Showing posts with label Mankato. Show all posts
Showing posts with label Mankato. Show all posts

Sunday, June 28, 2015

Tamasha la Vitabu Mankato Limefana

Leo, nikiwa na binti yangu Zawadi, tulikwenda Mankato kushiriki tamasha la vitabu, Deep Valley Book Festival. Niliandika habari za tamasha hilo katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Nilipeleka vitabu vyangu vinavyoonekana mtandaoni, pamoja kijitabu kiitwacho Africans in the World. Vile vile tulipeleka "t-shirt" kama hizo tulizovaa pichani, zenye nembo ya kampuni yangu ndogo Africonexion: Cultural Consultants. Tunajifunza mengi katika kukutana na watu wanaofika kwenye meza yetu. Hatujui nini kitamvutia mtu fulani na kwa nini. Lakini watu hujieleza. Tunasikia habari nyingi, nyingine za kushangaza, zinazomfanya mtu anunue hiki au kile.

Inatufurahisha kuwaangalia watu wakipita kwenye meza mbali mbali kuangalia vitabu, kuongea na waandishi, wachapishaji na wengine wanaokutana nao katika tamasha. Nasi tunapata fursa ya kukutana na watu mbali mbali. Leo, kwa mfano, wamefika watu kwenye meza yetu ambao wametuambia wamefika Afrika: Botswana, Tanzania, na Namibia. Tunahisi walivutiwa na "t-shirt" tulizovaa, zenye ya ramani ya Afrika. Kila mmoja ametusimulia habari za safari yake. Tulijua kuwa tutakutana na baadhi ya watu tuliokutana nao wakati nilipotoa mihadhara katika Chuo cha South Central, katika maandalizi ya safari ya Afrika Kusini. Kama tulivyotarajia, walikuwepo watu kadhaa.



Hapa kushoto anaonekana kiongozi wa safari ya Afrika Kusini, mwalimu Becky Fjelland Davis, ambaye ni mwandishi. Alishiriki tamasha. Mwingine ni Paul Dobratz ambaye alihudhuria shughuli zote nilizofanya wakati wa ziara yangu Chuoni South Central. Naye alikuwemo katika safari ya Afrika Kusini. Binti yangu nami tulifurahi sana kusikia habari za safari.




Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, watu wa rika mbali mbali huhudhuria matamasha haya ya vitabu. Wanayathamini sana, na mahudhurio huwa makubwa.

Daima ninaguswa ninapowaona wazazi wakiwa na watoto wao. Ninaguswa na jinsi wanavyowalea watoto wao katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.






Imekuwa siku ya furaha sana kwa binti yangu na mimi. Tumefurahi kukutana na kuongea na watu wa aina aina, tuliowafahamu na ambao hatukuwafahamu. Tumerudi na kumbukumbu nyingi.

Monday, February 23, 2015

Mihadhara ya Mankato ni Kesho

Siku zinakwenda kasi. Naona kama ndoto, kwamba safari yangu ya kwenda Chuo cha South Central, mjini Mankato, kutoa mihadhara ni kesho asubuhi.

Ninangojea kwa hamu kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yangu, ambayo ni kwanza kuongea na wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya Afrika Kusini kimasomo, na pili ni kutoa mhadhara kwa jumuia ya chuo ambao mada yake itakuwa "Writing About Americans."

Maongezi yote hayo yatahusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake ulimwenguni. Wanafunzi wanaokwenda Afrika Kusini wanajiandaa kuishi na kushughulika na wa-Afrika, katika utamaduni ambao ni tofauti na ule wa Marekani. Utaratibu huu wa maandalizi, ambao umeshakuwa jambo la kawaida hapa Marekani, ingekuwa bora ufuatwe na wengine, kama nilivyowahi kuwaasa wa-Tanzania wenzangu.

Katika maandalizi hayo, hao wanafunzi wanasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kitabu ambacho, japo kidogo, kinawagusa watu, tangu nilipokichapisha, tarehe 5 Februari, 2005. Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kukiandika kama nilivyoandika, hadi kimekuwa msingi wa mialiko ya kwenda kuongelea yaliyomo na yatokanayo.

Katika mhadhara wa "Writing About Americans," ninapangia kuelezea mchakato wa kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kuanzia chimbuko la wazo la kukiandika, mchakato wa kukiandika, mambo muhimu niliyojifunza katika kuandika huku, hadi jinsi kitabu kilivyopokelewa na jamii, hasa wa-Marekani, ambao ndio wanaoongoza katika usomaji wake.

Jambo moja kubwa nililojifunza katika kutafakari na kuandika ni kuheshimu tamaduni, pamoja na tofauti zake. Shaaban Robert angeishi miaka mingi zaidi ya ile aliyoishi, angetufundisha mengi kuhusu suala hilo.

Panapo majaliwa, nikikamilisha ziara ya kesho, nitaandika taarifa katika hii blogu yangu.

Wednesday, January 28, 2015

Katika Blogu, Sijui Ninamwandikia Nani Zaidi Yangu Mwenyewe

Je, mwandishi wa blogu anamwandikia nani? Kwa mtazamo wangu, hili ni suali gumu. Naliona gumu kulitafakari, achilia mbali kulijibu.

Baada ya kuona ugumu wa suali hili, nimeamua kukiri kuwa ninajiandikia mwenyewe. Ndio maana makala ninazoandika aghalabu zinanihusu mimi mwenyewe, shughuli zangu, matatizo na mafanikio yangu, mategemeo yangu na kumbukumbu zangu.

Sipendi sana kuwaongelea watu wengine, wala sipendi sana kuongelea mambo kinadharia, bila kujihusisha mwenyewe. Naweza kusema kuwa ndivyo nilivyoandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Sijajificha nyuma ya pazia la nadharia au taaluma. Nimejiweka wazi kwa namna nilivyoweza.

Mwandishi Ernest Hemingway aliongelea suala hili vizuri alipofafanua dhana ya ukweli katika uandishi. Nilivyomwelewa, anasema kuwa ukweli katika uandishi ni kwa mwandishi kuifungua na kuiweka bayana nafsi yake.

Ningependa sana niweze kuandika namna hii aliyoongelea Hemingway. Ni ndoto inayovutia, sawa na nyota inayong'aa mbali, ambayo mtu unaifuata kwa hamu ingawa haifikiki. Lakini, naona huku ndiko kujiandikia mwenyewe.

Kusema kuwa kuna hadhira ninayoiandikia katika blogu yangu ni kama kuota ndoto. Ni kujidanganya. Nasema hivi sio tu kutokana na tafakari yangu mwenyewe, bali ninakumbuka makala ya kufikirisha ya Walter J. Ong, "The Writer's Audience is Always a Fiction."

(Picha hapo juu nilijipiga mwenyewe jana, kwa ajili ya matangazo ya mihadhara yangu Mankato)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...