Kuhusu Kunyanyaswa kwa Jaji Warioba

Kati ya mambo yaliyonishtua sana mwaka huu ni kunyanyaswa kwa Jaji Warioba. Kadhia hii imetokana na kazi murua aliyofanya Jaji Warioba na tume yake ya kukusanya mawazo ya wananchi kuhusu Katiba Mpya.

Kumekuwa na mlolongo wa matukio kadhaa ya unyanyasaji huo, ambao, kwa kadiri ninavyofahamu, mwanzilishi wake ni Ikulu. Tukio la kupigwa Jaji Warioba mkutanoni, ambalo limeripotiwa sana, ni kilele cha utovu huu. Wengi tunaamini kuwa Jaji Warioba ananyanyaswa kwa sababu ya uwazi na uwakilishi wa mawazo ya wananchi, jambo ambalo ni mwiba kwa mafisadi.

Nimeshtushwa vile vile na kauli ya Rais Kikwete kuhusu tukio hili la vurugu na kupigwa Jaji Warioba. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, Rais Kikwete aliishia tu kusema kuwa anaomba yasimkute yaliyomkuta Jaji Warioba. Sikuona popote kama aliongelea suala hili kwa undani na mapana kama linavyostahili.

Yeye kama Rais, nilitegemea kwanza atambue kuwa vurugu zile ni aibu kwa nchi anayoiongoza. Nilitegemea awakemee walioleta vurugu zile zilizohusisha pia kunyanyaswa kwa Jaji Warioba.

Nilitegemea Rais Kikwete atumie fursa ile kuwakumbusha wa-Tanzania, wajibu wao wa kuheshimiana na kulumbana kwa hoja, sio kwa mabavu. Angefanya hivyo, nigesema Rais ameonyesha busara za kiuongozi. Nilitegemea angekemea utovu wa ustaarabu uliojitokeza. Angewakumbusha wa-Tanzania njia ya usataarabu. badala ya yeye kujiwazia yeye binafsi, kwamba anaomba yasimpate. Je, kauli yake hii si sawa na kumezea uovu? Kauli yake haikuonyesha busara za kiuongozi.

Halafu, kuna pia kauli ya Samuel Sitta, ambayo nayo imenikera. Sitta aliripotiwa akisema kuwa Jaji Warioba alijitakia yaliyomkuta. Niliposoma taarifa hii, sikuamini kama mzee Sitta, anayetegemewa ana busara, angeweza kuwa na msimamo kama huo.

Nasikia Sitta ni msomi. Nami najiuliza: ni msomi gani ambaye hatambui wala kutetea mijadala au malumbano ya hoja. Kusema kuwa Jaji Warioba alijitakia yaliyompata ni sawa na kumezea suala la mjadala kuingiliwa na vurugu ambazo hazikubaliki katika mijadala. Kauli ya Sitta ni kama inahalalisha ukosefu wa ustaarabu unaotegemewa hasa kwa wasomi.

Sijui Sitta alikulia wapi na katika maadili gani. Sisi wengine tulilelewa katika maadili ya kuwaheshimu wazee. Kitendo cha kumpiga mzee, kwa mujibu wa maadili yale, ni mwiko kabisa. Kama hukubaliani na mzee, unapaswa kutafuta namna ya kujieleza, ambayo ni ya heshima kabisa. Nilitegemea Sitta atambue na kuzingatia hilo. Atoe mfano kwa watoto na vijana.

Tena na tena, katika jamii yetu, tumezoea kukemea tabia tunazoziiita haziendani na maadili au utamaduni wetu. Nimeshangaa kuona kuwa Sitta, ambaye ni mzee, anayetegemewa kuwa mlinzi na mtetezi wa maadili bora, haonekani kutambua kuwa Jaji Warioba kama mzee, hawezi kuletewa vurugu kama alizoletewa. Nimekerwa kabisa na kauli ya Sitta na kauli ya Rais..Comments

Unknown said…
Asante Prof kwa kusimimia ukweli na kutukumbusha pia sisi watanzania jinsi ya kuheshimu wazee. ninatamani wayaone na kuyasoma haya maandiko yako.
Mbele said…
Shukrani, Ndugu Malifa Michael. Niliona pia ujumbe wako kule Facebook. Tanzania ni yetu wa-Tanzania; sio ya kikundi fulani, au ya serikali. Kila la heri.
Anonymous said…
Mimi sishangai hata kidogo yaliyotokea. Haya ni matokeo ya kuendeleza ujinga. Jamii za mwanzo uyunani ilijifunza kupitia mihadhara, hiyo ni miaka zaidi ya 2000 iliyopita. Japokuwa hatuna ushahidi wa kuwa au kutokuwa na vurugu lakini bado tuna lakujifunza. Sisi miaka 2000 baadae hatuwezi.
Ndio maana ujinga unazidi kutamalaki, mawazo ya kijinga na uongo yanaenea kwa kasi sana nchini kwetu. Muandishi mmja anasema kuna ujinga wa halaiki umeshika hatamu. Ukiwa mjinga huwezi kuwa na fikra sahihi.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini