Thursday, October 13, 2011

Ni Msimu Mwingine kwa Wanafiki Kumkumbuka Nyerere Kinafiki!

Tafakuri Jadidi

Chanzo Raia Mwema

Ni msimu mwingine kwa wanafiki kumkumbuka Nyerere kinafiki!
Johnson Mbwambo
12 Oct 2011


KESHOKUTWA, Ijumaa, Oktoba 14, Taifa litatimiza miaka 12 kamili tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kilichotokea kule London, Uingereza katika hospitali ya Mtakatifu Thomas.

Kama ambavyo imekuwa kwa miaka 11 iliyopita, Watanzania wataitumia pia keshokutwa kumkumbuka mpendwa wao huyo; huku wakitafakari, kama Taifa,
zile “t” tatu maarufu : Tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.

Na kama ilivyokuwa kwa miaka 11 iliyopita, Taifa litaiadhimisha siku hiyo ya Ijumaa, Oktoba 14, kwa makongamano, semina na matamasha yenye mahusiano na maisha ya Baba wa Taifa.

Kama ilivyokuwa kwa miaka 11 iliyopita, maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya Nyerere yatapambwa na kauli nzito kuhusu mchango wake katika kujenga Taifa letu, mawazo yake na visheni yake.

Wengi wataonyesha kwa dhati hisia zao za mapenzi waliyokuwanayo kwa mtu huyo ambaye, kwa jinsi alivyoipenda Tanzania, mimi naamini itatuchukua miaka 50 mingine kumpata anayemkaribia japo kwa asilimia 60 tu!

Lakini watakuwepo pia viongozi wachache wanafiki ambao watasimama majukwaani na, kwa unafiki, kuisifu visheni na uongozi wa Nyerere; huku kiutendaji wakiendelea kuibomoa misingi yote ya taifa ambayo mzee wetu huyo alitujengea.

Ndugu zangu, ni kipindi kama hiki ambapo tutawasikia hata wale waliokuwa wafuasi wake wakubwa katika kuitekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea katika Tanzania, lakini baadaye wakaitelekeza siasa hiyo, wakitoa kauli za kumsifu Mwalimu Nyerere kwa yale yote aliyoyasimamia. Ni Oktoba 14 ya kila mwaka wanapodhihirisha unafiki wao huo.

Ngoja tuwakumbushe unafiki wao viongozi hao wanafiki ambao zamani walikuwa wafuasi wa Nyerere, lakini sasa ni wafuasi wa Ubeberu wa Magharibi unaozidi kuwakamua wakulima na wafanyakazi masikini wa nchi hii.

Tuanze na Siasa ya Kujitegemea: Nyerere aliwaambia hivi kuhusu hilo, na wakajitia wako naye: “Tutaijenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe. Akipatikana mtu wa kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine.”

Natujiulize; Baada ya kifo cha Mwalimu, Oktoba 14, 1999, wafuasi wake hao ambao bado wapo madarakani ndivyo wanavyoiendesha nchi? Je; wanaamini na kutekeleza dhana hiyo ya kujitegemea?

Jibu langu ni “hapana”. Angalau bado tunamkumbuka mtawala wa sasa (Rais Kikwete), kwenye kampeni za mwaka jana, alipoomba apewe kura kwa sababu yeye ni hodari wa “kuhemea vibaba Ughaibuni”.

Mtawala mwenye mtazamo huo hawezi kamwe kuwa muumini wa kweli wa Siasa ya Kujitegemea ambayo Mwalimu Nyerere alipigania kuijenga nchini wakati wote wa uhai wake.

Kwa hiyo, si siri kwamba watawala wetu wa sasa si waumini wa kweli wa dhana ya kujitegemea, na ndiyo maana safari zao kwenda Ughaibuni kutembeza bakuli la ombaomba zimekuwa nyingi tangu Mwalimu afariki. Majuzi tu hapa Kikwete karejea kutoka Marekani (kuhemea!?) na aliporejea, Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda naye akapanda ndege kwenda Brazil (kuhemea?!).

Vyovyote vile; kama wafuasi hawa wa zamani wa Mwalimu Nyerere watazungumza lolote la kumkumbuka hiyo Ijumaa, Oktoba 14, na kusema kuwa wanafuata nyayo zake katika suala hilo la kujitegemea, watakuwa wanadhalilisha uwezo wetu wa kufikiri, na kwa hakika, watakuwa wanauanika tu hadharani unafiki wao!

Kuhusu ujenzi wa Ujamaa na kuupiga vita Ubepari; wafuasi hao wa Mwalimu wanaonyesha unafiki huo huo. Si siri kwamba Ujamaa aliouhubiri Nyerere sasa umebaki kwenye Katiba tu; huku wakubwa wakiimba na kucheza ngoma ya Ubepari.

Haikuwachukua hata miaka saba tangu Nyerere aondoke madarakani kwa wafuasi wake hao kuliua Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwa kuweka Azimio la Zanzibar mwaka 1992. Na bado Ijumaa, Oktoba 14, kina Ngombale Mwiru watakuwa na ujasiri wa kupanda jukwaani na kutoa kauli za kulisifu Azimio la Arusha alilolipigania Nyerere; ilhali ndio hao hao walioliua kwa azimio lile la Zanzibar!

Wafuasi hao wameliua Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na wakaamua kuukumbatia Ubepari, lakini sote tunajua jinsi Mwalimu alivyouchukia Ubepari (kiasi cha kuuita ni unyama). Alipata kusema hivi: “Ni majitu (mabepari) yanayokaa na uwezo wao na yanatumia wengine kama vyombo vya uzalishaji. Kwa hiyo, kwao mfanyakazi na randa ni sawa sawa. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ni nchi ya kibepari.”

Katika suala la fursa sawa kwa wote, pia matendo yao hayaendani na ya Mwalimu. Enzi za Mwalimu, kila mwananchi alikuwa na fursa sawa, na haikujalisha utajiri au umasikini wake, kabila lake, elimu yake, dini yake au rangi yake.

Lakini tangu Mwalimu aondoke, mambo yamebadilika kwa kasi. Hivi sasa kuzungumzia fursa sawa kwa mtoto wa kiongozi (tajiri) na mtoto wa masikini, kunahitaji ujasiri wa ‘ki-uendawazimu’.

Hali imebadilika mno. Mfano mzuri ni katika elimu. Wakati watoto wa wakulima masikini wanakalia ndoo shuleni kwa sababu ya ukosefu wa madawati, watoto wa viongozi ama wanasoma nje ya nchi au katika shule za binafsi zenye kila kitu.

Hata katika suala la ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini pia wameitelekeza visheni ya Mwalimu. Mwalimu alisema hivi kuhusu viwanda: “Maana ya maendeleo ya leo ya uchumi wenye nguvu, ni maendeleo ya viwanda. Nchi yenye viwanda tunasema ni nchi iliyoendelea. Nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na viwanda vya kisasa.”

Ili kulitekeleza hilo kwa vitendo, Mwalimu alisimamia ujenzi wa viwanda vingi nchini. Kwa mfano, mpaka wakati anaondoka madarakani, nchi ilikuwa na viwanda vya nguo 12.

Lakini alipong’atuka madarakani, hao waliokuwa wafuasi wake wakaanza mbio za kuuza viwanda hivyo vya umma kwa watu binafsi; tena kwa bei ya kutupa. Ilikuwa ni katika kutekeleza sera yao mpya ya uchumi wa soko huria.

Matokeo yake ni kwamba hivi sasa ni kama vile sekta ya viwanda haipo kabisa katika Tanzania! Kutoka kwenye viwanda 12 vya nguo (kwa mfano) sasa nchi ina viwanda vitatu tu vya nguo! Leo hii, hata leso tu za kujifutia jasho zinatoka Beijing kwenye viwanda vya Wachina!

Pamoja na usaliti huo, bado watawala wetu watakuwa na ujasiri, hiyo Oktoba 14, kupanda jukwaani na kutudanganya kuwa wanaifuata sera ya Mwalimu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda! Unafiki mtupu!

Hata katika suala la kudumisha amani na usalama ambao ndio umekuwa wimbo wao mkubwa siku hizi wa kuwatisha wapinzani, ni hivyo hivyo. Watasimama majukwaani na kutuongopea kwamba wanaijenga misingi iliyowekwa na Mwalimu ya kudumisha amani na usalama nchini!

Uongo mtupu; maana sote tunakumbuka kwamba Mwalimu alisema kuwa “usione vinaelea, vimeundwa”; kwamba amani tuliyonayo inatokana na misingi ya usawa iliyojengwa, na kwamba hatuwezi kubaki nayo kama tutaachia pengo kati walio nacho na wasio nacho liongezeke.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, pengo hilo limekuwa kubwa mno. Wakati wanavijiji wengi nchini wanaishi katika nyumba za mbavu za mbwa, viongozi mijini wanamiliki majumba kadhaa ya kifahari.

Wakati masikini wanakula mlo mmoja kwa siku, matajiri wanakula na kusaza, na wakati Watanzania wengi wanashindwa kumudu kununua hata baiskeli moja tu, viongozi na matajiri wanamiliki misururu ya magari ya kifahari nk.

Mwalimu alipata kututahadharisha kuhusu hali hiyo kwa kusema hivi: “Wachache wanapoonekana waziwazi wakiogelea katika utajiri wa wizi na magendo na unyonyaji, wakati wengi wanakabiliana na dhiki ya kweli kweli, si rahisi kulinda amani na umoja wetu.

Je; watawala wetu wa sasa wanazingatia tahadhari hiyo ya Mwalimu kwamba tusiruhusu pengo kati ya matajiri na masikini liongezeke? Jibu unalo mwenyewe mpenzi msomaji.

Tukija kwenye suala la ardhi na maliasili zetu nyingine ni hivyo hivyo. Mwalimu alitambua na kuthamini haki ya wananchi kumiliki ardhi, lakini baada ya kifo chake sote tumeshuhudia ekari kwa ekari za ardhi za wananchi wakipewa wawekezaji. Hali hii imeibua misuguano mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji hao huko Loliondo, Babati, Manyara na Mbarali.

Katika sekta ya madini, stori ni hizo hizo. Mwalimu hakuwa na pupa kubinafisha migodi yetu kwa wageni. Alitaka Watanzania wajiandae vyema kabla ya kuchimba migodi hiyo ili iweze kuwaletea maendeleo. Lakini alipokufa, sote tuliiona kasi ya kina Mkapa kuibinafsisha migodi hiyo kwa wawekezaji wa kigeni! Na sasa, muda si mrefu watatuachia mashimo matupu!

Ndugu zangu, ninaweza hata kuandika vitabu vitatu kueleza mambo mengi mema ambayo Mwalimu alituwekea misingi na kutuonyesha njia; lakini wale waliokuwa wafuasi wake wakaamua kuyatelekeza na kutuchagulia njia potevu baada ya kifo chake; lakini itoshe tu kusema kwamba laana yake itawashukia.

Nina hakika kama muujiza ungetendeka na Mwaliimu akafufuka leo, na kuyaona hayo yanayofanywa na waliokuwa wafuasi wake, angewakana mara moja kwa kusema: “Hakika, siwajua watu hawa waovu”.

Nihitimishe safu yangu kwa kukumbusha tena kwamba, huu ni msimu mwingine kwa viongozi wanafiki kumkumbuka Mwalimu Nyerere ki-nafiki. Kwa mwaka mwingine tena, watapanda majukwaani, Ijumaa, Oktoba 14 na kumpamba Nyerere na kusifia sera na miongozo yake; huku wakijua mioyoni mwao kwamba si waumini wa kweli wa fikra zake, na kwamba wanachokifanya ni kinyume kabisa na mafundisho yake.

Hata hivyo, unafiki huo wanaoufanya ni kwa madhara ya afya zao wenyewe! Niwakumbushe wanafiki hao maneno ya Yurii katika riwaya ya Doctor Zhivago ya mwandishi mahiri wa kale wa Urusi, Boris Pasternak.

Yurii anasema hivi: Your health is bound to be affected if day after day, you say the opposite of what you feel, if you grovel before what you dislike ”; yaani kwamba utaathirika kiafya iwapo siku hadi siku utazungumza kinyume ya kile unachokiamini.

Kama hivyo ndivyo, basi, nawashauri wanafiki hawa ambao zamani walikuwa wafuasi wa kweli wa Mwalimu Nyerere lakini wakayatosa mafundisho yake baada ya yeye kufariki; kuzijali, basi, afya zao na kuepuka hiyo Ijumaa, Oktoba 14, kuyasifia mafundisho yake na yale yote aliyoyasimamia wakati wa uhai wake; ilhali mioyoni mwao wanajua kwamba hawayaamini!

Ujumbe wangu kwao ni huu: Watakuwa wanazilinda afya zao kama watakuwa wakweli kuhusu waguswavyo na Nyerere. Waache unafiki.

Lakini kwa waumini wa kweli wa Mwalimu Nyerere, niwakumbushe tu kwamba wana kila sababu ya kusimama kijasiri majukwaani na kumtetea Mwalimu kwa nguvu zao zote; maana hata kama alifanya makosa ya hapa na pale, yake yalikuwa ni makosa ya kibinadamu.

Yake hayakuwa ni makosa yaliyochochewa na uchu wa kutajirika zaidi na zaidi katikati ya mamilioni ya watu masikini; kama ilivyo kwa watawala wetu wa sasa.

Nawatakieni nyote maadhimisho mema ya kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha mpendwa wetu, J.K. Nyerere. Tafakari.

1 comment:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Makala imeiva hii. Hata mimi niliwahi kulalamika enzi zile nilipopigwa mikwara baada ya kuweka video za Mwalimu Nyerere katika kibaraza changu. Unaweza kujikumbusha hapa:

http://matondo.blogspot.com/2009/10/mwalimu-nyerere-na-jangwa-lake-la.html

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...