Saturday, July 19, 2014

Tunajiandaa kwa Tamasha la Afrifest, Agosti 2

Kila mwaka, tangu mwaka 2007, nahudhuria tamasha la Afrifest, ambalo hufanyika hapa Minnesota, Marekani.

Imewahi kutokea kwamba nilikuwa Tanzania wakati wa tamasha hilo. Binti zangu wananiwakilisha.Wanafahamu vizuri shughuli zangu, na wanawaeleza watu wanaoulizia kuhusu shughuli zangu na vitabu vyangu.

Hizo "ti-sheti" tulizovaa zina nembo ya kikampuni changu kiitwacho Africonexion: Cultural Consultants, ambacho najaribu kukijenga.





Hapa kushoto anaonekana Deta, binti yangu wa kwanza. Siku hiyo sikuwepo.













Hapa kushoto anaonekana Zawadi, binti yangu wa mwisho, akiwa anangojea watu. Hapo ni wakati alipokuwa mdogo. Alianza kuipenda shughuli hii tangu alipokuwa mdogo sana. Alikuwa akifuatana nami kwenye matamasha ya utamaduni, akinisikiliza ninapoongea na watu. Tangu akiwa na umri ule mdogo, aliweza kuwaeleza watu kuhusu shughuli zangu na kuhusu vitabu vyangu. Kwa mfano, katika mji wa Faribault kulikuwa na tamasha la tamaduni, nami nikiwa Tanzania. Zawadi alihudhuria mwenyewe. Alihojiwa na gazeti la Faribault Daily News, akatoa maelezo vizuri kabisa.





Shughuli kama Afrifest ni fursa ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia na tamaduni mbali mbali kukutana. Naamini kuwa kwa watu wazima, vijana, na watoto, hii ni elimu bora kabisa.Hapa kushoto Zawadi anaonekana akiwa na watu wawili kutoka visiwa vya Caribbean.



Hapa kushoto wanaonekana Deta na Zawadi wakihojiwa. Kila mwaka, habari za Afrifest zimekuwa zikitangazwa katika vyombo vya habari vya hapa Minnesota. Mahojiano na waandaaji na washiriki huwa sehemu ya taarifa hizo.
Kwa mtoto au kijana, kuhojiwa namna hii ni kujijengea tabia ya kujiamini na pia uwezo wa kujieleza.






Hapa naonekana nikiwa na mama mmoja aliyekuja kwenye meza yangu. Nilimweleza yale aliyoulizia. Hata hivi, kwa kumwangalia usoni, hakuonekana anavutiwa na yale niliyokuwa nasema. Niligundua hatimaye kuwa dhana yangu haikuwa sahihi, kwani, bila mimi kutegemea, alitoa pochi yake, akalipia vitabu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales.Baada ya kuchukua hivyo vitabu, akajiondokea zake, kimya kimya. Nilizidi kuamini kuwa huyu mama sio mzungumzaji sana.


Mwaka huu, Afrifest itafanyika North View High School katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota, tarehe 2 Agosti. Lakini shughuli za mwanzo zitafanyika siku moja kabla, yaani Agosti 1, kama unavyoona katika tangazo hapa chini. Kwa taarifa zaidi, tembelea www.afrifest.org

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Nawatakieni kila la heri na mbarikiwe sana.

Mbele said...

Asante sana kwa kutukumbuka namna hiyo. Tunangojea kwa hamu ujio wa hiyo siku.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...