Wednesday, November 24, 2010

Kitendo cha CHADEMA Kususia Hotuba ya JK

Kitendo cha wabunge wa CHADEMA kususia hotuba ya JK Bungeni kimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wa-Tanzania. Wakati mjadala huu ukiendelea, nami nina la kusema.

CHADEMA imesema kuwa, mapema kabisa, ilipeleka malalamiko kwenye tume ya uchaguzi (NEC) kuhusu mchakato wa utangazaji wa matokeo ya urais, na kuomba utangazaji ule usimamishwe ili kuchunguza dosari ambazo CHADEMA ilikuwa na taarifa nazo.

Kwa msingi huu, ningependa kusikia taarifa ya NEC, niweze kufahamu kama kweli ililetewa malalamiko hayo. Kama iliyapata, napenda kujua iliyashughulikia vipi. CHADEMA inasema kuwa NEC haikuyajibu wala kuyashughulikia malalamiko yale.

Kama hii ni kweli, basi naitupia NEC lawama nzito. CHADEMA imesema kwamba kutokana na kuupuziwa malalamiko yao na NEC, na kutokana na kwamba sheria inasema kuwa tangazo la NEC la mshindi wa urais haliwezi kupingwa mahakamani au penginepo, walilazimika kutafuta hatua zingine za kuelezea malalamiko yao. CHADEMA wanasema kuwa kususia hotuba ya JK ni njia waliyoamua kuchukua kwa msingi huo.

Kama hali ndio hiyo inayoelezwa na CHADEMA, na kama NEC haitatoa maelezo ya kuthibitisha vingine, msimamo wangu ni kuwa CHADEMA walikuwa na haki ya kususia hotuba ya JK kama walivyofanya. Kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, bali ni mpenda haki, uwazi, na ukweli, nawaunga mkono CHADEMA kwa suala hilo.

Nchi lazima iwe na kiongozi muda wote. Kwa msingi huu, JK ni rais, na CHADEMA hawajakataa hilo, ingawa kuna watu ambao, kwa sababu wanazozijua wao, wanaizushia CHADEMA uwongo kuwa haimtambui rais na serikali yake. Najiuliza kama watu hao wana akili timamu au kama wanaitakia mema nchi yetu.

2 comments:

John Mwaipopo said...

nami pia nadhani hoja za chadema katika hili zina mashiko. kuanzia awali wakati wa utangazaji wa majumuisho ya kura za urais walitamka kutomtambua aliyetangazwa mshindi. hawakwenda alikotangazwa wala alikoapishwa. kutoka kwao bungeni kulikuwa muendelezo wa msimamo wao thabiti. vinginevyo wangeonyesha kutokuwa na msimamo.

Mbele said...

Nikiongezea hapo hapo, naona kuwa kishindo hiki walicholeta wabunge wa CHADEMA kitasaidia kuliamsha Taifa usingizini, ili liwe makini katika kuandika katiba mpya.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...