Friday, September 5, 2014

Leo Nimeanza Tena Kufundisha

Baada ya kuumwa kwa miezi mingi, na kuwa katika likizo ya matibabu, leo nimeanza tena kufundisha. Hali yangu inaendelea kuimarika, na ingawa naendelea na matibabu kidogo kidogo, madaktari wameridhia ombi langu kuwa nirudi darasani. Wameniwekea sharti kuwa nisibebe mzigo mkubwa wa kozi za kufundisha, na nisihusishwe na shughuli nyingine ambazo walimu huzifanya, kama vile ushiriki katika kamati mbali mbali na mikutano. Hiyo picha hapa kushoto nimejipiga mwenyewe leo, baada ya kutoka darasani.

Hali itakuwa hiyo kwa muhula mzima, ambao umeanza leo, na utamalizika katikati ya mwezi Desemba. Ninafundisha kozi mbili, ya kwanza ni "South Asian Literature," na ya pili ni "Writing." Katika hiyo kozi ya kwanza, ambayo niliitunga miaka michache iliyopita, nafundisha riwaya kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Riwaya hizo ni, Untouchable, iliyoandikwa na Mulk Raj Anand (India); Twilight in Delhi, iliyoandikwa na Ahmed Ali (India); The Crow Eaters, iliyoandikwa na Bapsi Sidhwa (Pakistan); Shalimar the Clown, iliyoandikwa na Salman Rushdie (India); na Reef, iliyoandikwa na Romesh Gunesekera (Sri Lanka).

Ninapangia kufundisha pia mashairi kutoka katika nchi hizo. Kwa wakati huu, katika kujiandaa, ninasoma kitabu cha mashairi ya Michael Ondaatje kiitwacho The Cinnamon Peeler. Michael Ondaatje alizaliwa Sri Lanka, ila anaishi Canada. Ninafanya pia uchunguzi wa vitabu vya mashairi ambayo nitaweza kuyatumia. Kila ninapofundisha kozi hii, nabadilisha, kwa kiasi fulani, vitabu au waandishi.

Fasihi ya hiyo sehemu ya dunia imejengeka katika historia, siasa, dini, tamaduni, na harakati za watu wa kule tangu miaka elfu tano au zaidi iliyopita hadi kwenye kipindi cha ukoloni, na baada ya kupata uhuru. Waandishi wengi wa India na Pakistan, kwa mfano, wanaelezea janga kubwa lililotokea kabla tu ya kupata uhuru na wakati nchi ilipogawanyika na kuwa nchi hizi mbili, mwaka 1947.

Katika kozi ya "Writing," ninafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza. Kadiri miaka ilivyokwenda, nami kujijengea uzoefu zaidi na zaidi wa kufundisha kozi hii, nimekuwa nikitafuta mbinu mpya za kufundisha. Leo nimewaambia wanafunzi kuwa, tofauti na miaka yote iliyopita, na tofauti na wanavyofanya waalimu wengine, muhula huu tutatumia vitabu viwili tu. Kitabu kimoja ni The Trickster, kilichoandikwa na Paul Radin, na kingine ni The Elements of Style, kilichoandikwa na William Strunk Jr. na E.B. White.

Lengo langu katika hii kozi ya uandishi ni kuwafundisha kwanza kabisa namna ya kuandika sentensi bora kabisa ya ki-Ingereza, kama alivyoelekeza mwandishi maarufu Ernest Hemingway, na baada ya hapo tutaendelea hadi kuweza kuandika insha bora kabisa. Nimewaeleza wanafunzi kwamba uandishi bora ni jambo la lazima kwa mafanikio maishani mwao, nikatoa mifano mbali mbali ya namna watakavyohitaji uwezo wa kuandika ipasavyo. Wameona uzito wa hoja na mifano niliyotoa.

Nimefurahi kuwa nimefikia hali ya kuweza kuingia tena darasani, nikizingatia hali yangu kiafya ilivyokuwa mbaya kabla sijalazwa hospitalini. Kwa mara nyingine tena, namshukuru Mungu, na nawashukuru madaktari na wauguzi, familia yangu, marafiki, na wote wanaonitakia mema. Mungu awabariki wote.

3 comments:

NN Mhango said...

Hongera kaka kurejea ulingoni. Naamini kufundisha kutakupa nafuu zaidi hasa ikizingatiwa kuwa utauamsha ubongo na kuupa changamoto. Nakutakia sifa na kazi njema. Mie kwa sasa niko naandaa mswada wa Kitabu changu cha Souls on Sale ambacho inshallah kitachapishwa na Kampuni ya Langaa ya Kameruni. Pia nimepata ofa toka Poland ya kukitafsiri kwenye kijerumani. Ni kitabu cha mashairi pia.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe wako, Ndugu Mhango. Nimefurahi kusikia kuwa unaandaa mswada mwingine. Vile vile, napenda nichukue fursa hii kukufahamisha kuwa kwa wiki kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika ujumbe kwenye blogu yangu, kuhusu ujumbe ulioandika kwenye blogu yangu, ukielezea vitabu ambavyo umevisoma hivi karibuni. Nilikuwa nimewauliza wadau kama wamesoma vitabu vingapi kwa muda ambao nilifafanua, nawe ulielezea vitabu ulivyosoma.

Ujumbe wako ule ulinigusa vilivyo, na niliona ni sherti niandike Makala kwenye blogu yangu, Makala juu yako, ukiwa ni mfano wa kuigwa. Nitafanya hivyo, siku za karibuni.

NN Mhango said...

Kaka Mbele nami nimefurahia kuona sasa unaendelea vizuri kiasi cha kuweza mikikimikiki ya kufundisha.Bila kusoma inakuwa vigumu kuandika na bila kuandika inakuwa vigumu kusoma. Binadamu ana muda wa kutosha kujisomea na kujiendeleza. Juzi nilisoma maisha ya watu maarufu kama Bill Gate wanavyohakikisha angalau kila siku wanatumia saa moja kujisomea.
Nilisahau kuandika kuwa pamoja na kuandaa mswada mwingine nilisaidia kuhariri mashairi ya Nuosu toka China yanayotarajiwa kuchapishwa na Da Philo Ikonya mwandishi kutoka Kenya anayeishi Austria ambaye ametokea kuwa rafiki wa karibu sana. Na ni huyu dada anayeshughulikia miswada yangu miwili yaani Nyuma ya Pazia ambayo ilishapitishwa kuchapishwa Tanzania lakini wachapishaji wakaogopa mafisadi na Souls on Sale (SOS). Kutokana na mashairi yangu ya Souls on Sale da Philo ameweza kuandika mengine ya Save our Souls (SOS). Huyu ndiye aliyeniunganisha na Langaa na tuko mbioni kuanzisha African Literaria Society (ALS) ili kusaidiwa waandishi ambao hawajabahatika kuchapisha. Kwa sasa niko nasoma vitabu vingine vya kiada kama Getting to Yes without giving in.
Kaka nisikuchoshe, nangoja kusoma hiyo makala, Inshallah huenda nami nikaijibu kama itahitaji kufanya hivyo.