
Tamasha huanzia siku moja kabla, jioni, kwa burudani ya muziki, maonesho ya mavazi na kadhalika. Hivyo ndivyo ilivyokuwa tarehe 1 Agosti. Siku inayofuata, tamasha hufanyika nje uwanjani. Kunakuwepo na mabanda ya wafanya biashara, pia watoa huduma mbali mbali. Kunakuwepo muziki, michezo ya watoto, na mechi ya soka. Ndivyo ilivyokuwa mwaka huu kule Brooklyn Park.
Mwaka huu, wa-Kenya walijitokeza kwa wingi kuliko wa-Afrika wa nchi nyingine yoyote. Palikuwa na meza ambapo paliwekwa bidhaa na vitu mbali mbali kutoka Kenya. Bendera ya Kenya ilipepea siku nzima. Ilifurahisha kuona wenzetu walivyoonyesha umakini katika kuitangaza nchi yao.
Mimi na binti zangu tunakumbuka, kwa mfano, jinsi kijana mmoja alivyofika hapo mezani, akaongea nasi kwa ki-Swahili. Alionekana kijana wa kawaida tu, nasi tulidhani ni mmoja wa wale wanaotaka kuelewa shughuli zangu, kuhusu vitabu vyangu, na kisha wanaenda kwenye meza au mabanda mengine. Bila sisi kutegemea, alinunua vitabu vitatu kabla ya kuondoka.
No comments:
Post a Comment