Tuesday, November 17, 2009

Maprofesa Hatuvunji Msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi

Picha hii ilichapishwa tarehe 15 Novemba katika blogu ya Haki Ngowi, pamoja na maelezo haya: Mwalimu, Albert Juakali wa shule ya msingi Iboma iliyopo kijiji cha Udinde Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya akifundisha wanafunzi wa darasa la kwanza chini ya Mti wa Mbuyu kama alivyokutwa na Mpigapicha wetu. Picha na Brandy Nelson
Nina mengi ya kusema kuhusu picha hii. Kwa leo napenda kumwongelea huyu mwalimu, kwa kuirejesha makala yangu iliyotokea katika gazeti la KWANZA JAMII.

Maprofesa hatuvunji msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi


Na Profesa Joseph L. Mbele

TUNAONGELEA sana mfumo wa elimu. Kitu kimoja ninachoona hatukizungumzii ipasavyo ni wadhifa wa mwalimu wa shule ya msingi. Jamii haimwoni mwalimu wa shule ya msingi kama mtu wa pekee sana. Lakini, akitokeza mwalimu wa chuo kikuu, kama mimi, jamii inafungua macho na kutega masikio. Jamii inamwona mwalimu wa chuo kikuu, profesa, kuwa mtu wa pekee sana, kumzidi mwalimu wa shule ya msingi.

Kwa miaka kadhaa sasa, nimejjijengea mtazamo tofauti kuhusu suala hilo. Hii ndio mada ya makala yangu hii. Hoja yangu ni kuwa, mwalimu wa shule ya msingi anastahili heshima ya pekee. Tunaposema shule ya msingi, tuzingatie neno msingi.

Neno msingi tunalitumia sana tunapoongelea ujenzi wa nyumba. Basi, tuchukulie mfumo wa elimu kama nyumba. Tunapowazia kujenga nyumba, tunazingatia sana msingi, kuhakikisha kuwa ni imara. Kila mtu anajua kuwa ukishafanya hivyo, nyumba yako itakuwa imara. Basi, na elimu ni hivyo hivyo. Ili iwe imara, ni lazima tuanzie kwenye msingi. Na hapo ndipo tunamkuta mwalimu wa shule ya msingi. Yeye ni kama yule fundi mjenzi tunayemtegemea kutujengea msingi imara. Hapo tunaanza kuelewa maana halisi ya dhana ya shule ya msingi.

Tunaweza kutoa mfano mwingine. Tukichukulia ualimu kama kazi ya ukulima, basi mwalimu wa shule ya msingi ni sawa na yule mkulima anayevunja msitu. Sisi walimu tunaokuja baadaye kwa mfano chuo kikuu, tunakuta shamba limeshatayarishwa. Kazi yetu ni nyepesi tukiichukulia kwa mtazamo huu wa kumkumbuka aliyevunja msitu. Ni lazima tumwenzi mvunja msitu, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi. Ni msitu gani huo anaovunja?

Mwalimu wa darasa la kwanza ana jukumu la kuleta mapinduzi katika akili ya mtoto. Anamtoa katika fikra na mazoea ya kucheza siku nzima na kuwinda ndege na kumwingiza katika ulimwengu wa ukurasa wa daftari na kitabu. Huu ni ulimwengu mwingine kabisa, na mapinduzi yanayofanyika hapa ni makubwa. Mtoto alikotoka anajua lugha ya kuongea na kusikia. Lakini mwalimu wa darasa la kwanza anambadilisha na kumfanya aifahamu lugha andishi. Maneno ambayo mtoto alizoea kuyasema tu na kuyasikia, sasa anapaswa ayaone na ayaelewe yanakuwaje kimaandishi. Ajifunze kuandika na kusoma, sio kusema tu na kusikia. Ajifunze namna ya kupanga kila herufi, neno, na sentensi kwenye mstari ulionyooka. Afahamu ukurasa unapangwaje: aanzie juu kwenda chini, si vinginevyo. Maneno ayaandike vipi, nukta na mkato aziweke wapi, na alama za kuuliza na kushangaa aziweke wapi. Haya ni mapinduzi makubwa ya akilini.

Katika mapinduzi hayo, mtoto anaanza kukiona kila kitu kwa mtazamo wa maandishi. Akiona kiti, anajua namna ya kuandika neno kiti. Akiona mnyama au mdudu, anajua namna ya kuandika mnyama au mdudu. Akili ya kuielewa lugha kama kitu cha kusema na kusikia tu inapanuliwa. Akili hiyo inakutana na lugha kwa kutumia macho. Hii ni lugha andishi.

Baada ya mwalimu wa shule ya msingi kufanya hayo mapinduzi akilini mwa mtoto, ndipo sisi walimu wa madarasa yanayofuata tunaletewa huyu mtoto. Sisi hatuleti mapinduzi. Hatuvunji msitu, wala kujenga msingi. Tunaingia darasani na kuongea sana, na wanafunzi wanaandika wanachosikia. Tunawaambia waende maktabani wakasome. Lakini hayo yanawezekana tu kwa vile mwalimu wa shule ya msingi alishawafundisha hao wanafunzi kuandika na kusoma. Bila hivyo, sisi tungekwama. Kwa bahati mbaya, tunasahau jambo hilo. Tunamsahau aliyevunja msitu na tunadhani kusoma na kuandika kuliwezekana au kulijitokeza kiurahisi tu.

Huwa najiuliza, je, nikiambiwa nikafundishe darasa la kwanza, nitaweza? Nina hakika nitaumia kichwa. Bahati nzuri, kwa miaka kadhaa nimekuwa nawatafuta walimu wa shule za msingi sehemu mbali mbali za Tanzania na kuongea nao. Wamenifungua macho kuhusu mambo kadhaa, kama vile saikolojia na tabia ya watoto. Wamenielimisha kuwa watoto wana saikolojia tofauti kufuatana na umri: watoto wa darasa la kwanza wana tabia hii na hii, na unapaswa unapowafundisha ufanye hivi au hivi. Ukifanya vile au vile, hutafanikiwa katika kuwafundisha. Mimi sikujua hayo, lakini walimu wa shule ya msingi wamenifundisha.

Walimu hao wameniambia kuwa unapowafundisha watoto wadogo, uangalie unatumia muda gani kwa kitu kimoja, ili ubadili na kufanya kitu kingine. Usijaribu kuwafundisha kitu kimoja kwa muda mrefu. Ukitoa maelezo kwa dakika kadhaa, unabadili; labda uwaimbishe wimbo. Baada ya dakika kadhaa, labda wachukue daftari na kuchora; baadaye wasome, na kadhalika. Usijaribu kutoa mhadhara kwa muda mrefu, kama tunavyofanya chuo kikuu. Elimu hii nimeipata kutoka kwa walimu wa shule za msingi. Kwa maana nyingine, ningekurupuka tu na kwenda kufundisha kule, ningeharibu mambo. Sijui maprofesa wangapi wanajua hayo.

Kitu kimoja tunachohitaji ni kumtambua mwalimu wa shule ya msingi kwa kazi anayofanya na kumpa fursa kamili ya kufanya kazi yake. Katika Tanzania, tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru, tuna jadi ya kuwatwisha walimu majukumu ambayo si ya lazima. Kwa mfano, kwenye sherehe za kitaifa au mapokezi ya viongozi, walimu wametegemewa kuwaandaa watoto wa shule katika gwaride, nyimbo, ngoma, au halaiki. Maofisa kilimo, wahasibu na watumishi wengine ambao wangeweza kabisa kufanya shughuli hizo, hawaguswi. Kwa nini hao wasifanye hizo shughuli za magwaride, ngoma, na halaiki, kama ni shughuli muhimu? Walimu wametumika katika shughuli nyingine pia, kama vile kusimamia kura na hata kuwapikia viongozi. Hizi ni kero zisizo na sababu. Walimu wana kazi nyingi: kuandaa masomo, kufundisha, na kusahihisha daftari za wanafunzi au mitihani..

Baadhi ya matatizo yanayoendelea kuwepo kutokana na walimu wa ngazi mbali mbali kutokuwa na mshikamano. Ingekuwa bora iwapo walimu wa shule za msingi na wale wa sekondari, hadi wa vyuo vikuu, wawe na mshikamano thabiti, na mawasiliano ya daima. Kama nilivyogusia hapo juu, mwalimu wa shule ya msingi ana mengi ya kutufundisha sisi wengine. Anao uwezo wa kutupa mwanga kuhusu njia waliyosafiri wanafunzi tunaowafundisha vyuoni.

Naamini, ingekuwa bora pia kwa walimu wa vyuo vikuu kujaribu kufundisha shule ya msingi. Ingekuwa njia nzuri ya kujielimisha. Ninafahamu kuwa profesa akienda kufundisha shule ya msingi, waTanzania watamshangaa, na huenda wakadhani amechanganyikiwa. Lakini kuna mengi muhimu ambayo profesa anaweza kujifunza kwa kufundisha shule ya msingi, angalau mara moja moja.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...