Monday, July 14, 2014

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo mchana, wakati binti yangu Deta ananirudisha kutoka hospitalini, tulisikia katika redio ya garini mahojiano na Sean Hemingway, mjukuu wa Ernest Hemingway. Mahojiano yalihusu toleo jipya la kitabu cha Ernest Hemingway, The Sun Also Rises. Ilikuwa ni mwanzo kwangu kusikia kuwa Sean amehariri  toleo jipya la kitabu cha The Sun Also Rises.

Sikushangaa kusikia kuwa kampuni ya Scribner ndiyo imechapisha. Nimefahamu tangu zamani kuwa Scribner ni kampuni kongwe ambayo ilichapisha vitabu vya Hemingway tangu zamani.

Niliposikiliza mahojiano hayo, niliamua hapo hapo kwenda kutafuta nakala ya hili toleo jipya. Tulipita kwenye duka la vitabu la chuo cha St. Olaf na nikaambiwa kuwa tayari wanacho kitabu hiki. Niliwaambia waniwekee, ili nije kununua.

Wakati huo huo, niliamua kutafuta nakala ya toleo la mwanzo la The Sun Also Rises. Katika kusoma maandishi ya Hemingway, kwa miaka, nilifahamu kuwa The Sun Also Rises ni kitabu kilichompa Hemingway umaarufu miaka yake ya mwanzo kama mwandishi. Kilichapishwa mwaka 1926, na kiliupa umaarufu mji wa Pamplona ulioko Hispania. Nilikuwa sijakisoma kitabu hiki, na bado sijakisoma, lakini kwa miezi mingi kimekuwa ni kipaumbele katika maazimio yangu ya vitabu vya kuvisoma mapema iwezekanavyo.

Mahojiano niliyoyasikia redioni yalidhihirisha kuwa toleo hili jipya la The Sun Also Rises lina mambo kadhaa ambayo hayakuwemo katika toleo la mwanzo. Jambo hili lilinizidishia hamu ya kupata nakala ya toleo la mwanzo, ili nitakaposoma, niweze kufananisha. Basi, tulipitiliza hadi mji wa Apple Valley, kutafuta hili toleo la mwanzo la kitabu, katika duka la Half Price Books. Kwa bahati mbaya hawakuwa na nakala.

Badala yake, nilinunua vitabu vingine vinne. Kitabu kimojawapo ni Papa Hemingway, kilichoandikwa na A.E. Hotchner. Huyu alikuwa rafiki wa karibu wa Ernest Hemingway. Nilinunua nakala ya kitabu hiki miaka kadhaa iliyopita, lakini leo nimeona toleo lenye picha ya Hemingway kwenye jalada, nikavutiwa. Kwa hivi, ninazo nakala mbili za kitabu hiki.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni Leaf and Bone, kilichohaririwa na Judith Gleason. Ninacho kitabu hiki tangu zamani, "hard cover," na nimekisoma mara kadhaa na kukitumia katika somo la "folklore." Lakini leo nilivyoliona toleo la "paperback" niliamua kununua. Kwa hivi, ninazo nakala mbili za kitabu hiki.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni Shalimar the Clown, riwaya ya Salman Rushdie. Ingawa nina vitabu kadhaa vya Salman Rushdie, hiki sikuwa nacho. Mwaka jana nilifundisha riwaya maarufu ya Salman Rushdie, Midnight's Children. Sio riwaya rahisi kuielewa, ila ina mvuto wa aina yake.

Wakati wa kufundisha kitabu hiki, nilikuwa nashangaa kwa nini watu walikuja juu na kulaani riwaya yake ya Satanic Verses, wakati staili aliyotumia katika Satanic Verses, na pia baadhi ya kejeli ni zile zile katika Midnight's Children. Kwa mujibu wa nadharia ya fasihi, sio sahihi kumshambulia mwandishi kwa yale yanayosemwa na wahusika katika kitabu chake, kama vile haya ndio mawazo au msimamo wa mwandishi mwenyewe.

Ni mbaya pia pale wanaomshambulia ni watu ambao hawajasoma alichoandika. Mtu unaweza kujiuliza: kati ya maelfu walioandamana kulaani kitabu cha Satanic Verses, ni wangapi walikuwa wamekisoma? Ni wangapi wanaojua ki-Ingereza na fasihi kiasi cha kuweza kukielewa kitabu hiki?

Kitabu cha nne nilichonunua leo ni English Fairy Tales, mkusanyiko wa hadithi za jadi za wa-Ingereza. Ninazo baadhi ya hadithi hizo katika vitabu vyangu vingine. Lakini nilipenda kuwa na kitabu hiki, ambacho, kwenye jalada, kimesemwa kuwa ni "Complete and Unabridged," yaani ni mkusanyiko kamilifu, bila marekebisho ya kuzirahisisha hadithi zilizomo. Ningependa kujadili dhana ya "fairy tales" na kuitofautisha na "folk tales," kama wengi tuliomo katika taaluma ya "folklore" tunavyotofautisha. Lakini kwa leo, nitaishia hapa.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...