Tuesday, September 2, 2014

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania Kuhusu Katiba Mpya

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Katiba Mpya

JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA


Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:

Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.

Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote
yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI.

Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI.

Tunaamini kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.

Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili:

Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahi ya nani?

Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya WANANCHI.

Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE.

Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;

1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.

2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.

3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.

4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.

5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.

6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.

Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.

Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.

“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)

IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE.

Imetolewa leo Agosti 28, 2014
Na MKUTANO WA JUKWAA LA WAKRISTO
Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT)
Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)

CHANZO: Wavuti

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...