Showing posts with label Mto wa Mbu. Show all posts
Showing posts with label Mto wa Mbu. Show all posts

Wednesday, July 2, 2014

Mandhari ya Mto wa Mbu na Ziwa Manyara

Mwezi Januari, 2013, katika mizunguko yangu Tanzania na wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf, tukiwa tunafuatilia safari na maandishi ya Ernest Hemingway, niliamua tusimame kwenye mlima juu ya Mto wa Mbu, pembeni ya barabara iendayo Karatu.

Mkisimama hapo, mnauona mji wa Mto wa Mbu kule bondeni, na kwa mbali kule mbele mnaliona ziwa la Manyara.








Hata miaka iliyotangulia, wakati nasafiri na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, tulifika mahali hapa. Mimi kama mwalimu naona ni muhimu kwa wanafunzi kufika sehemu hiyo na kuangalia sehemu hizi ambazo Hemingway alizielezea vizuri katika kitabu chake cha Green Hills of Africa. Inavutia kusoma maelezo ya Hemingway wakati mpo mahali hapa, anavyouelezea mji, mto unaopita hapo, duka la m-Hindu na uzuri wa Ziwa Manyara.

Nina imani kuwa sina haja ya kueleza kuwa anayeonekana hapo kushoto ni mimi.

Tuesday, March 12, 2013

Mabucha, Mto wa Mbu

Nilipiga picha hii hapa kushoto kwenye mtaa mmoja wa Mto wa Mbu. Nilivutiwa na mwonekano huu: safu ya mabucha na pia akina mama wakiwa wamejitokeza tu hapo mlangoni  na kuelekea walikokuwa wanaelekea.

Nilitafakari suala la haya mabucha, ila sikupata fursa ya kuongea na yeyote kuhusu suala hilo. Sikuweza kujua kama wenye mabucha hayo ni akina nani.

Miezi mingi iliyopita, kulikuwa na taarifa za mgogoro Mto wa Mbu baina ya wa-Kristo na wa-Islam. Sikufuatilia undani wa tatizo, isipokuwa haikuwa taarifa njema, kwani migogoro si jambo jema.

Taarifa hii ilinigusa kwa namna ya pekee kwa sababu nilishafika Mto wa Mbu mara kadhaa na nafahamiana na baadhi ya watu wa pale. Mimi kama mgeni nilikuwa na hisia kuwa Mto wa Mbu ni mji uliotulia sana. Sikutegemea mgogoro wa aina ile. Hayo yote yalinijia kichwani wakati napiga picha hii.

Wednesday, July 15, 2009

Mafanikio ya Mradi wa Utalii: Mto wa Mbu

Nimesoma taarifa ya kufurahisha katika Arusha Times kuwa mradi wa utalii Mto wa Mbu, umeteuliwa kuwa mfano wa kuigwa nchini Tanzania. Ni heshima kubwa, nami natoa pongezi kwa vijana wanaoendesha mradi huu.

Nimewafahamu vijana hao kwa miaka kadhaa, tukizungumzia masuala mbali mbali muhimu. Katika kupita kwangu Mto wa Mbu na wanafunzi wa kiMarekani, vijana hao wamekuwa wenyeji wetu wa kutueleza masuala ya tamaduni za mji ule.

Nimeandika habari zao kwenye blogu yangu. Nao katika blogu yao wameandika habari ya ushirikiano wetu.

Ni jambo la kufurahisha kuwaona vijana wakijituma katika shughuli za maendeleo namna hii, na nawatakia mafanikio makubwa zaidi siku za usoni.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...