Wizard of the Crow: Riwaya ya Ngugi wa Thiong'o

Siku hizi, katika darasa langu mojawapo, tunasoma Wizard of the Crow, riwaya ya Ngugi wa Thiong'o. Kama kawaida yake miaka hii, Ngugi huandika riwaya zake kwanza katika lugha ya Kikuyu. Ndivyo alivyofanya kwa riwaya hii, kisha akaitafsiri kama Wizard of the Crow.

Hatujamaliza kuisoma, bali tunakaribia katikati. Ni moja kati ya riwaya ndefu kabisa zilizowahi kuandikwa na wa-Afrika. Kwa kigezo hiki, riwaya hii inanikumbusha ile riwaya maarufu ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali iliyoandikwa na Aniceti Kitereza.

Katika riwaya hii, Ngugi si yule Ngugi ambaye tumezoea kumsoma kwa miaka yapata thelathini sasa, ambaye vitabu vyake katika kipindi hiki, tofauti kiasi fulani na miaka ya mwanzo, vimebeba hisia za kupambana na uonevu, unyonyaji, na ukoloni mamboleo bila mzaha. Kwa miaka mingi, Ngugi ameonekana kama mwandishi mwenye hasira, na wasomaji na wahakiki wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hasira hizi zimedhoofisha sanaa katika uandishi wake.

Lakini Wizard of the Crow inavutia kwa kigezo cha sanaa. Ngugi amejidhihirisha kuwa msimuliaji wa hadithi mwenye uwezo wa kutumia kejeli na mizaha. Kwa upande wa dhamira, anaelezea hali halisi ya utawala na siasa inayoonekana sehemu nyingi za Afrika ya leo, ambamo wale tunaowaita viongozi ni mafisadi waliobobea katika majungu na ushirikina na uvunjaji wa haki za binadamu. Ingawa hali anayoelezea si ya kufurahisha, Ngugi anafanikiwa kuwaanika hao watu kwa mbinu mbali mbali za kisanii, kama nilivyogusia. Mtu unaposoma Wizard of the Crow, huwezi kujizuia kuwakumbuka madikteta kama vile Mobutu, Bokasa na Banda.

Ngugi wa Thiong'o amejipambanua kama mwandishi bora tangu zamani. Baadhi yetu tunaamini kuwa riwaya yake ya A Grain of Wheat ndio ilitia fora katika kazi zake zote, na wengine wanaihusisha pia Petals of Blood. Lakini naamini wasomaji na wahakiki sasa watakubali kuwa Wizard of the Crow ni bora kuliko zote ambazo Ngugi amewahi kuandika.

Comments

Kwa mbali kinaonekana ni kitabu kizuri sana binafsi sijawahi kukisoma..nawatakieni usomaji mwema..
Mbele said…
Ni kweli kitabu hiki ni kati ya vitabu vinavyovutia kuvisoma. Nawasikitikia watu ambao hawasomi vitabu, kwani wanakosa mengi.
Ila naona waTanzania wengu utamaduni huu wa kusoma vitabu umepotea kabisa. inasikitisha sana.

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania