Sunday, September 21, 2014

Jibu Langu kwa "Anonymous" Aliyenikosoa Leo

Hapa naleta maoni ya "anonymous," aliyoyatoa leo kwenye taarifa niliyoleta jana kuhusu dhuluma za polisi dhidi ya waandishi wa habari.  Taarifa niliyoweka hii jana ni hii hapa. Baada ya maoni ya "anonymous", nami nimejaribu kuweka jibu langu chini yake, ikashindikana. Kwa hivi, nimeweka hapa maoni yale ya "anonymous" na jibu langu. Mdau karibu ujisomee: ----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------- Anonymous said...

Naona na wewe umejiunga katika kundi la wanaharakati ambao wanajiita waandishi. kwa taarifa yako huyo Isango anafanya kibarua (sio ajira rasmi) gazeti la Tanzania Daima na huyo Badi pia anapeleka picha (si muajiriwa rasmi kwa muda mrefu tu, sababu hazijulikani) na wote walikuwa wanakaidi amri halali ya polisi. Nani kasema uhuru wa habari hauna mipaka? Mbona nyie huko Snowden na wikileaks hamuwaachii wafanye watakalo? Babu usijivunjie heshima yako ndogo uliyonayo
Anonymous said...
Tanzania Daima, kukuongezea tu, ni la Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema. Hata mwangosi hakuwahi kuwa mwandishi wa habari (hakuwa na taaluma kama walivyo badi na Isango) bali ni mwanaharakati kama ambavyo wewe unataka kuelekea

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Anonymous, kwanza nikushukuru kwa kufika hapa kwenye blogu yangu, kusoma taarifa, na kuweka maoni.

Taarifa niliyoleta sikuiandika mimi, wala picha sio zangu. Mwishoni mwa taarifa ile, nimetaja chanzo: "Maisha Times." Mjumbe hauawi.

Taarifa za polisi kuwapiga waandishi ziliripotiwa katika magazeti na blogu mbali mbali, na pia katika televisheni,na kila mahali ilisemwa kuwa polisi waliwapiga waandishi. Umejaribu kuelezea kuwa Isango na Badi si waandishi, kwa msingi kuwa si waajiriwa rasmi.

Kigezo cha kuwa mwandishi sio kuajiriwa au kuajiriwa rasmi. Wako pia wanaofanya uandishi bila kuajiriwa. Mimi mwenyewe ni mfano hai, kwani nimeandika katika magazeti ya Tanzania na ya Marekani, bila kuajiriwa nayo.

Katika mazingira haya, jina "waandishi," linawajumlisha  hata wapiga picha na wanablogu kama walikuwepo.

Hoja yako ya kuwaweka kando akina Isango na Badi, eti kwa vile hawajaariwa rasmi na eti kwa vile Badi anapeleka picha haina uzito.

Hao waandishi waliopigwa na polisi walivunjiwa haki zao za kibinadamu, ambazo zimeelezwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu (ki-Ingereza tangazo hili hujulikana kama "The Universal Declaration of Human Rights"). Soma kifungu hiki:

Article 19.
•Everyone has the right to freedom of opinion and expression; this right includes freedom to hold opinions without interference and to seek, receive and impart information and ideas through any media and regardless of frontiers.

Kwa wale ambao hawajui ki-Ingereza, kifungu hiki kinatamka kuwa kila binadamu anayo haki ya kujieleza na kutoa mawazo yake, na haki hii inajumlisha pia haki ya kuwa na mawazo au mtazamo bila kuzuiwa, na anayo haki ya kutafuta, kupata, na kusambaza taarifa, mawazo na mitazamo kwa kutumia vyombo vyovyote bila mipaka. Hapa nimetumia neno vyombo nikimaanisha magazeti, televisheni, blogu, redio na kadhalika.

Tangazo halisemi mtu awe ana ajira rasmi kama mwandishi ndipo aweze kutafuta na kusambaza habari. Isango na Badi wanayo hiyo haki, sawa na wewe na mimi.

Kuhusu mipaka ya uhuru wa habari, binafsi, sipendi kuwawekea watu mipaka. Naheshimu uhuru wa kila mtu kujiwekea mipaka yeye mwenyewe. Hata kwenye hizi blogu zangu, yaani hii ya "hapa kwetu" na ile ya ki-Ingereza, naweka maoni yoyote ambayo watu wanaleta. Sijawahi kuzimisha maoni ya mchangiaji yeyote. Ninachozingatia ni kuwa mtu amejaribu kujenga hoja, na pia kuwa watu hupishana kwa akili na ufahamu.

Ndio maana hata mawazo yako nimeyaweka hapa, ingawa sikubaliani nayo. Kuna wengine wamewahi hata kujenga hoja za kunikebehi au kunitukana, lakini sikuwazimisha, ingawa uwezo wa kufanya hivyo ninao. Ningekuwa siheshimu haki hiyo, ningeweza hata kuweka blogu zangu katika mfumo ambao hauruhusu maoni. Ziko blogu za namna hiyo, lakini kwangu milango iko wazi.

Iwapo mtu anaona mwandishi amevuka mpaka, tunazo njia za kistaarabu za kushughulikia suala hilo. Kwa mfano tunazo mahakama.

Kama polisi waliona waandishi wa habari wamevunja sheria, au wamekaidi hicho unachokiita "amri halali," wangewakamata na kuwafikisha mahakamani. Picha zinaonyesha kabisa kuwa hao akina Isango walishakamatwa na polisi, na haingekuwa vigumu kuwapeleka mahakamani.

Lakini polisi waliamua kutumia njia isiyo ya ustaarabu, yaani kuwapiga. Huu si ustaarabu. Polisi wanavunja haki za binadamu, wanajifedhehesha, na wanaifedhehesha nchi.

Unasema, katika sentensi yako ya kwanza kuwa mimi nimejiunga na kundi la wanaharakati wanaojiita wandishi. Mimi siwajui hao unaowaita wanaharakati. Sijajiunga, na sihitaji kujiunga nao.
Nina historia yangu; nimeelimishwa na kujielimisha hadi nikafikia mtazamo nilio nao sasa, na kadiri ninavyoendelea kujielimisha, ninaweza nikafikia kuwa na mawazo tofauti. Ni uhuru wangu na haki yangu.

Sikuanza leo kutetea haki za waandishi. Kwa mfano, mwaka ule kitabu cha Dr. Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai kilipopigwa marufuku na serikali ya Tanzania, nilipinga sana kitendo cha serikali, hasa huko mtandaoni. Na nilikuwa nafanya hivyo nikijitambulisha kwa jina langu kamili, wala sikuandika kama "anonymous." Nilitetea haki ya Hamza Njozi ya kutoa mawazo na fikra zake.

Tafuta kitabu alichoandika Njozi baada ya hicho cha Mwembechai, utaona kuwa katika "Utangulizi" amenishukuru kwa kutetea haki yake.

Msimamo wangu ulikuwa kwamba kama serikali haikuafiki aliyoandika Njozi, basi iandike kitabu chake, na kama polisi hawakuafiki, nao waandike kitabu chao, na yeyote mwingine mwenye msimamo tofauti anaandike kitabu chake. Katika hali hii ya mawazo na fikra mbali kukutanishwa au kugonganishwa, ukweli utajitokeza.

Siafiki dhana yako ya kuwapa polisi wadhifa wa kutuwekea mipaka ya uhuru wetu wa kutafuta habari na kuzisambaza. Hali hii itakuwa ni janga kubwa.
Kuhusu Mbowe kumilikia gazeti la "Tanzania Daima," ni jambo la kumshukuru, kwani anatoa fursa ya watu kupata na kupashana habari, mitazamo, na taarifa, kama linavyoelekeza tangazo la kimataifa nililonukuu hapa juu. Ungekuwa mtu mwenye ufahamu, ungetambua hilo.

Kuhusu Snowden, mimi sina mamlaka yoyote kuhusu mambo ya aina hii hapa Marekani. Kwa vile sio raia wa nchi hii, na sijawahi hata kuwazia kuwa raia, sipigi kura. Mpiga kura angalau ana uwezo fulani, ingawa ni mdogo sana, wa kuathiri mwelekeo wa nchi yake.

Binafsi, namshukuru Snowden na WikiLeaks, kwa kufichua uovu katika siasa na uongozi wa nchi. Wenye visa na Snowden na WikiLeaks ni wale wanaotawala nchi, na ndio wenye mamlaka, sio mimi.

Nimalizie na usemi wako kwamba nisijivunjie heshima. Kati yako na mimi, ni nani anayejivunjia heshima? Wewe unayewapa polisi wadhifa wa kutuamulia mipaka ya uhuru wetu, au mimi ninayezingatia tangazo la kimataifa la haki za binadamu?

3 comments:

Anonymous said...

Mzee Mbele sijui kwanini unapoteza muda kumjibu mtu kama huyu, hajielewi. Anadhani watu maalumu ndio wanahitaji haki zao kulindwa. Sasa hapa inaonesha ni wazi kuwa waandishi waliopingwa ni kuwa mashambulizi yao yalipangwa.
Nchi hii inaujinga wa hali ya juu, hata uelewe wa watu ni mdogo sana.

Mbele said...

Ndugu Anonymous uliyeleta ujumbe Septemba 21, saa kumi na dakika 53, shukrani kwa ujumbe wako na nasaha zako.

Napenda kukuhakikishia kuwa nami najiuliza mara mbili tatu kwa nini nijibu ujumbe kama ule wa anonymous wa mapema leo. Bado sijaweza kuwa na msimamo, bali nawazia tu labda kwa kujibu, inatokea fursa ya kuelimishana. Sijui.

Ila nakushukuru kwa kuhoji kwa nini nafanya hivyo. Unanipa fursa ya kufikiri zaidi.

Anonymous said...

Kwa kumjibu Anonymous umeonyesha kiasi gani ni muungwana. Kuficha majina ni uwoga na kukosa uhakika kuhusu maoni aliyotoa. Kama alivyoeleza mtoa maoni mwingine, Watanzania bado tupo gizani kwa kiasi kikubwa hasa katika kuheshimu uhuru wa mtu. Si ajabu kusikia mtaani mtu anazomewa kwa kuvaa mavazi ya aina Fulani eti tunasema tunalinda maadili. Ni shiidaa professor.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...