Saturday, November 7, 2009

Tutajengaje Utamaduni wa Kusoma Vitabu?

Leo asubuhi nilienda kwenye mji wa Brooklyn Park, Minnesota, kuhudhuria kikao cha kamati inayojishughulisha na masuala ya kujenga na kuboresha mahusiano baina ya waAfrika na waMarekani Weusi. Baada ya kikao, wakati narudi kwenye mji ninapoishi, nilipita kwenye mji wa Apple Valley, nikaingia katika duka la vitabu la Half Price Books. Ni duka ambalo nimelitembelea mara nyingi. Half Price Books ni mtandao mkubwa wa maduka ya vitabu hapa Marekani, ambao una maduka katika miji mingi kama inavyoonekana hapa.

Kama kawaida, ninapoingia katika maduka ya vitabu hapa Marekani, nawakuta watu wa kila aina wakizungukazunguka kutafuta vitabu, wakivisoma, na wakivinunua. Kuna maduka mengi ya vitabu hapa Marekani ambamo watu wanaleta vitabu vyao kuviuza, na wengine wanakuja kununua. Unaweza kuja kuuza vitabu vyako na kununua vitabu vingine. Nimewahi kufanya hivyo. Maduka ya Half Price Books yanafuata mtindo huo. Kwa hivi, daima utawaona watu wakija na mifuko au makasha ya vitabu vya kuuza, wakati huo huo unawaona watu wakinunua vitabu.

Leo, kama ilivyo kila ninavyoingia katika maduka haya, niliona jinsi Wamarekani wanavyojali utamaduni wa kusoma vitabu. Niliwaona wazee, watu wazima, wake kwa waume, vijana, na watoto. Niliwaona wazazi wakiwa na wamekuja na watoto wao. Niliwasikia wakiongea na watoto kuhusu vitabu, wakiwasomea watoto vitabu, wakijibu masuali ya watoto, na kadhalika.

Nilijisikia vibaya kukumbuka hali ilivyo nchini mwetu Tanzania. Leo ni Jumamosi. Je, ni mzazi gani Mtanzania ambaye siku kama ya leo anaenda kwenye duka la vitabu? Ni mzazi gani ambaye anampeleka mtoto wake kwenye duka la vitabu?

Sasa, kama watoto wa wenzetu wanalelewa hivyo, je, tunaweza kutegemea kuwa Taifa letu litaweza kushindana na hao wenzetu katika ulimwengu huu wa leo na wa kesho ambao unategemea elimu na maarifa? Ni lini na vipi waTanzania tutajenga utamaduni wa kusoma vitabu? Hatima ya Taifa letu itakuwaje?

2 comments:

John Mwaipopo said...

Profesa hili ni swali gumu kwa sisi watanzania. awali ya yote kuna sehemu ya sisi watanzania tunaoamini kuwa vitabu ni chanzo cha maarifa. halina ubishi hilo. Lakini utamaduni ama uchumi wetu umefanya vitabu viwe lulu. mie nadhani kitabu kinafaa kimrudishie nguvu kiasi fulani mtunzi/mwandishi na pengine msambazaji. kweli havitakiwi viwe bureee. lakini tofauti na hivyo huku tanzania vitabu vimefanywa biashara 'haramu'. vimefanywa bidhaa inayoogopwa na mnunuzi. watanzania wa kawaida wanaoweza kununua vitabu vya maarifa ni wachache sana kulingana na bei iliyopo madukani. kwa mfano, kule mlimani city hakuna kitabu cha barrack obama kinachouzwa chini ya elfu 40. amazon wanaviuza kwa dola 7 (viwili) na dola 15. sidhani kwa tanzania vinafaa kuuzwa dola 40.

hapo hapo mlimani city kamusi ya tuki inayouzwa elfu 10 mlimani inauzwa elfu 23. nadhani ni tofauti kubwa sana.

vitabu ni lulu lakini sidhani vinafaa viwe lulu isiyofikiwa. kwe mwendo huu kidogo kidogo hamasa ya mtu kutamani kusoma inapotea. mathalani nikiwa sekondari nilikuwa 'kichaa' wa african writers series hata vile visivyotakiwa katika mtaala. pia nilipenda novel za kizungu. pengine kukosa kazi maalumu kulifanya nipende kusoma fictions hata mie kutamani kuwa mwandishi wake siku moja (sijafanikiwa hata sasa). niliweza kusoma kurasa 200 kwa siku moja na nusu tu. Niliwahi kusoma kitabu cha Edison Yongai kiitwacho "Who Killed Mohta" kurasa zaidi ya 80 kwa masaa matano tu kwani kitabu kilikuwa 'on transit'. Leo sijasoma fictions nima miaka miwili. sidhani kama niko bize sana. nachukua fursa hii pia kuomba radhi maktaba nilizoziibia vitabu enzi hizo.

nadhani kuna haja ya kutengeneza sheria ya uchapaji tanzania na ya uingizaji vitabu itakayofanya upatikanaji wake uwe wa bei poa. Pia kuwa na mpango madhubuti wa kuhamasisha usomaji vitabu, hasa vya maarifa. vitabu vinaogopwa kutokana na bei yake, watu kuwa bize na kusaka noti (hata kwa kuiba) na vitabu kutotoa majibu ya haraka. mtu yuko radhi akamuulize jirani yake jinsi ya kufuga samaki kuliko kusoma yeye mwenyewe.

Mbele said...

Ndugu Mwaipopo, shukrani kwa changamoto yako ya kufikirisha na kuburudisha akili.

Napenda nichangie kidogo tu. Nami nilipita hapa Mlimani City mwanzoni mwa mwezi Septemba, nikaona bei za vitabu unazoongela. Sikuthubutu hata kuvigusa.

Au labda wanafuata utaratibu wa maduka ya kitalii? Kuna kitabu changu kimoja nilikiona kinauzwa kwenye hoteli ya kitalii kule Karatu kwa bei mbaya, wakati kinapatikana hapa Sinza kwa bei nafuu.

Hata hivi, maendeleo ya tekinolojia yanatupa matumaini mapya. Tatizo la bei za vitabu litapungua sana kutokana na kuenea kwa tekinolojia inayotoa vitabu bila karatasi.

Vitabu hivi vinasomwa kwenye skrini za kompyuta au vifaa maalumu vya kuhifadhia na kusomea vitabu. Vifaa hivi vinaitwa "e-readers" au "e-book readers."

Unanunua kifaa hiki na ukiona kitabu mtandaoni kinachokuvutia, unakilipia na kukiingiza kwenye kifaa chako. Unaweza ukawa na mamia ya vitabu kwenye hiki kifaa chako.

Mimi mwenyewe kama mwandishi, kwa kuzingatia maendeleo hayo, nimeamua kwenda na wakati. Wiki iliyopita, nimejikakamua na kuvichapisha vitabu vyangu kama "e-books," kama unavyoona kwenye kurasa za hizi blogu zangu.

Kwa maana hiyo, Mnyakyusa wa Tukuyu akiwa na "e-reader," anaweza kuvipata kitabu vyangu papo kwa papo, badala kungojea kifurushi kisafiri kwa wiki mbili hadi kije posta.

Maendeleo haya ya tekinolojia yatawavuruga wachapishaji wetu na wenye maduka ya vitabu tunaowaongelea. Watalazimika kujibadili ili waende na wakati au watasambaratika.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...