Maongezi na Wanafunzi Wamarekani Waendao Tanzania


Leo nilikwenda kwenye mji wa Apple Valley, Minnesota, kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus kilichoko St. Peter, Minnesota. Mkutano wetu tulifanyia katika ukumbi wa kanisa la Shepherd of the Valley. Maongezi yangu yalikuwa sehemu ya maandalizi ya wanafunzi hao kwa ajili ya safari ya kwenda Tanzania kwa masomo ya mwezi moja. Safari yao inawafikisha Iringa, katika Chuo Kikuu cha Tumaini, na vijiji vya Tungamalenga na Ilula.

Nilikuwa nimeombwa na profesa wao nikaongee nao kuhusu masuala ya tofauti ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mwamerika. Katika kujiandaa kuonana nami, wanafunzi hao walikuwa wameshasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho wanafunzi wa vyuo vingi hapa Marekani wanakitumia pia, katika kujiandaa kwenda Afrika.

Baadhi ya wanafunzi hao wa Gustavus Adolphus wanasomea masuala ya afya. Nilitumia fursa ya leo kuwaeleza jinsi nilivyoingia katika shughuli ya kutafakari masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mmarekani na wa Mwafrika, na jinsi ninavyopenda kuongea na watu mbali mbali kuhusu masuala hayo, wakiwemo wanafunzi, watafiti, wasafiri, na kadhalika.

Mazungumzo yetu yalidumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita kasorobo mchana. Wanafunzi waliuliza masuali mengi kutokana na yale waliyosoma katika kitabu changu, nami nilifanya kila juhudi kujibu na kutoa maelezo.

Chuo cha Gustavus Adolphus kimeshapeleka wanafunzi Tanzania kabla. Mwaka jana wanafunzi wa Chuo hiki pamoja na wale wa Chuo cha St. Olaf, ambapo nafundisha, walifanya safari ya Iringa, kwa masomo. Hao walikuwa wanafunzi wa somo la uuguzi ("Nursing.") Nilialikwa pia kuongea nao, kwenye mji huo huo wa Apple Valley, siku moja kabla ya safari yao ya Tanzania. Maongezi yalihusu masuala yaliyomo katika kitabu hicho hicho.

Nilipoandika kitabu changu, sikutegemea kuwa hata wauguzi wangekiona kinawafaa, kwani mimi sikusomea taaluma hiyo. Isipokuwa, nilipopata mwaliko wa kuongea na wanafunzi wa taaluma hii, nilianza kufahamu kilichokuwa kinawavutia.

Bila kuchelewa, nilichukua jukumu la kujielimisha, nikasoma majarida mbali mbali, na nikafahamu jinsi masuala ya utamaduni yanavyozingatiwa katika taaluma hii ya uuguzi. Juhusi hiyo ilinifanya nikiangalie kitabu changu kwa mtazamo mpya pia, nikaona kuwa nilikuwa nimeongelea masuala ya afya, usalama, vyakula, na mahusiano katika jamii, na mtazamo wa Wamarekani na Waafrika kuhusu masuala hayo yote. Hayo yote ni masuala muhimu kwa waganga na wauguzi.

Nilipokuwa narejea chuoni kwangu leo, nilikuwa na mawazo mengi kichwani. Kwa mfano niliwazia sana ukweli kwamba wanafunzi wanaotoka Tanzania kwenda kusoma Marekani au nchi zingine za nje hawapewi maandalizi ya aina hii. Wanapelekwa tu, wakajue wenyewe kuogelea au kuzama katika utamaduni wa kigeni. Hii ni hatari, na ingekuwa bora kama tungejifunza kutoka kwa hao Wamarekani.

Kwenye picha hapo juu, profesa wa hao wanafunzi ni mama aliyesimama nyuma, wa pili kutoka kulia. Mzee mwenye ndevu aliye pembeni yake, mwishoni kabisa, ni mchungaji.

Kwa taarifa zaidi za mradi huu soma hapa.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini