Monday, October 12, 2015

Kama Mwandishi, Ninawaenzi wa-Kenya

Mimi kama mwandishi, ninawaenzi wa-Kenya. Naandika kutokana na uzoefu wangu. Tena na tena, mwaka hadi mwaka, nimeshuhudia wa-Kenya wakifuatilia vitabu vyangu. Wamekuwa bega kwa bega nami kama wasomaji wangu.

Tangu nilipochapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, wa-Kenya walikichangamkia. Ndugu Tom Gitaa, mmiliki wa gazeti la Mshale aliandaa mkutano kuniwezesha kukitambulisha kitabu hicho, kama ilivyoelezwa katika taarifa hii.

Kati ya watu waliohudhuria alikuwepo Julia Opoti, m-Kenya mwingine, ambaye alishajipambanua kama mpiga debe wa kitabu hiki. Siku hiyo alimleta rafiki yake m-Kenya, Dorothy Rombo, naye akapata kunifahamu na kukifahamu kitabu changu.

Julia hakuishia hapo. Siku moja ulifanyika mkutano mkubwa wa wa-Kenya hapa Minnesota, ambao uliwakutanisha wana-diaspora wa Kenya na viongozi mbali mbali waliofika kutoka Kenya ili kuongelea fursa zilizopo nchini kwao katika uwekezaji na maendeleo kwa ujumla, na namna wana-diaspora wanavyoweza kushirikiana na wenzao walioko nyumbani.

Nilihudhuria mkutano ule sambamba na wengine waliokuwa wanaonesha bidhaa na huduma zao. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Julia alimleta ofisa wa ubalozi wa Kenya, Washington DC kwenye meza yangu, akatutambulisha. Alimwelezea kuhusu kitabu changu cha Africans Americans: Embracing Cultural Differences, naye akanunua nakala. Baada ya siku kadhaa aliniandikia ujumbe kama nilivyoandika katika blogu hii. Maneno ya afisa huyu yalinigusa, na baadhi ni haya:

Kuhusu kitabu chako, hivi sasa nafikiri kimesomwa na watu kadri ya watano hapa ubalozi wetu na kimependwa sana. Ni matumaini yangu kuwa ukipata wasaa mzuri utaandika vitabu zaidi katika fani hii ili upate kunufaisha watu juu ya swali hili muhimu la tafauti ya mila na utamaduni

Siku nyingine nilikuwa natoa mhadhara katika Chuo cha Principia. Aliyeanzisha mchakato wa kunialika ni m-Kenya ambaye alikuwa amesoma taarifa zangu mtandaoni. Mama mmoja m-Kenya aliyehudhuria aliamua kuniunganisha na jamii ya wa-Kenya wa Kansas City, ambako alikuwa anaishi, ili niweze kwenda kutoa mhadhara. Mipango ilikamilika nikaenda, kama nilivyoelezea hapa.

Mara kwa mara, nimeona jinsi wa-Kenya wanavyojitokeza katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki. Katika Afrifest, kwa mfano, hawakosekani. Nimewahi kuelezea jambo hilo, miaka michache iliyopita na mwaka jana.

Nimeona niandike taarifa hii kwa kuwa naguswa na tabia za majirani zetu hao wa-Kenya. Walinifanyia ukarimu mkubwa nilipokuwa nafanya utafiti nchini mwao baina ya mwaka 1989 na 1991, hata kunialika kutoa mihadhara kuhusu utafiti wangu. Naendelea kuguswa na moyo wao huku ughaibuni. Nimejithibitishia kuwa wanaheshimu taaluma, nami nawaheshimu kwa hilo. Nategemea kuandika zaidi kuhusu suala hilo hapa katika blogu yangu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...