimu vile vile kuandika sisi wenyewe habari zetu na za kule tutokako. Kwa hivi nazienzi juhudi zako na napenda uendelee.

Ndugu Albert Paul, nashukuru kusikia kuwa ni mfuatiliaji makini wa makala zangu. Hii tayari ni changamoto ya kunifanya niendelee kuandika, maana vinginevyo naogopa kukuangusha.

Kuna wakati, kutokana na mada ninazoandikia, najiuliza kama blogu yangu hii itadumu kweli au itakwenda na maji, maana inaaminika kuwa udaku ndio wenye wasomaji :-)

Fadhy Mtanga said...

kaka Mbele, ingawa kuendesha blog si jambo jepesi, bado ni jambo la muhimu sana. Nasema ni muhimu kwa kuwa unapowaelimisha wengine nawe wapata nafasi ya kuelimika.
naifurahia sana ile hali ya kuumiza kichwa juu ya nini unataka kublog siku ya leo.
kublog kuna changamoto sana.

Mbele said...

Ndugu Mtanga, umetumia maneno ya kweli kuhusu hali halisi yetu wanablogu, tunavyopambana na hali ya, "kuumiza kichwa juu ya nini unataka kublog siku ya leo."

Maneno hayo yanasaidia kisaikolojia, kutupa nguvu ya kuendelea. Ingekatisha tamaa iwapo bloga ungewasikia mabloga wenzako wakisema kuwa kublogu ni rahisi kama kunywa glasi ya bia.

Hapo kweli mtu ungeweza kuishiwa nguvu kwa kujiona wewe ndio peke yako mwenye akili butu.

Ujumbe wako nauona muhimu kwa maana kwamba unatukumbusha kuwa tuko pamoja na tuendelee kuwa pamoja. Wahenga walisema adhabu ya kaburi aijuaye maiti. Na sisi mabloga tunapaswa kushikamana, kwani ndio tunaojua adhabu ya kublogu. Mfano hai wa mshikamano ni dada yetu Subi, ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa wengi wetu.

Msomaji na Mpiga Debe Wangu Aikwaa Tuzo

Jana niliandika taarifa za msomaji na mpiga debe wangu Joy Zenz, mKenya aishiye uJerumani. Napenda niseme kuwa juhudi zake za kuwaunganisha ...