Nilitafakari suala la haya mabucha, ila sikupata fursa ya kuongea na yeyote kuhusu suala hilo. Sikuweza kujua kama wenye mabucha hayo ni akina nani.
Miezi mingi iliyopita, kulikuwa na taarifa za mgogoro Mto wa Mbu baina ya wa-Kristo na wa-Islam. Sikufuatilia undani wa tatizo, isipokuwa haikuwa taarifa njema, kwani migogoro si jambo jema.
Taarifa hii ilinigusa kwa namna ya pekee kwa sababu nilishafika Mto wa Mbu mara kadhaa na nafahamiana na baadhi ya watu wa pale. Mimi kama mgeni nilikuwa na hisia kuwa Mto wa Mbu ni mji uliotulia sana. Sikutegemea mgogoro wa aina ile. Hayo yote yalinijia kichwani wakati napiga picha hii.