Showing posts with label Colorado College. Show all posts
Showing posts with label Colorado College. Show all posts

Wednesday, July 2, 2014

Mandhari ya Mto wa Mbu na Ziwa Manyara

Mwezi Januari, 2013, katika mizunguko yangu Tanzania na wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf, tukiwa tunafuatilia safari na maandishi ya Ernest Hemingway, niliamua tusimame kwenye mlima juu ya Mto wa Mbu, pembeni ya barabara iendayo Karatu.

Mkisimama hapo, mnauona mji wa Mto wa Mbu kule bondeni, na kwa mbali kule mbele mnaliona ziwa la Manyara.








Hata miaka iliyotangulia, wakati nasafiri na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, tulifika mahali hapa. Mimi kama mwalimu naona ni muhimu kwa wanafunzi kufika sehemu hiyo na kuangalia sehemu hizi ambazo Hemingway alizielezea vizuri katika kitabu chake cha Green Hills of Africa. Inavutia kusoma maelezo ya Hemingway wakati mpo mahali hapa, anavyouelezea mji, mto unaopita hapo, duka la m-Hindu na uzuri wa Ziwa Manyara.

Nina imani kuwa sina haja ya kueleza kuwa anayeonekana hapo kushoto ni mimi.

Tuesday, July 1, 2014

Ngorongoro

Hapa ilikuwa ni mwezi Januari, 2013. Niko katika bonde la Ngorongoro, mmoja ya vivutio vikubwa vya utalii Tanzania. Nimebahatika kufika sehemu hiyo mara kadhaa. Kila wakati naguswa na uzuri na upekee wa mahali hapo.



Mara ya kwanza kufika hapo nilikuwa kiongozi wa wanafunzi na wazazi wao kutoka shule ya Shady Hill, Boston. Nilikuwa nimeombwa na kampuni ya Thomson Safaris kuongoza msafara huu.







Miaka iliyofuata nimefika hapo na wanafunzi kutoka vyuo vya Marekani vya Colorado na St. Olaf, tukiwa katika kozi ya "Hemingway in East Africa," ambayo niliitunga. Nimeandika makala kadhaa kuhusu kozi hiyo, na makala ya hivi karibuni kabisa ni hii hapa

Kila wakati naguswa na uzuri na upekee wa mahali hapo. Kuna wanyama wa aina aina, kama vile samba, pundamilia, twiga, tembo, vifaru na nyati.

Mara zote, tulitembelea pia hifadhi za Serengeti, Manyara, na Tarangire. Zote hizo ni utajiri mkubwa wa nchi yetu, kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Saturday, June 8, 2013

Nimetoka Mbali na Kozi ya Hemingway

Kila siku, nawazia habari za mwandishi Ernest Hemingway. Kila siku nawawazia pia waandishi wengine, kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Hakuna siku inayopita nisisome angalau kurasa kadhaa za maandishi yao, au uchambuzi wa maandishi hayo. Kwa hilo, naweza kusema Hemingway ndiye anayetawala mawazo yangu kila siku.

Nilifanya utafiti na tafakari ya miaka kama sita hivi, kabla sijaunda kozi ya "Hemingway in East Africa." Kozi hii imeniwezesha kuzifahamu sehemu nyingi za Tanzania kaskazini, na  kufahamiana na watu wengi katika sehemu hizo.

Cha zaidi ni kuwa nimefahamiana na wanafunzi wengi wa ki-Marekani, waliokuja Tanzania kwenye kozi hiyo. Katika picha hapa kushoto, ambayo ilipigwa na Profesa Bill Davis wa chuo cha Colorado, ninaonekana nikitoa mhadhara juu ya Hemingway. Wanafunzi walikuwa kutoka chuo hicho. Huo ulikuwa ni mwaka 2008. Mara ya kwanza kufundisha kozi hiyo ilikuwa ni mwaka 2007, na wanafunzi walitoka chuo hicho hicho. Hapo ni katika viwanja vya chuo cha MSTCDC kilichopo eneo la Usa River, Arusha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...