Friday, October 21, 2011

Sehemu za Kupumzikia, Mbamba Bay

Mbamba Bay ni mji mdogo, kando kando ya Ziwa Nyasa, upande wa Tanzania. Ingawa umaarufu wa mji huu tangu zamani ni bandari, hapo ni mahali pazuri kwa mapumziko. Picha ninazoleta hapa nilipiga mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu.

Unaweza kusogea hapo ufukweni, ukawa unapunga upepo na kuangalia shughuli za wavuvi, wauzaji wa samaki, akina mama wakifua nguo, na watoto wakicheza majini. Kama unajua kuogelea, mahali hapo utafafurahia. Ukija siku ambapo meli inakuja, utajionea ujio wa meli na kuondoka kwake.






Kama unapenda kukaa kwenye mwinuko, uangalie mji na Ziwa kwa chini yako, hoteli ya masista panafaa. Habari zake niliandika hapa. Ukipata chumba kinachoangalia upande wa Ziwa, huko nyuma ya hoteli, utafaidi mandhari ya Ziwa na sehemu kadhaa za Mbamba Bay. Ukitoka nje ukaingia bustanini, utapanda mawe na kuliona Ziwa vizuri sana.





Hapo kwenye paa la blue ni baa ya Four Ways, ambayo picha zake niliwahi kuziweka hapa. Mwaka huu, nilipokuwa Mbamba Bay sikupata fursa ya kuingia ndani.










Hapa kushoto niko katika baa ya Bush House na wadau niliokutana nao humo, ambao walitaka tupige picha.

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli ni sehemu nzuri mimi sikupata fursa mwaka huu kufika huko ila mwaka mwingine ni lazima teana mpaka Lundo nilikozaliwa ntafika. Swali la kizushi niliwahi kusikia kuwa kuna mamba huko ziwani na kama umechoka maisha basi ogelea.
Sasa hapo kwenye hiyo picha ya mwisho mbona wengine hawana kinywaji?...LOL

Mbele said...

Ajabu ni kuwa kila ninapokuwa maeneo haya ya Ziwa Nyasa, huwa nasahau kuwa kuna mamba. Labda ni kutokana na raha ya kuliangalia Ziwa na mawimbi yake mazuri na upepo mwanana. Ilikuwa hivyo hivyo nilipokuwa Matema Beach.

Kuhusu hao jamaa kwenye picha, ni kwamba walihama meza yao wakasogea hapa kwangu ili kupiga picha. Ninayo picha nyingine ambamo wako kwenye meza yao na ulabu wao.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...